Waziri Dkt.Mwigulu: BoT imepanga kukuza wastani ukuaji ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3)

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (MB) amesema,kwa mwaka 2023/24, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imepanga kukuza wastani wa ukuaji wa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) kwa kiwango kisichopungua asilimia 10.

Mheshimiwa Waziri ameyasema hayo Juni 7, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha bungeni Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka 2023/24.

"Lengo ni ili kuendana na mahitaji ya shughuli za kiuchumi, kuboresha mazingira ya kuchochea ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi.

"Pia, kudhibiti na kupunguza kiwango cha mikopo chechefu pamoja na kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayotosheleza mahitaji ya kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi kisichopungua miezi minne,"amefafanua Waziri Dkt.Mwigulu.
 
Awali, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu amebainisha kuwa, katika mwaka 2022/23, Benki Kuu ya Tanzania ilipanga kuchochea na kudhibiti ustawi wa viashiria vya uchumi jumla.

Pia kukuza wastani wa ukuaji wa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) ili kuendana na mahitaji ya shughuli za kiuchumi.

Sambamba na kuchochea ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi, kudhibiti na kupunguza kiwango cha mikopo chechefu na kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayotosheleza mahitaji ya kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi kisichopungua miezi minne.

Waziri Dkt.Mwigulu amesema,hadi Aprili 2023, wastani wa ongezeko la ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) ulikua kwa asilimia 17.2 dhidi ya lengo la asilimia 10.3,na mfumuko wa bei ulifikia asilimia 4.3 ikilinganishwa na lengo la asilimia 5 hadi 7.

Aidha, mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa asilimia 22.5 ikilinganishwa na lengo la asilimia 10.7. "Mwenendo mzuri wa ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi umetokana na kuimarika kwa mahitaji ya mikopo mipya kufuatia hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji na biashara na usimamizi imara wa sera za fedha na bajeti.

"Kiwango cha mikopo chechefu kilipungua kufikia asilimia 5.5 dhidi ya lengo la asilimia 5. Vilevile, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa katika viwango vya kutosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi katika kipindi kisichopungua miezi minne,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu amesema, kwa mwaka 2023, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania imepanga kuzalisha mapato ya shilingi bilioni 45.1 kukuza faida ya benki kabla ya kodi ya shilingi bilioni 18.5.

Na kutoa mikopo ya shilingi bilioni 336.7, kukuza mali za benki ili kufikia shilingi bilioni 562.7 na kufuatilia urejeshaji wa mikopo kutoka kwa wateja shilingi bilioni 62.

"Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2023, Benki ya Maendeleo ya TIB imepanga kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 51 kwa miradi ya maendeleo kwenye sekta za maji, nishati na uongezaji thamani mazao ya kilimo, kukusanya shilingi bilioni 39.6 za marejesho ya mikopo kutoka kwa wateja, kukusanya shilingi bilioni 57 za marejesho ya mikopo iliyoshindikana na kuondolewa kwenye mizania ya benki.

"Katika mwaka 2023, Benki ya Biashara Tanzania imepanga kuzalisha mapato ya shilingi bilioni 184.2, kukuza faida ya benki kabla ya kodi ya shilingi bilioni 12.4, kutoa mikopo ya shilingi bilioni 904, kukusanya amana za wateja shilingi bilioni 1,121,kukuza mali za benki ili kufikia shilingi bilioni 1,446,kukuza mtaji kufikia shilingi bilioni 123.8 na kuunda mfumo wa kielektroniki wa tathmini na ufuatiliaji wa mwenendo wa mikopo inayotolewa na benki,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu.

Bima

Akizungumzia kwa upande wa taasisi za bima, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu amelieleza Bunge kuwa,kwa mwaka 2023/24,Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) inatarajia kufanya uchambuzi wa mikataba ya bima mtawanyo kwa kampuni 32.

Sambamba na kufanya ukaguzi wa wadau wa bima,kuandaa mwongozo wa bima za kilimo, kuhamasisha kampuni za bima kuandaa bidhaa za sekta ya kilimo pamoja na kupokea na kushughulikia malalamiko ya wateja wa bima.

"Aidha, Shirika la Taifa la Bima linatarajia kukamilisha taratibu za kupata uthibitisho wa cheti cha ubora cha utoaji huduma kwa wateja (ISO 9001 2015), kuongeza wateja wapya 116 wa bidhaa za taasisi na kubuni bidhaa tatu mpya zitakazokidhi mahitaji ya soko,"amefafanua.

Uwekezaji

Mbali na hayo,Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwingulu amelieleza kuwa,katika mwaka 2023/24,Kampuni ya Uwekezaji wa Pamoja -UTT AMIS inatarajia kuongeza rasilimali za mifuko kwa kiwango cha asilimia 15, kuongeza idadi ya wawekezaji kwa asilimia tano na kuhamasisha taasisi za Serikali, Mifuko ya Hifadhi za Jamii, Mashirika na vikundi mbalimbali vya kijamii kama vile SACCOS kujiunga na mifuko ya UTT AMIS.

Aidha,amesema Mfuko wa SELF unatarajia kutoa mikopo yenye masharti nafuu ya shillingi bilioni 44.8 kwa wajasiriamali 38,000,kufuatilia urejeshaji wa mikopo usipungue asilimia 95 na kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa walengwa au wanufaika 5,500.

Kupitia hotuba hiyo, Wizara ya Fedha na Mipango imeomba ridhaa ya Bunge kutumia jumla ya shilingi trilioni 15.94 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo kwa mafungu yake tisa ya kibajeti.

Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 15.38 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 564.22 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

"Aidha, ninaomba Bunge lako Tukufu liidhinishe shilingi bilioni 97.13 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Fungu 45-Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 87.72 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 9.41 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo,"amebainisha Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news