Wiki tamu, chungu wengi 'thank you'

NA DIRAMAKINI

WIKI hii inaonekana kuwa ya moto zaidi katika klabu na timu mbalimbali ambazo zinashiriki Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara ambapo, wengi wameshuhudia na kuona mikataba ikivunjwa, vigogo wakigomea kuongeza mikataba na wengine kudaiwa kupewa dau nono ili kwenda kukipiga nje ya nchi.

Mbali na hayo, nyota mbalimbali wametwaa tuzo huku baadhi ya timu zikijinasua kushuka daraja na nyingine kupigwa bei.

Tuanzie na Yanga SC

Uongozi wa klabu ya Yanga umetangaza kuachana na kocha wake Nasredeen Mohamed Nabi kufuatia Mtunisia huyo kukataa kuongeza mkataba baada ya kumaliza.

Nabi hakushinda taji katika msimu wake wa kwanza tu Yanga, lakini miwili iliyofuatia alibeba mataji yote, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC).

Aidha, msimu huu amewafikisha pia Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambako walishindwa na USM Alger kwa mabao ya ugenini baada ya sare ya jumla ya 2-2, wakifungwa 2-1 jijini Dar es Salaam na kushinda 1-0 Algiers nchini Nigeria.

Wakati huo huo,Yanga SC imeachana na kocha wake makipa,Milton Nienov raia wa Brazil baada ya misimu miwili ya kufanya kazi kwa mafanikio.

Mbrazil huyo aliyewahi kufanya kazi kwa watani, Simba anamfuatia kocha Mkuu, Nasredine Nabi ambaye aligoma kuongeza mkataba kwa klabu hiyo ya jijini Dar es Salaam.

Mayele

Wakati huo huo, mshambuliaji wa Kimataifa, Fiston Kalala Mayele wa Klabu ya Yanga kuna fununu huenda akaingia kandarasi la zaidi ya shilingi bilioni mbili na mmoja wapo ya vilabu huko Uarabuni.

Mayele ni miongoni mwa wachezaji bora zaidi ambapo ameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara msimu wa 2022-2023.

Kupitia usiku wa sherehe za tuzo hizo hivi karibuni jijini Tanga, ulikuwa usiku mzuri kwa mabingwa wa Ligi Kuu ya NBC, Yanga SC ambayo imebeba tuzo nyingine ikiwemo Mayele kuchukua pia ya Ufungaji Bora kwa pamoja na kiungo Mrundi wa Simba, Saido Ntibanzokiza baada ya wote kumaliza na mabao 17.

Mayele aliondoka na tuzo tatu, pamoja na ya Bao Bora la msimu kutokana na bao lake alilofunga kwenye mechi dhidi ya Mtibwa Sugar.

Tena

Kiungo mshambuliaji wa Klabu ya Simba, Saido Ntibazonkiza ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa kiungwana (Fair Play) katika hafla ya tuzo za TFF zilizofanyika jijini Tanga.

Ntibazonkiza alipata tuzo hiyo baada ya kuwapiku Pape Sakho na Jean Baleke aliokuwa akishindana nao kwenye kinyang’anyiro hicho.

Aidha, Ntibazonkiza alishinda tuzo hiyo baada ya kumzuia mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele kwenda kumrudishia Mzamiru Yassin aliyekuwa amemfanyia madhambi katika mchezo wa Derby ya Kariakoo uliofanyika Aprili 16, mwaka huu.

Pia, mshambuliaji Said Ntibazonkiza alikabidhiwa tuzo yake ya mchezaji bora wa mashabiki wa mwezi Mei (Emirate Aluminium Profile Simba Fans Player of the Month).

Ntibazonkiza alikabidhiwa tuzo hiyo baada ya kuwashinda walinzi Shomari Kapombe na Henock Inonga ambao alikuwa ameingia nao fainali ya kinyang’anyiro hicho.

Baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Ntibazonkiza aliwashukuru wadhamini Emirate Aluminium Profile, wachezaji wenzake na mashabiki kwa kufanikisha kuibuka mshindi.

Ntibazonkiza alisema, tuzo za Emirate zinaongeza hamasa kwa wachezaji na kujitoa kwa kila hali kuisaidia timu kupata matokeo chanya uwanjani.

“Nawapongeza Emirate Aluminium Profile kwa kuona umuhimu wa hii tuzo kwetu. Tuzo hii inaongeza chachu ya kila mtu kujituma kuipa timu mafanikio.

“Nalishukuru benchi la ufundi kwa kunipa nafasi, wachezaji wenzangu kunipa ushirikiano uwanjani pamoja na mashabiki kwa kunipigia kura, naomba tuendelee na utaratibu huu msimu ujao,”alisema Ntibazonkiza.

