Wizara ya Fedha yajiwekea vipaumbele nane 2023/24

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (MB) amesema, kwa mwaka 2023/24 wizara hiyo imejiweekea vipaumbele nane.
Mheshimiwa Waziri ameyasema hayo Juni 7, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha bungeni Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka 2023/24.

Amesema kuwa, maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka 2023/24 yamezingatia miongozo mbalimbali ya kisera ya wizara, kitaifa, kikanda na kimataifa. 

Miongozo hiyo ni pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22-2025/26,Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/24, Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2023/24.

Pia kuna Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020, Hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati wa Uzinduzi wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria ya Bajeti,Sura 439 pamoja na kanuni zake.

Aidha, kuna mikakati na makubaliano mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa,Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa Awamu ya Tatu, Mpango Mkakati wa Wizara wa Miaka Mitano 2021/22-2025/26 na masuala mtambuka ikijumuisha jinsia, lishe, mazingira, mabadiliko ya tabia nchi, na UKIMWI.

Vipaumbele

"Mheshimiwa Spika, vipaumbele vya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka 2023/24 ni kama ifuatavyo;

i. Kutafuta na kukusanya mapato ya shilingi trilioni 40.8 kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti ya Serikali;
ii. Kuhudumia deni la Serikali;
iii. Kufanya tafiti, tathmini na mapitio mbalimbali yakitaalamu kuhusu mifumo ya usimamizi wa mipango,uchumi na bajeti ya Serikali;
iv. Kujenga, kuboresha, kufungamanisha na kuhuishamifumo ya TEHAMA ya usimamizi wa mapato na matumizi ya Serikali;
v. Kujenga uwezo wa watumishi kuhusu usimamizi wa masuala ya sera, uchumi, mipango na fedha;
vi. Kuboresha miundombinu ya ofisi za Wizara na taasisi zake pamoja na miundombinu ya kufundishia na kujifunzia;
vii. Kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo inayotekelezwa na Wizara na Serikali kwa jumla; na
viii. Kukamilisha maboresho ya Sheria ya Msajili wa Hazina."
Waziri Dkt.Mwigulu akizungumzia vipaumbele vya Mpango na Bajeti kwa Fungu 45-Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi amesema ni kufanya ukaguzi wa rasilimali za umma kwa Serikali Kuu, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma; kufanya kaguzi za kiufundi,ufanisi, maalum, kiuchunguzi, miradi ya maendeleo na mifumo ya TEHAMA.

Pia, kuimarisha matumizi ya TEHAMA ndani ya Ofisi na kuendelea na ujenzi na ukarabati wa Ofisi za Ukaguzi mikoani.

Vipaumbele vya Taasisi

"Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza awali, baadhi ya majukumu ya wizara yanatekeleza kupitia taasisi za elimu, bodi za kitaalamu na kitaaluma, usimamizi na udhibiti wa masuala ya fedha, kodi, bima, ununuzi na ugavi, michezo ya kubahatisha, uwekezaji na uwezeshaji pamoja na takwimu,"amesema.

Elimu

Akizungumzia kwa upande wa taasisi za elimu, amesema Wizara ya Fedha na Mipango inasimamia jumla ya taasisi za elimu tano ambazo ni Chuo cha Usimamizi wa Fedha, Taasisi ya Uhasibu Tanzania, Chuo cha Uhasibu Arusha, Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, na Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika. 

Waziri Dkt.Mwigulu amesema, kwa mwaka 2023/24, vyuo vyote vinatarajia kudahili jumla ya wanafunzi 77,432, ikijumuisha ngazi ya cheti 14,108, stashahada 18,744, shahada 41,483 na uzamili 397.

Pia amefafanua kuwa, katika mwaka 2023/24, Chuo cha Usimamizi wa Fedha kimepanga kukamilisha ujenzi wa Kampasi ya Geita, kuanza ujenzi wa awamu ya pili wa Kampasi ya Simiyu.

Ni kupitia Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Juu kwa Ajili ya Mageuzi ya Kiuchumi na kuendelea na ujenzi wa jengo la taaluma likijumuisha ofisi zenye uwezo wa kuhudumia wahadhiri 40 na madarasa yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,520 kwa wakati mmoja katika kampasi ya Mwanza.

