Wizara ya Afya yakabidhi magari kusaidia shughuli za maji na usafi

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imekabidhi magari sita yenye thamani ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya kusaidia shughuli za maji na usafi wa mazingira katika mikoa ya Shinyanga, Lindi, Simiyu, Katavi, Singida na Ruvuma. 
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe leo Juni 9, 2023 amekabidhi magari hayo katika ofisi za Wizara ya Afya jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga aliyewawalikisha Makatibu tawala wengine pamoja na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Kheri Kagya.

Katika makabidhiano hayo, Dkt. Shekalaghe amesema hii ni awamu ya pili ya utoaji wa magari hayo ambapo awamu ya kwanza yalitolewa Sita, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kutoa magari zaidi kwaajili ya uratibu wa shughuli za maji na usafi wa mazingira utakaosaidia kukabiliana na magonjwa mbalimbali kwa wananchi.
Sambamba na hilo Dkt. Shekalaghe ametoa wito kwa wananchi wa kusafisha mazingira pamoja na kutunza vyanzo vya maji ili kuepuka magonjwa hasa magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa kipindupindu na kuumwa tumbo.

Aidha, Dkt. Shekalaghe amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya Waziri wa Afya, kutokana fedha nyingi anazotoa kwaajili ya maboresho ya Sekta ya Afya ikiwemo vifaa tiba, magari, miundombinu pamoja na fedha za uratibu wa mapambano dhidi ya magonjwa. 
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Prof. Siza Tumbo amemshukuru Rais Dkt. Samia kupitia Wizara ya Afya kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za mapambano dhidi ya magonjwa katika Mkoa wa Shinyanga kupitia magari hayo yatayosaidia katika uratibu wa shughuli mbalimbali ikiwemo ya elimu dhidi ya magonjwa na masuala ya maji na usafi wa mazingira. 
Amesema, licha ya mkoa wa Shinyanga kuendelea kufanya vizuri kwenye masuala ya usafi wa mazingira gari hili litasaidia kuongeza kasi zaidi ya utoaji elimu juu ya maji na usafi wa mazingira pamoja na shughuli nyingine ili kuwakinga wananchi dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo ya tumbo na kipindupindu. 
Nae, Mratibu wa masuala ya maji na usafi wa mazingira Wizara ya Afya, Bw. Anyitike Mwakitalime amesema mradi wa huduma endelevu za maji na usafi wa mazingira nchini unatekelezwa katika mikoa 17 na Halmashauri 86 ambapo mpaka sasa shughuli za ujenzi wa na matumizi ya vyoo bora umefikia 74% ya kaya zenye vyoo bora huku kwenye upande wa vituo vya huduma za afya uboreshaji wa miundombinu ya maji ukiendelea hususan katika vyoo na sehemu za kunawia mikono pamoja vichomea taka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news