NA MUNIR SHEMWETA-WANM
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula amewataka viongozi wa dini nchini kuwakumbusha mara kwa mara waumini pamoja na watu wote umuhimu wa kusimamia haki na kudumisha amani.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt. Angeline Mabula akiongozwa na viongozi wa Kanisa la Waadventista Sabato kuelekea kupanda mti kwenye eneo la Kanisa hilo Kwembe Dar es Salaam tarehe 18 Juni 2023.
Dkt. Mabula alisema hayo wakati akifungua Siku Kuu za Makambi za Kanisa la Waadventista Wasabato Mtaa wa Magomeni Mwaka 2023 iliyofanyika Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam.
"Amani ni suala muhimu na bila amani hakuna maendeleo hivyo basi hatuna budi kusimamia haki, kuenzi pamoja na kuitunza amani yetu kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo,’’ alisema Dkt.Mabula.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi aliyekuwa Mgeni rasmi kwenye Ufunguzi huo wa Makambi mwaka 2023, kwa sasa dunia imekuwa na mabadiliko makubwa mengine yakiendana na mafundisho ya dini huku mengine yakiwa hayamtukuzi mungu na kutolea mfano jinsi ya mioyo ya watu ilivyobadilika.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Makambi ya Kanisa la Waadventista Sabato Mtaa wa Magomeni 2023 uliofanyika Manispaa ya Dar es Salaam tarehe 18 Juni 2023.
‘’Wivu, chuki, husuda na mambo ya aina hiyo yanachangia kusambaratika kwa familia, marafiki na hata jamii kwa ujumla na mambo hayo yameongezeka sana, wakati mwingine mambo kama haya yanafikia kuleta mauaji katika jamii,’’ alisema Dkt. Mabula.
Alitoa rai kwa madhehebu ya dini kuelekeza kufundisha yaliyo mema ili jamii ifuate mapenzi ya mungu na kuepuka kujiingiza kwenye machukizo kwa mungu huku akilishukuru Kanisa la Waadventista Sabato Tanzania kwa kuweka wazi msimamo na masharti kwa yale mambo yanayoenda kinyume na maadili ya mtanzania na kubainisha kuwa msimamo huo ukifuatwa utalisaidia kanisa na jamii kwa ujumla.
Sehemu ya washiriki wa ufunguzi wa Mkutano wa Makambi ya Kanisa la Waadventista Sabato Mtaa wa Magomeni 2023 uliofanyika Dar es Salaam tarehe 18 Juni 2023.
Aliwaomba viongozi hao wa dini kutochoka kufundisha na kulea vijana katika maadili mema pamoja na kuthamini kufanya kazi halali huku akitahadharisha kuwa kushuka kwa maadili ni jambo lenye athari mbaya kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula akizungumza kabla ya kwenda kupanda mti kwenye eneo la Kanisa la Waadventista Sabato Kwembe Manispaa ya Ubungo Dar es Salaam tarehe 18 Juni 2023.
Waziri wa Ardhi, aliwataka viongozi wa dini kusaidia kulea vijana kwa sababu wao wao ndiyo wahanga wakuu wa maovu yanayotendeka lakini pia wao ndiyo taifa la leo na viongozi na wachungaji wa kesho.
‘’Tukiwandaa vyema vijana, mustakabali wa Taifa letu na watu wake utakuwa kwenye mikobno salama tu, tukishindwa leo tutalia na kusaga meno,’’ alisema Dkt.Mabula.
Sehemu ya washiriki wa ufunguzi wa Mkutano wa Makambi ya Kanisa la Waadventista Sabato Mtaa wa Magomeni 2023 uliofanyika Dar es Salaam tarehe 18 Juni 2023.
Kanisa la Waadventista Sabato Magomeni limekuwa na utaratibu wa kuwa na Makambi kila mwaka kwa lengo la kutoa mafundisho kwa waumini wake na kwa mwaka huu wa 2023 mkutano huo umebeba ujumbe usemao ‘NITAKWENDA KUJIHUSISHA’.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt.Mabula ameshiriki kupanda miti eneo la uwekezaji la Kanisa Waadentista Sabato lenye ukubwa wa ekari 20 lilipo Kwembe Dar es Salaam.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Dkt. Angeline Mabula akipanda mti kwenye eneo la Kanisa la Waadventista Sabato lilipo Kwembe Manispaa ya Ubungo Dar es Salaam mara baada ya kufungua Mkutano wa Makambi Mtaa wa Magomeni 2023 tarehe 18 Juni 2023.
Kwa mujibu wa Israel Kamuzora ambaye ni mmoja wa Wazee wa Kanisa hilo, uwekezaji utakaofanywa eneo hilo utahusisha mambo mbalimbali kama vile kuwa na Ukumbi, Hosteli, Shule za Muziki, Makumbusho ya Kanisa, Chuo cha Mapishi Bora, Hospitali ya Mama na Mtoto pamoja na Maktaba kubwa ya Kanisa.
‘’Eneo hili tutalitumia kama eneo la uwekezaji wa Kanisa letu maana tutajenga ukumbi wa mkutano wenye uwezo wa kuchukua watu 3,000, Hostel watu 500, Shule ya Muziki pamoja na eneo la Makumbusho,’’ alisema Kamuzora.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ,Dkt.Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Kanisa la Waadventista Sabato alipokwenda kufungua Mkutano wa Makambi wa Kanisa hilo Mtaa wa Magomeni 2023 jijini Dar es Salaam tarehe 18 Juni 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).
Kwa upande wake Waziri wa Ardhi, Dkt.Mabula amelipongeza Kanisha la Waadventina Sabato kwa kwa jitihada mbalimbali inazofanya ikiwemo kuwa na malengo ya kuanzisha uwekezaji eneo la Kwembe alioueleza kuwa, utakaposimamiwa vizuri kwa kiasi kikubwa utagusa wananchi.