NA MWANDISHI WETU
WAZEE wameitaka jamii kuepukana na migogoro ya familia inayopelekea kusambararika na kuacha mzigo kwa wazee kulea watoto wanaoachwa.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akimtunuku cheti cha pongezi kwa mchango wake katika jamii mmoja wa wazee wa jiji la Dodoma wakati wa Maadhimisho ya siku ya kupinga ukatili dhidi ya wazee yaliyofanyika kimkoa kwenye kata ya Ihumwa, Juni 15, 2023.
Wito huo umetolewa na baadhi ya Wazee wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukatili Dhidi ya Wazee Juni 15, 2023 katika kata ya Ihumwa Jijini Dodoma.
"Wazazi wengi hawawajibiki kufuatilia matendo ya watoto wao kuanzia asubuhi hadi usiku ni kwa sababu ya wazazi kutengana au kuwa na ugomvi wa mara kwa mara ndani ya nyumba, hali ya Uchumi, Umakini, uzembe ni mfumo uliopo hivi sasa" amesema Mzee Godwin Kadeje mkazi wa kata ya Ihumwa.
Mwenyekiti wa wa Baraza la Ushauri la wazee Mkoa wa Dodoma, Petro Mpolo akisoma risala ya wazee huo, wakati wa Maadhimisho ya siku ya kupinga ukatili dhidi ya wazee kimkoa Juni 15, 2023 katika kata ya ya ihumwa jijini Dodoma.
Aidha Wazee wengine wamewasihi Wazee wenzao kutumia nafasi zao kwenye kuisimamia Maadili badala ya kuwa chanzo cha mmomonyoko wa maadili.
Akisoma risala ya Wazee wa Mkoa wa Dodoma, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoani hapa Petro Mpolo amebainisha kwamba matendo ya ukatili yamepungua kwa kiasi kubwa maeneo mengi japo kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya.
"Pamoja na juhudi zote za Serikali na Wadau Bado vitendo vya ukatili vimeendelea kwa Wazee, lakini hata Wazee wanapotelekezewa wajukuu, huo nao ni unyanyasaji," amesema Mzee Mpolo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na wazee pamoja na wananchi wa kata ya Ihumwa, jijini Dodoma katika Maadhimisho ya siku ya kupinga ukatili dhidi ya wazee yaliyofanyika kimkoa kwenye kata hiyo, Juni 15, 2023.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na Wazee hao amesema Serikali itaendelea kuwashirikisha Wazee katika masuala mbalimbali ya Maendeleo kwani wana mchango mkubwa katika kuendeleza Taifa.
"Nimeona mchango wa Wazee kwenye kulea Jamii hata pale ambapo watoto wao hawawajibiki Wazee wamesimama, tuna Wazee wengi wameendelea kufanya mambo mazuri kwenye Jamii, kutunza upendo kwa watoto wao, suala la kutelekezewa watoto tutalifanyia kazi. Nafurahi kuona baadhi ya Wazee hawajachoka kulea Jamii kwa upendo ingawa baadhi ya Jamii zinawakatili," amesema Dkt. Gwajima.
Baadhi ya wazee na wananchi walioshiriki maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukatili Dhidi ya Wazee katika mkoa wa Dodoma kwenye kata ya Ihumwa, wakifuatilia matukio yanayoendelea wakati wa maadhimisho hayo Juni 15, 2023.
Katika hatua nyingine Waziri Dkt. Gwajima amewatunuku vyeti wazee wanne kutoka kata ya Mkonze jijini Dodoma kutokana na kutambua mchango wao kwenye jamii zao.
Mkurugenzi wa Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI,Subisya Kabuje akitoa salaam za ofisi hiyo kwa wazee, katika maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukatili Dhidi ya Wazee Juni 15, 2023, kwenye kata ya Ihumwa jijini Dodoma yalipofanyika kimkoa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Subisya Kabuje amewapongeza Wadau wote wanaopaza sauti kupinga Ukatili Dhidi ya Wazee nchini na kutoka Rai waendelee kushirikiana na Serikali kwa Ustawi wa Wazee.