Wanawake wa Kitanzania 'watekwa' na wageni biashara dawa za kulevya

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imesema kutokana na udhibiti mkubwa wa dawa za kulevya nchini wafanyabiashara wa dawa za kulevya wameendelea kubuni mbinu mpya za usafirishaji wa dawa za kulevya ili kukwepa kukamatwa. 
Hayo yamebainishwa leo Juni 19, 2023 jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo wakati akitoa taarifa ya ukamataji wa dawa hizo mbele ya waandishi wa habari.

"Mamlaka imebaini mbinu hizo na kuchukua hatua. Mbinu mojawapo inayotumika ni raia wa kigeni kuanzisha mahusiano ya kimapenzi na wanawake wa kitanzania zaidi ya mmoja na kuficha dawa za kulevya kwenye makazi ya wanawake hao huku wao wakipanga nyumba tofauti na wanakoishi wapenzi wao. 

"Hali hii husababisha wanawake wa kitanzania kuingia kwenye matatizo makubwa ya kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria huku wanaume wakiwakana wanawake hao,"amefafanua Kamishna Jenerali Lyimo.

Amefafanua kuwa, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imejipanga kikamilifu kupambana na biashara ya dawa za kulevya. 

"Hivyo, wote wanaojihusisha au wenye mpango wa kujihusisha na biashara hiyo, waache mara moja au wajisalimishe wenyewe kabla hawajafikiwa na mkono wa sheria.

"Pia, wananchi wanapaswa kuwa makini na mizigo wanayopewa kubeba au kuhifadhi pasipo kujua ndani yake kuna nini. 

"Wanawake wanatakiwa kuwa makini zaidi kwani katika baadhi ya matukio, wamekuwa wakitumiwa na wapenzi wao hasa raia wa kigeni kusafirisha na kupokea mizigo wasiyoijua na wakati mwingine mizigo hiyo huwa na dawa za kulevya na hivyo hujikuta matatani."

Amesema, kifungu cha 15 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kinaeleza kwamba, ni kosa kusafirisha dawa za kulevya, na mtu yoyote akithibitika kutenda kosa hilo atawajibishwa kisheria ikiwa ni pamoja na kifungo kisichopungua miaka 30 au kifungo cha maisha gerezani.

Pia, amesema Serikali imejipanga ipasavyo kuhakikisha inamaliza tatizo la dawa za kulevya kwa ustawi wa jamii nchini Tanzania. 

Kamishna Jenerali Lyimo amefafanua kuwa, juhudi hizo zinafanyika saa 24 kutokana na kuwepo madhara makubwa ya kiuchumi, kijamii na kisaikolojia yanayotokana na matumizi ya dawa za kulevya.

"Hivyo, ni vema wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa kuwafichua wote wanaojihusisha na matumizi na biashara ya dawa za kulevya ili kwa pamoja tuweze kulikomboa taifa kutoka katika janga hili.

"Aidha, katika kuhakikisha biashara na matumizi ya dawa za kulevya yanatokomea nchini,mamlaka imejikita katika utoaji wa elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya kwa jamii. 

"Ili kupanua wigo wa utoaji elimu, Mamlaka imeingia makubaliano na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutumia klabu zao zilizokwisha anzishwa kwenye shule na vyuo kutoa elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya. Hivyo, elimu ya kupambana na rushwa na dawa za kulevya itatolewa kupitia klabu hizo,"amefafanua Kamishna Jenerali Lyimo.

Maadhimisho

Katika hatua nyingine, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho Siku ya Kimataifa ya kupiga vita dawa za kulevya ambayo kitaifa yatafanyika Juni 25, mwaka huu katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Lengo la siku hiyo ni kuongeza uelewa wa jamii na kuhamasisha umma kushiriki katika mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya ambapo Kamishna Jenerali wa DCEA,Aretas Lyimo amefafanua kuwa, maadhimisho hayo kwa mwaka huu kitaifa yatafanyika kuanzia Juni 23 hadi Juni 25 , 2023 jijini Arusha.

“Maadhimisho haya yataambatana na maonesho ya shughuli mbalimbali za udhibiti zinazofanywa na Mamlaka pamoja na wadau wake katika udhibiti wa dawa za kulevya na utoaji elimu kuhusu tatizo la dawa za kulevya.Mgeni rasmi siku ya kilele tarehe 25 Juni, 2023 ni Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Kauli mbiu ya maadhimisho haya ni “Tuzingatie Utu na Kuboresha Huduma za Kinga na Tiba”. Wananchi wote hususani wakazi wa Arusha na mikoa ya jirani mnakaribishwa kushiriki katika maadhimisho hayo,”amesema.

Kuhusu DCEA

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015. Sheria hii iliifuta Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Kuanzishwa kwa Mamlaka Kulitokana na mapungufu yaliyokuwepo katika mfumo wa udhibiti wa dawa za kulevya.

Mapungufu hayo yalikuwa ni pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya iliyoanzishwa na Sheria ya ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995 kukosa nguvu ya kisheria ya kupeleleza, kufanya uchunguzi na kukamata wahalifu wa dawa za kulevya.

Kutokana na mapungufu hayo, Baraza la Mawaziri katika kikao chake cha tarehe 8 Novemba, 2007 (Waraka Na 60/2007) liliagiza, kurekebisha au kufuta Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995, ili kukidhi matakwa na changamoto za udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya.  

Baraza la Mawaziri liliagiza kuundwa kwa chombo cha kupambana na dawa za kulevya chenye uwezo kiutendaji kwa kukipa mamlaka ya ukamataji, upekuzi na upelelezi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa dawa za kulevya nchini.

Kufuatia agizo hilo, tarehe 24/03/2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kupitisha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015 na kuanza kutumika rasmi tarehe 15 Septemba, 2015 kupitia tangazo la Serikali namba 407 (GN NO.407/2015).

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilianza kutekeleza majukumu yake kikamilifu Februari 17, 2017 baada Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Kamishna Jenerali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news