NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema, tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini na duniani kwa ujumla limekuwa likiongezeka na madhara yake ni makubwa na wakati mwingine athari zake ni za kudumu kwa jamii.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisikiliza maelezo ya wataalamu waliokuwepo kwenye Banda la Maonesho la Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kuhusiana na kazi mbalimbali ambazo mamlaka hiyo inafanya katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Kupiga Vita Matumizi na Biashara ya Dawa za Kulevya Duniani ambayo Kitaifa yalifanyika Juni 25, 2023 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. (Picha na Ikulu).
"Tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini na duniani kwa ujumla limekuwa likiongezeka na madhara yake ni makubwa, na wakati mwingine athari zake ni za kudumu kwa jamii.
"Mbali na kupoteza nguvu kazi ya uzalishaji mali, matumizi ya dawa za kulevya yamekuwa kichocheo kwa vitendo vya uhalifu kama vile wizi na uyang'anyi kama vile tulivyosikia, mashuhuda hapa walivyojieleza wenyewe, lakini pia inasababisha kuambukizana maradhi.
Pia, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amesema, mbali na kupoteza nguvu kazi ya uzalishaji,matumizi ya dawa za kulevya yamekuwa kichocheo cha vitendo vya uhalifu ikiwemo wizi na unyang’anyi na hata kuambukizana maradhi kama Ukimwi na Kifua Kikuu.
Ameyasema hayo Juni 25, 2023 wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Katika maadhimisho hayo ambayo yaliongozwa na kauli mbiu isemayo “Zingatia Utu; Boresha Huduma za Kinga na Tiba", Mheshimiwa Rais Dkt.Samia alikuwa mgeni rasmi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akipokea
Tuzo ya Kutambua Mchango wake kwenye Mapambano dhidi ya dawa za Kulevya
nchini kutoka kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyeiwasilisha kwa niaba
ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) katika
Maadhimisho ya Kitaifa ya Kupiga Vita Matumizi na Biashara ya Dawa za
Kulevya Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid
Jijini Arusha Juni 25, 2023.
"Kama Ukimwi na TB (Kifua Kikuu) kutokana na kushirikiana katika matumizi ya vifaa wanavyotumia katika kufanya mambo yao hayo, sasa niseme ni kwa sababu hii Serikali iliunda chombo mahususi cha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.
"Madhumuni ikiwa ni kuongoza mapambano dhidi ya dawa za kulevya, tulitaka kuwa na chombo chenye mamlaka na uwezo wa kusimamia na kutokomeza tatizo hili, kama alivyoeleza Kamishna Jenerali (Aretas Lyimo) majukumu ya mamlaka hii ni kuzuia uzalishaji, uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya nchini.
"Vile vile, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na Kimataifa katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya kwa kushirikiana na taasisi nyingine, kuweza kuzuia uhitaji wa dawa za kulevya, na kupunguza madhara yatokanayo na matumizi ya dawa hizo.
Jitihada kubwa
"Ni dhairi kwamba, tangu kuanzishwa kwake Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imefanya jitihada kubwa katika kutekeleza majukumu yake na kwa kweli, bila uwepo wa mamlaka hii (DCEA) hali ingekuwa mbaya zaidi.
"Takwimu alizotoka Kamishna Jenerali zinathibitisha hili, kama mlivyosikia ametoa takwimu za ukamataji wa dawa za kulevya tangua mwaka 2017 hadi sasa, na kazi iliyofanywa ya upanuzi wa huduma za tiba kwa walioathirika na dawa hizo na kulevya, kama ilivyoelezwa hapa.
"Kwa mujibu wa taarifa za hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) limeeleza kwamba, Tanzania ilifanikiwa kupunguza uingizwaji wa dawa za kulevya kutoka kwenye nchi zinazozalisha kwa zaidi ya asilimia 90.