Aidha, Said Ntibazonkiza alikabidhiwa fedha taslimu shilingi 2,000,000 na tuzo kutoka kwa wadhamini Emirate Aluminium Profile.

Naye mshambuliaji Jentrix Shikangwa alikabidhiwa tuzo yake ya mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Serengeti Lite Women’s Premier League (SLWPL) 2022/23.

Shikangwa alikabidhiwa kiatu cha dhahabu katika hafla ya tuzo za TFF 2022/23 zilizofanyika jijini Tanga, Shikangwa pia alichaguliwa katika kikosi bora cha SLWPL msimu wa 2022/23.

Wachezaji wengine walioingia kwenye kikosi bora cha msimu ni pamoja na walinzi Fatuma Issa ‘Fetty Densa’ na Violeth Nicholas.

Mauzo

Mbali na hayo, uongozi wa Singida Big Stars FC umefanya makubaliano ya kibiashara ya kuuza hisa zake kwa uongozi wa Fountain Gate Academy.

Makubaliano hayo yameambatana na baadhi ya mabadiliko katika uendeshaji wa klabu kwa upande wa Bodi na Menejimenti.

Kutokana na mauziano hayo, sasa Singida Big Stars FC itafahamika kama Singida Fountain Gate FC na jina la utani la ‘The Big Stars’ kwa wenyeji hao wa mkoani Singida.

Azam FC yatimua

Nao Azam FC wameachana na makocha wake, Kocha wa makipa Mspaniola Dani Cadena na kocha wa Fiziki, Mtunisia Dkt.Moadh Hiraoui na aliyekuwa Kaimu kocha wake Mkuu, Muingereza mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kalimangonga Ongala.

Makocha hao wanaondoka kupisha wasaidizi wapya watanaoletwa na kocha mpya, Msenegal Youssouph Dabo ambaye ataanza kukiandaa kikosi kwa ajili ya msimu ujao.

Pia, Azam FC imeachana na nyota wake watatu wa kigeni, beki Mzimbabwe Bruce Kangwa, kiungo Mkenya, Kenneth Muguna na mshambuliaji Mzambia, Rodgers Kola na wazawa Ismail Aziz Kader na Cleophace Mkandala.

Wakati huo huo, Azam FC imeachana na Kocha wake Msaidizi, Aggrey Morris baada ya kuitumikia klabu tangu mwaka 2009 akianza kama mchezaji kabla ya kuingia kwenye benchi la ufundi msimu huu.

"Ahsante sana kwa mchango wako ndani ya klabu yetu ukiwa kama nahodha, kocha msaidizi. Ulikuja Azam FC ukiwa mdogo sana mwaka 2009 kama mchezaji hadi leo unaondoka ukiwa sehemu ya benchi letu la ufundi," imeeleza sehemu ya taarifa ya Azam FC.

Simba SC

Nayo Klabu ya Simba imeachana na kocha wa makipa,Chlouha Zakaria kutoka nchini Morocco baada ya kufanya kazi kwa msimu mmoja tangu arithi mikoba ya mzawa, Muharami Mohamed (Shilton)."Tunakutakia kila la kheri katika maisha yako mapya nje ya Simba."

Aidha, Simba SC imeachana na makocha wake wa Fiziki, Kelvin Mandla Ndlomo na Fareed Cassiem wote raia wa Afrika Kusini baada ya msimu mmoja wa kuwa kazini huku klabu ikiambulia patupu.

Katika hatua nyingine Klabu ya Simba imeachana na kocha wake wa timu yake ya wanawake,Charles Lukula raia wa Uganda baada ya kuwa kazini kwa msimu mmoja.

Tupo

Mbali na hayo, vijana wa Kinondoni (KMC FC) chini ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jiijini Dar es Salaam imefanikiwa kusalia Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Mbeya City.

Ni baada ya kumenyana Juni 16, 2023 katika dimba la Uhuru lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

KMC walivushwa kupitia mchezo huo wa marudiano wa mchujo wa kukwepa kuteremka daraja baada ya mabao ambayo yalifungwa na Daruwesh Saliboko dakika ya tatu na Awesu Awesu dakika ya 28.

Hata hivyo, KMC inabaki Ligi Kuu kwa ushindi wa jumla wa 3-2 kufuatia kufungwa 2-1 kwenye mchezo wa kwanza jijini Mbeya na sasa Mbeya City itakwenda kumenyana na Mashujaa ya Kigoma kujaribu tena kubaki Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news