106 wahukumiwa kwenda jela Arusha

ARUSHA-Jeshi la Polisi mkoani Arusha kuanzia Januari hadi Juni, 2023 limefanikiwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa makosa makubwa ya uhalifu ambapo 106 walipatikana na hatia na kuhukumiwa kwenda jela vifungo mbalimbali.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP Justine Masejo ameyasema hayo Julai 21, 2023 wakati akitoa taarifa ya jeshi hilo.

Amesema watuhumiwa hao walihukumiwa vifungo hivyo kwa makosa makubwa ikiwemo ubakaji, ulawiti, kusafirisha dawa za kulevya, unyang’anyi wa kutumia silaha, mauaji pamoja na kupatikana na nyara za Serikali.

Kamanda Masejo aliendelea kufafanua kuwa, kati ya waliohukumiwa, watuhumiwa 25 walihukumiwa vifungo vya maisha jela kwa makosa ya ubakaji, ulawiti na mauaji.

Pia, watuhumiwa 30 walihukumiwa kwenda jela miaka 30 kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha, kusafirisha dawa za kulevya, ubakaji na ulawiti. Wengine watano walihukumiwa vifungo vya miaka 20 kwa makosa ya kupatikana nyara za Serikali.

Mbali na hayo ACP Masejo alisema kuwa, jeshi hilo limefanikiwa kupunguza matukio ya uhalifu mkoani humo kwa asilimia 11, ambapo takwimu zinaonesha kwa mwezi Januari hadi Juni 2022 makosa yalikuwa 1,345 hali ambayo ni tofauti na kipindi kama hicho mwaka huu ambapo makosa yaliyoripotiwa ni 1,198 sawa na upungufu wa makosa 147.

Halikadhalika amesema, kwa kipindi kama hicho walifanikiwa kupunguza ajali za barabarani kwa asilimia 59 ambapo mwaka 2022 ajali zilizoripotiwa zilikuwa 184 ukilinganisha na ajali 76 zilizotokea mwaka huu ambapo ni sawa na upungufu wa ajali 108.

Aidha, amesema kupitia misako mbalimbali ambayo ilifanyika kuanzia mwezi Januari hadi Juni, mwaka huu dhidi ya dawa za kulevya walifanikiwa kukamata mirungi kilo 747 na gramu 695, bangi tani mbili na nusu pamoja na kuteketeza jumla ya tani tano na hekari 60 za bangi, lakini pia walikamata heroine gramu 560.75.

Halikadhalika alisema kwa kipindi hicho walifanikiwa kukamata watuhumiwa 233 wakiwa na pombe ya moshi maarufu kwa jina la gongo lita 1,091 pamoja na mitambo 21 ya kutengeneza pombe hiyo.

Lakini pia, Kamanda Masejo alisema Jeshi hilo limeimarisha ulinzi maeneo yote hasa kwa kuzingatia kipindi hiki ambacho kuna ongezeko kubwa la watalii (high season) pamoja na uwepo wa mikutano mbalimbali ya kimataifa ambayo inaendelea kufanyika mkoani humo.

Pia ametoa wito kwa wananchi kuendelea kufichua matukio ya uhalifu katika jamii ili wachukue hatua za kisheria dhidi ya wote watakaobainika.

Sambamba na hilo pia amewataka watu wachache wanaojihusisha na matukio ya uhalifu kuacha mara moja kwani watawakamata na kuchukua hatua za kisheria dhidi yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news