"Na hapa ndipo aliposema Kamishna Jenerali (Aretas Lyimo) kwamba kwa sababu mamlaka yetu ilifanikiwa kupunguza uingizwaji wa dawa hizi, sasa dawa za kienyeji ndizo zimeshika kasi, mabangi na mamirungi sasa ndiyo yameshika kasi.
"Kwa sababu tumefanikiwa kiasi kikubwa kupunguza uingizwaji wa Cocaine, na Maheroine vile vile, tumekuwa kinara kwenye udhibiti wa kemikali bashirifu ambapo Shirika la UNODC kupitia Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (INCB) imetambua mchango wa Tanzania.
"Na kuiteua mamlaka yetu hapa Tanzania kutoa mafunzo kwenye nchi tisa ambazo ni Rwanda, Burundi, Madagascar, Zambia, Malawi, Ethiopia, Msumbiji, Eritrea na Mauritius kuhusu udhibiti wa kemikali bashirifu.
"Hili siyo jambo dogo na inaonesha kwamba, kazi inayofanywa inaonekana na taasisi hii imeweza kujipambanua kimataifa, hongereni sana Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.
Kuimarisha mahusiano
"Heshima hii mliyopewa pia muitumie kuimarisha mahusiano na nchi hizi hususani kwenye suala zima la kubadilishana taarifa za kiibtelijensia zinazohusiana na biashara ya dawa za kulevya, wakati tukisisitiza ushirikiano kati yetu na nchi jirani.
"Mkazo wetu uwekwe baina ya mamlaka za kuzuia na dawa za kulevya za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, lazima kuwe na ufanyaji kazi kwa karibu zaidi, lazima kuwe na ushirikiano mkubwa zaidi.
"Kama mnavyofahamu, bandari zetu ni milango ya kuhudumia usafiri na usafirishaji wa bidhaa kwenda nchi jirani, inawezekana baadhi ya wahalifu wakatumia usafirishaji wa shehena hizo kupitisha dawa za kulevya na ndiyo sababu ninasisitiza umuhimu wa kubadilishana taarifa za kiintelijensia.
"Na nchi jirani, lakini pia kufanya kazi kama taasisi moja baina ya Bara na Zanzibar kwa sababu, milango hii Zanzibar ipo wazi sana, mtu akitoka duniani njia yoyote anaweza kuingia Zanzibar na kutoa Zanzibar kuleta Bara ni kazi nyepesi sana.
Rais Dkt.Samia pia ameitaka jamii kuimarisha ushirikiano na viongozi wa dini pamoja na viongozi wa kijamii wakiwemo machifu kwa kuwa ndio walinzi wakuu wa maadili,utamaduni, mila na desturi.
"Kwa hiyo, tushirikiano kwa karibu zaidi ili tuweze kushinda au kuongeza mapambano dhidi ya dawa hizo, ni matumaini yangu kuwa, maboresho yanayoendelea kufanywa kwenye bandari zetu yatajumuisha ufungaji wa mitambo ya kisasa itakayosaidia kubaini shehena zinazopitishwa zikiwa na dawa za kulevya ndani yake.
“Hata hivyo kuwa na mitambo ni jambo moja, lakini kuwa na watendaji waadilifu ni jambo la pili, tukiwa na mitambo bila watendaji wenye uadilifu hatutopata matokeo tunayoyatarajia, tunahitaji watumishi wenye uzalendo wanaoweka mbele maslahi ya Taifa.
"Watumishi wa bandari, wa TMDA (Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba), wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) wote tutangulize maslahi ya Taifa mbele ndipo tutashinda vita hii,” amesisitiza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.
Ripoti ya PM
"Nilipata kupitia ripoti iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu kuangalia hali ya dawa za kulevya nchini, katika ripoti hiyo kuna maeneo kadhaa ambayo ninataka niyagusie hapa leo, eneo la kwanza, katika ripoti ile nimeona jitihada kubwa na nimeona kwenye mabanda ya maonesho pia.
"Jitihada kubwa inaelekezwa kwenye kutibu kuliko kukinga, ninapongeza kazi kubwa inayofanywa na asasi za kiraia kwenye tiba na uratibu, wa kuunganisha waraibu na huduma za kliniki.
