NA LUSUNGU HELELA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewapongeza Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zilizopiga hatua katika maendeleo ya kidijitali huku akiwataka Watumishi hao kujiimarisha zaidi kwenye ubunifu.
Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao kilicholenga kuhimiza uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Mhandisi Benedict Ndomba akielezea majukumu ya taasisi yake kwa viongozi wakuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakiongozwa na Waziri Mhe. George Simbachawene.
"Katika dunia ya sasa maendeleo ya nchi yamekuwa yakipimwa kwa kuangalia endapo nchi inatumia mifumo ya kidigitali katika kuendesha mambo yake," amesema Mhe.Simbachawene.
Aidha, Mhe.Simbachawene ameutaka uongozi wa eGa kuendelea kuwekeza kimkakati kwa watumishi kwa kuwawezesha kwenda kusoma katika nchi zilizopiga hatua zaidi kwenye masuala ya kidijitali.
"Nimeambiwa kuna baadhi ya watumishi wanasoma hapa nchini, natamani kuona idadi kubwa zaidi ya watumishi wanawake na wanaume wanakwenda kusoma nchi za nje hususani katika nchi zilizotuzidi kwenye masuala haya" amesisitiza Mhe.Simbachawene.
Katika hatua nyingine, Mhe. Simbachawene ameitaka Mamlaka hiyo kujitangaza ipasavyo ambapo amesema, licha ya mifumo mingi ya kidigitali inayotumiwa na Taasisi za Serikali kubuniwa na Mamlaka hiyo na kupelekea kuokoa fedha nyingi za Serikali lakini Mamlaka hiyo haiyatangazi mafanikio hayo kwa Umma.
"Nataka mtoke muwaeleze Watanzania mmetekeleza kwa kiasi gani Ilani ya CCM (2020 - 2025) na pia mmeisaidia kwa kiasi gani Serikali katika kutumia mifumo ya kidigitali hususan katika kuwahudumia wananchi," Mhe. Simbachawene amesisitiza.
Kwa upande wake Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewapongeza watumishi wa eGA kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kubuni mifumo mbalimbali ya kidigitali yenye tija kwa taifa na kuwasisitiza kujitangaza zaidi ili wananchi wajue kwa kina shughuli zinazofanywa na Mamlaka hiyo.
Naye, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amewataka watumishi wa umma kuzingatia maadili ya utendaji katika utumishi wa umma huku akiwasisitiza kutunza siri katika mifumo ya kidigitali ambayo Serikali inaitumia katika kuwahudumia wananchi.