"Katika mwaka 2023/24, Chuo cha Uhasibu Arusha kinatarajia kuendeleza watumishi 45 katika ngazi ya Shahada, Uzamili na Uzamivu ndani na nje ya nchi, kupitia mitaala 10 pamoja na kuandaa mitaala mipya miwili, kufungua kampasi mpya ya Songea mkoani Ruvuma.

"Kuanza ujenzi katika kampasi ya Dodoma, kufanya tafiti mbili na kutoa ushauri wa kitaaluma, kuanza ujenzi wa kituo cha TEHAMA katika kampasi ya Arusha na kuanza ujenzi wa jengo la taaluma na maktaba katika kampasi ya Songea."

Aidha, kwa upande wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Waziri Dkt.Mwigulu amesema kimepanga kukamilisha ujenzi wa bweni la wanafunzi na ukumbi wa mihadhara na kuanza ujenzi wa jengo la utawala katika kampasi ya Dodoma, kuanza ujenzi wa kituo cha mafunzo katika eneo la Nala Dodoma, kukamilisha ujenzi
wa bweni, maktaba na kuanza ujenzi wa bweni la wanafunzi katika Kituo cha Mafunzo-Mwanza. 

"Aidha, chuo kinatarajia kufanya tafiti 10 na kutoa huduma za ushauri elekezi kwa kuzingatia mahitaji ya wadau."

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/24, Taasisi ya Uhasibu Tanzania itaendelea na ujenzi wa jengo moja linalojumuisha ukumbi wa mihadhara,maabara ya kompyuta na maktaba katika Kampasi ya Mbeya.

"Jengo la taaluma Misungwi-Mwanza, vyumba vya madarasa manne, maktaba, maabara ya kompyuta na nyumba ya watumishi na hosteli mbili za wanafunzi wa kike na wa kiume kampasi ya Mtwara, jengo la taaluma katika kampasi ya Kigoma na kuanza ujenzi wa jengo la taaluma katika kampasi ya Zanzibar."

Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu amesema, katika mwaka 2023/24, Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika kimepanga kuendelea na ujenzi wa jengo la utawala, kuendeleza wahadhiri 28 na kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi 20.

Mheshimiwa Waziri ameendelea kufafanua kuw,a katika mwaka 2023/24, Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu inatarajia kusajili wahasibu 1,350 katika ngazi mbalimbali, kuanza ujenzi wa ofisi ya Makao Makuu jijini Dodoma, kufanya ukaguzi wa ubora wa uandaaji wa taarifa za fedha kwa taasisi 75.

Pia,kufanya ukaguzi wa ubora wa kampuni 65 za ukaguzi,kuendesha mitihani ya kitaaluma kwa watahiniwa 12,500 na kutoa mafunzo ya diploma ya viwango vya uandaaji wa taarifa za fedha serikalini kwa wahitimu 350. 

"Aidha,Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi inatarajia kusajili wataalamu 3,500 wa ununuzi na ugavi,kuendesha mafunzo na ushauri wa kitaalamu kwa wataalamu 6,500 na kuendesha mitihani ya kitaaluma kwa watahiniwa 4,000."

Kodi

Akizungumzia kwa upande wa taasisi za usimamizi wa masuala ya kodi, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu amefafanua kuwa, katika mwaka 2023/24, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajia kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya jumla ya shilingi trilioni 26.7.

Mipango mingine ya mamlaka hiyo ni kuendelea kuimarisha na kuboresha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato, kuwajengea uwezo wafanyakazi, kutoa elimu ya kodi na kuendelea kudhibiti uvujaji na upotevu wa mapato. 

Aidha, amesema Bodi ya Rufaa za Kodi, Baraza la Rufaa za Kodi na Ofisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi zinatarajia kupokea, kusikiliza na kutolea maamuzi mashauri, malalamiko na taarifa za kodi kutoka kwa walipakodi na wadau wa kodi. 

Vilevile,amesema Ofisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma zinazotolewa na ofisi hiyo.

Kubahatisha

Waziri Dkt.Mwigulu amelieleza Bunge kuwa, katika mwaka 2023/24, Bodi ya Michezo ya Kubahatisha inatarajia kutoa leseni 11,880 kwa waendesha michezo ya kubahatisha,ambapo 2,273 ni leseni mpya na 9,607 ni leseni zitakazohuishwa.