"Wanafanya kazi kubwa sana, lakini kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba, nitoe wito kwa asasi za kiraia kuongeza jitihada kwenye kutoa elimu katika jamii hususani kupitia kwenye taasisi zetu za elimu, kule kwenye vijana wadogo tuwawahi, kule twende tuseme nao huko.
"Tutoe elimu ili vijana wajienpushe na janga hili. Lakini, la pili nimeona kwenye ripoti kwamba kumekuwa na changamoto ya vijana wanaomaliza tiba na hapa wamesema, kurejea tena kwenye uraibu wa dawa za kulevya na hii ni kwa sababu, wakimaliza kutibiwa wanakuwa hawana kazi ya kufanya.
"Lakini, tumemsikia Kamishna Jenerali amesema hatua wanazojipanga nazo, lakini nilipokuwa kwenye mabanda kule niliwauliza wakuu wa taasisi za kiraia na wenyewe wana hatua wanajipanga nazo, lakini pamoja na hatua hizo na sisi Serikali tunakwenda kujipanga kuona nini cha kufanya kuwasaidia vijana hao.
Wito
"Lakini nitoe wito pia, kwamba Wizara ya Afya, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, asasi za kiraia, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) na wadau wa maendeleo kuhakikisha wanashirikiana ili kuhakikisha vijana hawa wanapata afua zitakazowafanya wasiweze kurudia tena kwenye uraibu wa ulevi wa dawa za kulevya.
"Bali wapate shughuli zinazoweza kuwashughulisha na wakafanya uzalishaji na wakajenga ustawi wa maisha yao. Jambo la tatu nililoliona kwenye ripoti kulikuwa kunazungumza kwamba kesi zinazokwenda mahakamani.
"Tumesikia tatkwimu hapa,nyingine nyingi zinashinda, lakini zipo nyingine nyingi pia zinashindwa na hii ni kwa sababu ya sababau kadhaa kuanzia usajili wa kesi, labda uwasilishaji wa vithibiti (vielelezo) au usahidi.
"Upelekaji wa ushaidi kule mahakamani kutoka ngazi moja kwenda ngazi nyingine au kutoka polisi kwenda mahakamani na wenyewe wanakuwa na mapungufu yake na kupelekea kesi nyingine hizo kuendelea kushindwa. kwa hiyo hapa nitoe wito kwa taasisi zote zinazohusika kuangalia pia weledi na uadilifu wa watu wetu wanaoshughulika na mambo haya.
Tume
"Ndugu zangu nyote mnafahamu kwamba, niliunda Tume ya Kuboresha Mfumo wa Haki Jinai nchini na ninatarajia kupokea taarifa yao hivi karibuni, lakini ni matarajio yangu kwamba, mapendekezo yatakayotolewa na tume hiyo yatasaidia kufanya mabadiliko kwenye taasisi zetu zinazosimamia haki ya jinai na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
"Na weledi zaidi na kwa maana hiyo tutapata nguvu zaidi kwenye mapambano dhidi ya dawa za kulevya, ndugu wananchi mbali na juhudi mbalimbali ambazo Serikali imefanya au kujipanga kufanya ninataka nisisitize nafasi maalumu ya familia katika jitihada hizi, kwani huko ndiko yanakoanzia matatizo.
Familia
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amesema, kutowajibika kwa wazazi husababisha watoto kuathirika na matumizi ya dawa za kulevya hivyo ni vyema kuwalinda watoto dhidi ya dawa hizo pamoja na vitendo vingine vilivyo kinyume na mila, desturi, maadili na silka zetu.
Rais Dkt.Samia pia ameitaka jamii kuimarisha ushirikiano na viongozi wa dini pamoja na viongozi wa kijamii wakiwemo machifu kwa kuwa ndio walinzi wakuu wa maadili,utamaduni, mila na desturi.
