NA DIRAMAKINI
MTANDAO wa Kutetea Haki za Kidigitali Tanzania (Digital Rights Coalition Tanzania) chini ya uratibu wa Zaina Foundation umeendesha warsha ya wadau katika kujadili na kuichambua Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022 (The Personal Data Protection Act No. 11 of 2022).
Warsha hiyo iliyowaleta pamoja wanachama wa mtandao huo na wadau mbalimbali wakiwemo wanasheria, walimu na wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali imefanyika jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kufungua na kuwakaribisha washiriki wa warsha hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Zaina Foundation ambaye pia taasisi hii ndiyo Sekretarieti ya Mtandao, Zaituni Njovu amesema kwamba, pamoja na malengo mengine warsha hiyo imewakutanisha wadau mbalimbali ili kupitia na kuichambua sheria hiyo iliyopitishwa na Bunge, pia kuziangalia kanuni za utekelezaji wa sheria husika.
Njovu amesema,kwa muda mrefu kumekuwa na kilio cha wadau kutaka uwepo wa sheria hiyo ili kuweza kulinda taarifa binafsi za watu.
Naye Mwanasheria William Kahale ambaye ndiye alikuwa mwezeshaji wa warsha hiyo amesema kwamba, kulikuwa na uhitaji mkubwa wa kuwepo kwa sheria hiyo.
"Kwa hiyo sasa ni fursa kwa wadau kufanya uchambuzi wa kina ili kuangalia ufanisi na taratibu zilizowekwa za utekelezaji wa sheria hii na kanuni zake."
Naye Mwenyekiti wa Digital Rights Coalition Tanzania, Ibrahim Samata wakati akifunga warsha hiyo alimpongeza Zaituni kupitia sekretarieti ya uratibu kwa kuitisha warsha hiyo ambayo kutokana na umuhimu wake inapaswa kupatikana nafasi nyingine zaidi ili washiriki waweze kufanya uchambuzi wa sheria hiyo na kanuni zake.
"Kwani licha ya sheria hii kuwa ni muhimu bado kuna mapungufu kadhaa ambayo yanahitaji kufanyiwa marekebisho ikiwemo sheria hii kuzibeba zaidi taasisi za Serikali huku zile taasisi binafsi zikitakiwa kufuata utaratibu.
"Vile vile kiwango cha faini kwa taasisi za umma kutolingana na taasisi nyingine ikiwemo za watu binafsi."
Samata wakati akifunga mafunzo hayo aliitaka Sekretarieti ya Mtandao chini ya Zaina Foundation kuangalia uwezekano wa warsha kufanyika kwa mara nyingine ili kuwapa fursa zaidi washiriki kuichambua kwa kina na mapendekezo yatakayopatikana basi yawasilishwe serikalini ili kufanyiwa kazi.
Wakati huo huo, washiriki wa warsha hiyo pia waliipongeza Serikali kwa
kutunga sheria hii muhimu na wamesema itakuwa mkombozi katika kulinda au
kuweka ulinzi kwa taarifa binafsi.
Pia, walibainisha wazi kuwa, yapo mapungufu
kadhaa yaliyopo kwenye sheria hiyo na kanuni zake, hivyo yakifanyiwa maboresho itakuwa miongoni mwa sheria bora zaidi nchini.
Tags
Data Protection Act 2022
Digital Rights Coalition Tanzania
Habari
Sheria za Tanzania
Zaina Foundation