NA MWANDISHI WETU
WMJJWM, DODOMA
WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum inajipanga kutoa elimu ya masuala ya fedha kwa jamii hasa makundi maalum kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akipokea mwongozo wa mafunzo ya Elimu ya fedha kutoka kwa Kamishna wa Sekta ya Maendeleo ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja, baada ya mafunzo mafupi kuhusu elimu ya masuala ya fedha kwa Menejimenti na watumishi Wizara ya Maendeleo ya Jamii, jijini Dodoma leo Juni 30, 2023.
Hayo yamebainika kwenye mafunzo yaliyotolewa na Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango kwa Menejimenti na watumishi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, kuhusu fursa zinazopatikana katika masuala ya fedha, leo Juni 30, 2023 jijini Dodoma.
Akifungua Mafunzo hayo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt Dorothy Gwajima, amesema ushahidi unaonesha kuwa, yapo Makundi mengi ndani ya Jamii ambayo yanatamani kuchangamkia fursa za kiuchumi lakini wanashindwa kutokana na kutokuwa na taarifa ya wapi pakuanzia.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Menejimenti wa Wizara hiyo, Naibu Katibu Mkuu Wakili Amon Mpanju na Wataalamu wa Wizara ya Fedha na Mipango baada ya mafunzo kuhusu masuala ya fedha yaliyotolewa na wataalamu hao leo Juni 30, 2023 jijini Dodoma.
Amesema Wizara itashirikiana kwa karibu zaidi na Wizara ya Fedha na Mipango kutoa elimu ya fedha kwa wataalamu ili wakaielimishe jamii hadi ngazi ya chini.
"Mwaka 2022 nilipata Bahati ya kutembelea Maonesho ya Saba Saba na kupita kwenye taasisi kadhaa za fedha ambapo nilibaini uwepo wa fursa ambazo wanajamii wengi hawazifahamu," amesema Waziri Dkt. Gwajima.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju na Mhasibu Mkuu wa Wizara hiyo Fatma Oloo wakipokea mwongozo wa mafunzo ya Elimu ya fedha kutoka kwa Kamishna wa Sekta ya Maendeleo ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja, baada ya mafunzo mafupi kuhusu elimu ya masuala ya fedha kwa Menejimenti na watumishi Wizara ya Maendeleo ya Jamii, jijini Dodoma leo Juni 30, 2023.
Aidha, Waziri Dkt. Gwajima amesema mafunzo hayo yanasaidia kubadili fikra kuanzia ngazi ya watendaji ili wawe daraja imara kuwafikia wananchi kwa taarifa sahihi hasa wanawake na makundi maalum ndani ya jamii.
Kwa upande wake Kamishna wa sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Charles Mwamwaja amesema Jamii ina kila sababu ya kuelimishwa kuhusu fursa na matumizi ya fedha katika maisha yao ya kila siku na kubadili utaratibu wa nidhamu ya fedha kwa kuwa na utaratibu wa kuweka akiba.
Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti na Watumishi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum wakifuatilia mafunzo yanayotolewa na wataalamu wa Wizara ya Fedha na Mipango kuhusu masuala ya fedha jijini Dodoma leo Juni 30 2023.
Dkt. Mwamwaja amebainisha kuwa, tafiti nyingi zilizofanyika zinaonesha watu wengi hawana uelewa mpana wa fursa zilizopo katika Sekta ya fedha, hivyo kupitia Wizara fedha wameendelea kutoa Elimu hiyo kwenye Jamii.
"Uwekaji wa akiba ni suala la Msingi sana, unapoona miradi mikubwa inafanyika leo hii, ni kwa kuwa tunajua tukishaweka miundombinu hii inachangia sana ukuaji wa uchumi, barabara, maji, umeme nk. vinapofika lazima thamani ya eneo hilo inakuwa juu zaidi,"amesema Dkt. Mwamwaja.
Mtaalamu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Dionisia Mjema akitoa mafunzo kuhusu masuala ya fedha kwa Menejimenti na Watumishi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dodoma leo Juni 30, 2023.
Naye Mtaalam wa Fedha, Bi. Dionisia Mjema, anayesimamia huduma ndogondogo za Kifedha kutoka Wizara ya Fedha, ameelezea mkakati wa Programu ya Elimu ya fedha kwa Umma pamoja na kusisitiza suala la uwekezaji kwenye Masoko ya hisa.