"Wazazi na walezi wanaposhindwa kufuatilia mienendo ya watoto wao na kuchukua hatua kila tunapogundua mabadiliko ya kitabia za watoto wetu ndipo tunapowapoteza watoto wetu na kusababisha mateso katika familia, jamii na Taifa kwa ujumla.
"Niwakumbushe wazazi wenzangu, na walezi wenzangu tuchukue nafasi zetu katika kuhakikisha watoto wetu wanakwenda kwenye njia iliyonyooka, nilimuona Innocent hapa kutoka kwa mama tu kwenda shule katikati hapo ameweza kuharibika, kwa hiyo wazazi tuwe wepesi sanma kufuatilia nyendo za watoto wetu.
"Zaidi ya hapo, wale tunaowaita watoto wa mitaani, miongoni mwao wana baba na wana mama zao, lakini wanatoroka majumbani kutokana na yanayotokea huko majumbani kwao, kwa hiyo baadhi yao wanaitwa watoto wa mitaani, lakini ni watoto ambao wazazi wao wapo.
"Sasa, katika hawa watoto wa mitaani wengi wao wanaathirika na balaa hili la dawa za kulevya, sasa kundi hili la watoto linatokana na kutokuwajibika kwa wazazi, na walezi wao kwa hiyo hapa ninasisitiza kuhusu nafasi ya wazazi na walezi katika kuwalinda watoto dhidi ya dawa za kulevya pamoja na vitendo vingine vyovyote vilivyo kinyume na mila, desturi, maadili na silka zetu za Kitanzania,"amesisitiza Rais Dkt.Samia.
Waziri Mhagama
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu),Mhe.Jenista Mhagama amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kuiwezesha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
"Nichukue nafasi hii kukushuru wewe binafsi Mheshimiwa Rais, kwa kukubali ombi la kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho haya pamoja na kwamba unayo majukumu mengi ya Kitaifa yanayokukabili.
"Ninawashukuru pia viongozi, wageni waalikwa pamoja na wananchi wote waliokuja hapa kushiriki kwenye tukio hili muhimu.
"Mheshimiwa mgeni rasmi, tunakushukuru sana kwa dhamira yako kuu na ya dhati ya kuiwezesha mamlaka hii kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
"Kama ambavyo tunafahamu mamlaka hii ni miongoni mwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama ambayo ina jukumu kubwa la kusimamia ustawi wa wananchi hususani kwenye mapambano dhidi ya biashara haramu na matumizi ya dawa za kulevya ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikiharibu vijana ambao ndiyo nguvu kazi kubwa ya Taifa,"alifafanua Mheshimiwa Waziri Mhagama.
Kamishna Jenerali DCEA
Wakati huo huo, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake ambazo zinaiwezesha mamlaka hiyo kutekeleza majukumu yake kikamilifu ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo aliyabainisha hayo wakati akitoa wasilisho lake mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani.
"Mheshimiwa Rais,tunatambua na kuthamini juhudi zako katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini. Tunakupongeza kwa juhudi unazoendelea kuchukua wewe binafsi pamoja na serikali yako nzima.Hongera sana Mheshimiwa Rais.
"Pia, Mheshimiwa Rais, tutakuwa wachoyo wa fadhila tusipokushukuru kwa namna ya kipekee kwa kuwa ni mara ya kwanza tangu mamlaka ianze kutekeleza majukumu yake imetengewa fedha za mradi wa maendeleo shilingi bilioni mbili kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Utengamao katika mwaka wa fedha 2023/2024.
"Kituo hiki kitajengwa eneo la Itega jijini Dodoma na kitakuwa na programu mbalimbali kama vile elimu ya stadi za maisha, huduma za upataji nafuu na huduma ya tiba saidizi.
"Programu hizo pia zitasaidia kuhakikisha waraibu wanapata utaalam utakaochangia kujiajiri wenyewe ili kutorudia matumizi ya dawa za kulevya,"amefafanua Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.
