Wakili Mkuu wa Serikali Dkt.Luhende atoa wito kwa mawakili wote nchini

NA MWANDISHI WETU

WAKILI Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende ametoa wito kwa Mawakili wote nchini kushiriki maadhimisho ya miaka mitano ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali yatakayoambatana na mafunzo, kwani ni fursa adhimu na ya kipekee.
Dkt. Luhende ameyasema hayo leo Juni 1,2023 jijini Dodoma wakati akizungumza na wandishi wa habari kuelekea maadhimisho hayo ambapo yatafanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete kuanzia Juni 6 hadi 8 huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kasim Majaliwa.

YALIYOJIRI LEO JUNI 1, 2023 WAKATI WAKILI MKUU WA SERIKALI, DKT. BONIPHACE LUHENDE AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI JIJINI DODOMA KATIKA UKUMBI WA IDARA YA HABARI-MAELEZO

#Tarehe 5 Juni, 2023, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inatarajia kuadhimisha miaka mitano tangu ilipoanzishwa tarehe 13 Februari, 2018 ambapo Mgeni Rasmi wa maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

#Maadhimisho hayo yatakuwa na kaulimbiu isemayo, "Miaka Mitano ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali: Tulipotoka, Tulipo na Tunapoelekea", ili ofisi iweze kufanya tathmini ya namna ilivyotekeleza majukumu yake ya uratibu, ushauri, usimamizi na uendeshaji mashauri ya madai na usuluhishi kwa niaba ya Serikali na Taasisi zake ndani na nje ya nchi.

#Maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma na yatahusisha matukio mbalimbali ambapo kutakuwa na mabanda ya maonesho kwa ajili ya kuelimisha umma masuala ya kisheria, mafunzo kwa Mawakili wa Serikali kwa ajli ya kuwajengea uwezo Mawakili hao katika masuala mbalimbali ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kwa weledi mkubwa zaidi.

#Mafunzo haya yatafanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 06 Juni, 2023 hadi tarehe 08 Juni, 2023 na yatahudhuriwa na Mawakili wa Serikali zaidi ya 600 kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara zote, ldara, Taasisi za Serikali, Mikoa pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

#Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imealika wakufunzi wabobevu 24 ambao ni Majaji na Majaji wastaafu kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania, Mahakama ya Rufani, wataalam wabobezi wa Sekta ya Sheria nchini, wakufunzi kutoka vyuo vikuu hapa nchini ambao watatoa mada mbalimbali kwa Mawakili tajwa kuhusu masuala ya sheria ikiwemo uandaaji wa mikataba, masuala ya uwekezaji, mafuta na gesi na usuluhishi wa migogoro kwa njia ya majadiliano.

#Pia, maadhimisho na mafunzo hayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, dini na wadau wengine ikiwa ni pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Mary Makondo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi, viongozi kutoka Taasisi na ldara za Serikali na wadau kutoka sekta ya Mahakama. Natoa rai kwa Mawakili wa Serikali wote kushiriki kimamilifu katika matukio haya.

#Watanzania tuna jambo la kujivunia kwani Mawakili wa Serikali kwa sasa wanaendesha kesi kwenye Mahakama kubwa ikiwemo Baraza la Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji chini ya Benki ya Dunia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news