Aidha, bodi hiyo inatarajiwa kufanya ukaguzi kwa waendesha michezo ya kubahatisha 101 na kusimamia uendeshaji wa Bahati Nasibu ya Taifa.

Masoko na mitaji

Akizungumzia kwa upande wa taasisi za usimamizi wa masoko ya mitaji, dhamana na bidhaa, Waziri Dkt.Mwigulu amesema, kwa mwaka 2023/24, Mamlaka ya Usimamizi wa Masoko ya Mitaji na Dhamana imepanga kuanzisha bidhaa mpya za masoko ya mitaji.

Pia kufanya mapitio ya kanuni na miongozo ya utoaji wa bidhaa katika masoko ya mitaji na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu masoko ya mitaji na bidhaa. 

Aidha,amesema Baraza la Rufaa za Masoko ya Mitaji linatarajia kuanza kupokea, kusikiliza na kutoa maamuzi kuhusu migogoro ya masoko ya mitaji. 

Vilevile, Soko la Bidhaa Tanzania linatarajia kuendelea na ujenzi wa jengo la ofisi jijini Dar es Salaam pamoja na kuendelea kuhamasisha matumizi ya mfumo wa soko wa kielektroniki ili kuongeza idadi ya bidhaa zinazouzwa na kununuliwa kupitia mfumo huo.

Takwimu

Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu akizungumzia kuhusu usimamizi wa takwimu rasmi amesema, katika mwaka 2023/24, Ofisi ya Taifa ya Takwimu inatarajia kusambaza matokeo ya sensa ya watu na makazi.

Pia, kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi ya takwimu za sensa na kuendelea kuandaa taarifa za sensa za kisekta kulingana na ratiba ya kazi zinazotakiwa kufanyika baada ya zoezi la sensa kukamilika. 

Aidha, amesema ofisi inatarajia kufanya tafiti za kitaalamu kuhusu watu wenye uwezo wa kufanya kazi,mapato na matumizi ya kaya binafsi, ajira, mapato na ustawi wa watoto katika jamii.

Ununuzi

Akizungumzia upande wa usimamizi wa ununuzi wa umma, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu amesema, katika mwaka 2023/24,Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma inatarajia kuendelea na ujenzi wa ofisi za Makao Makuu jijini Dodoma.

Majukumu mengine ni ujenzi wa mfumo wa ununuzi wa umma kwa njia ya mtandao awamu ya pili, kutoa mafunzo kwa watumishi 2,000 kutoka katika taasisi nunuzi 1,000 na wazabuni 5,000 kuhusu mfumo mpya wa ununuzi wa umma kwa njia ya kielektroniki na Sheria ya Ununuzi wa Umma, kufanya kaguzi ya thamani ya fedha katika taasisi nunuzi 85 na kaguzi ya ukidhi wa sheria kwa taasisi nunuzi 300 na kufanya mapitio ya nyaraka zote sanifu za zabuni.

"Katika mwaka 2023/24, Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini unatarajia kuanza ujenzi wa ofisi ya mkoa wa Kigoma, ofisi na kituo cha mafuta katika mikoa ya Njombe na Arusha pamoja na Wilaya ya Kahama, Korogwe na Masasi. 

"Aidha,Wakala umepanga kuboresha na kuhuisha mfumo wa GIMIS ili kuwezesha matumizi ya kadi katika huduma za ununuzi wa mafuta na kufanya upembuzi yakinifu ili kubaini uwezekano na mahitaji ya kuunganisha mfumo wa GIMIS na pampu, pamoja na tanki za mafuta. 

"Vilevile, Mamlaka ya Rufaa za Zabuni imepanga kutoa mafunzo kwa wajumbe, wafanyakazi wa mamlaka, wazabuni na taasisi nunuzi kuhusu utumiaji wa mfumo wa kielektroniki wa kusajili na kusimamia rufaa zitokanazo na michakato ya ununuzi wa umma,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu. 
 
Kupitia hotuba hiyo, Wizara ya Fedha na Mipango imeomba ridhaa ya Bunge kutumia jumla ya shilingi trilioni 15.94 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo kwa mafungu yake tisa ya kibajeti.

Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 15.38 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 564.22 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

"Aidha, ninaomba Bunge lako Tukufu liidhinishe shilingi bilioni 97.13 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Fungu 45-Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 87.72 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 9.41 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo,"amebainisha Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news