Aidha, Kamishna Jenerali Aretas Lyimo alimueleza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kuwa, mamlaka hiyo inaunga mkono jitihada zake ili kuifikia dhamira ya Serikali unayoiongoza ya kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi ikiwemo kuongeza pato la mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
"Sisi (DCEA) tunaona na kutambua kazi kubwa unayoendelea kuifanya katika kuiletea nchi yetu maendeleo, hasa katika kipindi hiki cha changamoto za uchumi wa dunia ambapo Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati nchi nzima ikiwemo ujenzi wa miundombinu mikubwa ya Barabara na ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere.
"Halkadhalika,ushirikishaji wa sekta binafsi katika uwekezaji hasa katika miundombinu ya mawasiliano na uchukuzi, ikiwemo Reli ya Kisasa ya SGR na Bandari ya Dar es Salaam, ni hatua inayostahili pongezi.
"Usimikaji wa mitambo ya kisasa ya utambuzi katika maeneo hayo hususani Bandari ya Dar es Salaam baada ya uwekezaji utasaidia kudhibiti bidhaa haramu zikiwemo dawa za kulevya na kemikali bashirifu kuingizwa nchini.
"Naomba tukuahidi Mheshimiwa Rais kuwa, tutaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kushughulikia changamoto zote zinazotokana na dawa za kulevya ili kulinda nguvu kazi ya Taifa hususani kundi la vijana ili
waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa letu.
"Mheshimiwa Rais, tunamshukuru kipekee Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kasim Majaliwa Majaliwa kwa uongozi wake mahiri na kuisimamia mamlaka vizuri kwa kuwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ipo chini yake.
"Mheshimiwa Rais, tunamshukuru Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Jenista Mhagama ambaye ndiye Waziri mwenye dhamana kuisimamia mamlaka. Amekuwa kiongozi bora kwetu kutusimamia,kuturatibu na kutuongoza katika kufanikisha shughuli hii ya leo,"amebainisha Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.
Mbali na hayo, Kamishna Jenerali Aretas Lyimo alifafanua kuwa,maadhimisho hayo yanahusisha mabanda ya
maonesho kutoka kwa wadau mbalimbali wanaojihusisha na mapambano dhidi ya dawa za kulevya wakiwemo wa haki jinai na afya.
Lengo kuu, Kamishna Jenerali Aretas Lyimo amesema ni kuelimisha umma juu ya masuala mbalimbali yanayohusiana na dawa za kulevya ikiwemo hali ya dawa za kulevya, aina ya dawa za kulevya, madhara pamoja na sheria inayosimamia na kuratibu masuala yote yanayohusu dawa za kulevya.
Pia, amesema wananchi wamepata fursa ya kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na ofisi zilizoshiriki kwenye maadhimisho hayo.
Sheria
Kamishna Jenerali Aretas Lyimo alimueleza, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kuwa, ili kuboresha udhibiti wa dawa za kulevya Bunge lilitunga Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na.5 ya mwaka 2015 ambayo ndiyo iliyoanzisha Mamlaka mwaka 2017.
Amesema, mamlaka inaendelea kupanua shughuli zake hadi ngazi za kanda na baadae kufika ngazi za mikoa. Katika kutekeleza hilo, amesema mamlaka ipo katika hatua ya kufungua ofisi ya kanda ya Kaskazini mkoani Arusha.
"Uongozi wa mkoa ukiongozwa na Mhe. John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, tayari umetupatia ofisi na tumeanza kuweka vitendea kazi ikiwemo rasilimali watu. Naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
"Pia,maandalizi ya kufungua ofisi ya kanda kwa upande wa Nyanda za Juu Kusini yanaendelea ambapo maombi ya ofisi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya yameshafanyika.
"Aidha, mamlaka imewasilisha maombi ya kupata maeneo ya kujenga ofisi katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Mbeya na Mtwara.Tunatarajia jitihada hizi zitaungwa mkono na mikoa husika,"amesema Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.
