Waziri Dkt.Tax amwakilisha Rais Dkt.Samia mkutano wa ICGLR

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 10 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) uliofanyika jijini Luanda, Angola leo Juni 3, 2023.
Mkutano huo wa dharura ulitanguliwa na Mkutano wa Mawaziri uliofanyika tarehe 2 Juni, 2023 umejadili na kuangalia hali ya amani na usalama katika katika Ukanda wa Maziwa Makuu hasa katika nchi za Jamhuri ya Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mkutano huo umeitishwa na Rais wa Angola na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) Mheshimiwa Joao Manuel Lourenco ikiwa ni utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa 16 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika mwezi Mei 2022 jijini Malabo, Equatorial Guinea. 
Mwezi Julai 2022, Jumuiya ya Kikanda ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) ilitoa Mpango wa Mchakato wa Mazungumzo ya Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo uliolenga kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na kisiasa na kujiridhisha kuhusu tuhuma mbalimbali zinazotolewa hususan ushirikiano wa Serikali ya Rwanda na kikundi cha M23 na ushirikiano wa Serikali ya DRC na kikundi cha FDLR. 
Mkutano huo pia umehudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Felix Antoine Tshisekedi Tshilombo; Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Mhe. Faustine Archange Touadera na viongozi wengine ambao waliwawakilisha marais wa nchi zao ambao ni Makamu wa Rais wa Uganda Mhe. Jessica Rose Alupo Epel; Waziri Mkuu wa Rwanda Mhe. Eduoardo Ngirente, Waziri wa Kenya Mhe. Musalia Mudavadi; Waziri Ofisi ya Rais wa Sudani Kusini Mhe. Barnaba Marial Benjamin; Waziri wa Mambo ya Nje wa Congo Mhe. Jean Cloude Gakosso; Waziri wa Ulinzi wa Zambia Mhe. Ambrose Lufuma; Mjumbe Maalumu wa Serikali ya Jamhuri ya Sudan Mhe. Balozi Daffa Alla Elhag Al Osman; Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Mhe. Moussa Faki Mahamat na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Innocent Bashungwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news