Pia, alimueleza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kuwa, miongoni mwa majukumu ya mamlaka ni pamoja na kuzuia uingizaji, uzalishaji na usambazaji wa dawa za kulevya (Supply Reduction), kuzuia uhitaji wa dawa za kulevya (Demand Reduction).
Majukumu mengine ni kupunguza madhara yanayosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya (Harm Reduction) na kuimarisha ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya (Regional and International Cooperation).
Amesema, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inatambua matarajio ya Serikali yanayoongozwa na maagizo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Sura ya kwanza kipengele (j) inayosomeka kudhibiti na kuimarisha mapambano dhidi ya uzalishaji, uagizaji,usambazaji, uuzaji na matumizi ya dawa za kulevya.
"Tunaahidi kutumia weledi wetu, ubunifu, nguvu na uwezo tulionao kuhakikisha tunatekeleza majukumu hayo ili kufikia matarajio hayo tukitanguliza mbele haki na uzalendo,"amebainisha Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.
Mafanikio makubwa
Wakati huo huo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Aretas Lyimo amesema,tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo ndani ya miaka sita yamepatikana matokeo chanya ndani na nje ya nchi.
"Mheshimiwa Rais, matunda ya kuanzishwa kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya yameanza kuonekana dhahiri ndani ya Serikali na nje ya nchi kwa ujumla.
"Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka sita tokea kuanzishwa kwa mamlaka yanayohusisha ukamataji wa dawa mbalimbali za kulevya kwa kiwango kikubwa,"amefafanua Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.
Amebainisha kuwa, tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo, Februari 2017 hadi Juni 2023. Jumla ya tani 712.81 za bangi, tani 121.83 za mirungi, kilogramu 2,190.5 za heroin, kilogramu 29.2 za cocaine, kilogramu 432.27 za methamphetamine, gramu 56.04 za mescaline na mililita 3,840 za dawa tiba aina ya Pethidine zilikamatwa.
Pia, amefafanua kuwa, kiasi cha tani 601.6 na lita 1,125 za kemikali bashirifu zinazoweza kutumika kutengeneza dawa za kulevya zilizuiliwa kuingia nchini kutokana na ukiukwaji wa taratibu za kuingiza bidhaa hizo ikiwemo kutoa
taarifa za kughushi.
Aidha, Kamishna Jenerali Lyimo anasema kuwa, katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi Machi 2023 hadi Juni 2023, mamlaka ilifanya operesheni kubwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro na Arusha.
"Katika kipindi hicho tumefanikiwa kukamata kilo 200.5 za heroin, gramu 531.43 za methamphetamine na mililita 3,840 za dawa tiba aina ya Pethidini.
"Pia, katika operesheni maalum iliyofanyika mkoani Arusha kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi, tumekamata na kuteketeza bangi kavu gunia 978 na bangi mbichi gunia 5,465. Jumla ya kiasi hicho cha bangi ni tani 615 kiwango ambacho ni kikubwa ukilinganisha na tani 20.58 iliyokamatwa kwa mwaka mzima wa 2022 sawa na ongezeko la asilimia 96.7,"amefafanua Kamishna Jenerali Lyimo.
Amesema, operesheni ya Arusha ilikuwa yenye mafanikio ambapo wananchi walipata uelewa na hamasa kubwa na kuanza kuchukua hatua ya uteketezaji wa mashamba ya bangi kwa hiyari yao.
Vile vile, Kamishna Jenerali huyo amesema,,amlaka imeendelea kufanya operesheni za kutokomeza vijiwe vya matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
"Katika kipindi cha mwezi Machi 2023 hadi Juni 2023,mamlaka imefanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya heroin kete 3,878, cocaine kete 138, bangi iliyosindikwa (skanka) kilogramu 1.5.
"Kwa ujumla,operesheni hizo zimehusisha ukamataji wa watuhumiwa 109 wakiwemo raia wa kigeni watatu. Aidha, uchunguzi umebaini kwamba,kati ya watuhumiwa waliokamatwa, watumiaji wa dawa za kulevya ni 94,"amebainisha.
Wakati huo huo, Kamishna Jenerali Aretas Lyimo alimueleza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kuwa,mamlaka imeendelea kufuata taratibu za kisheria za kuteketeza dawa za kulevya ambazo zimehifadhiwa katika maghala mbalimbali.
Amesema, zoezi hilo hufanyika kwa mujibu wa sheria kwa dawa zote za kulevya ambazo mashauri yake yamemalizika mahakamani au kwa yale yanayoendelea na usikilizwaji mahakamani ila kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo changamoto ya uhifadhi wa dawa husika, Mahakama hutoa amri dawa hizo za kulevya ziteketezwe.
"Lengo la kutekeleza zoezi hili ni kuhakikisha dawa hizi hazirudi tena kwenye mzunguko na kutumiwa na jamii. Katika kutekeleza hili,mamlaka ikishirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama na wadau wengine wa haki jinai tumeteketeza kiwango kikubwa cha dawa za kulevya aina mbalimbali kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2017 hadi Juni, 2023,"amebainisha.
Amesema, dawa hizo ni pamoja na bangi tani 621.9, hekari 2,274 za bangi na hekari 75 za mirungi,mchanganyiko wa bangi na mirungi tani 2, heroin kilogramu 867.82, methamphetamine (meth) kilogramu 355,mchanganyiko wa heroin na cocaine kilo 199, na cocaine kilogramu 75.44.
Kamishna Jenerali Lyimo amefafanua kuwa, mwezi Juni, 2023 uteketezaji umehusisha dawa za tiba za vikohozi lita 10,000 zilizobainika kuwa na viambata pungufu vya kemikali bashirifu baada ya kuchepushwa kwenye mchakato wa utengenezaji wa dawa hizo.
"Mheshimiwa Rais, miongoni mwa viashiria vinavyothibitisha kuongezeka kwa udhibiti wa dawa za kulevya nchini kutokana na ukamataji mkubwa unaofanyika ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya mashauri ya dawa za kulevya na kuongezeka kwa kasi ya kuyashughulikia mashauri hayo yafikishwapo mahakamani.
"Katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia April 2022 hadi Mei, 2023 jumla ya mashauri 6,818 yamefanyiwa kazi katika hatua mbalimbali ambapo kati ya hayo mashauri 1,648 yalitolewa maamuzi mahakamani,"amesema.
Aidha, alisema Jamhuri ilishinda jumla ya mashauri 987 na kushindwa mashauri 153 huku mashauri 508 yaliondolewa mahakamani kwa sababu mbalimbali.
Hadi sasa, Kamishna Jenerali Lyimo anasema, jumla ya mashauri yanayoendelea kusikilizwa mahakamani ni 2,266 na
mashauri 1,256 upelelezi wake haujakamilika.
"Mheshimwa Rais, kasi hii ya utendaji inaweza kuonekana dhahiri kwa taarifa ya mwezi Mei, 2023 pekee ambapo jumla ya mashauri 145 yamefunguliwa katika Mahakama mbalimbali nchini na mashauri 17 yametolewa hukumu.
"Kati ya mashauri yaliyotolewa hukumu, mashauri 14 watuhumiwa wametiwa hatiani na kufungwa kati ya miaka mitatu hadi kifungo cha miaka 30 jela. Mashauri matatu yameondolewa mahakamani kwa sababu mbalimbali,"amefafanua Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.
Aidha, amesema kwa operesheni iliyofanyika mkoani Arusha mwezi huu wa sita pekee wamefanikiwa kufungua jumla ya mashauri 20.
Tanzania yang'ara
Pia, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DECA) imesema, Tanzania imefanikiwa kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya kwa zaidi ya asilimia 90.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo wakati akitoa wasilisho lake mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema;
"Mheshimiwa Rais, kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) inaonesha kuwa Tanzania imefanikiwa kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya kwa zaidi ya asilimia 90.
"Haya ni mafanikio makubwa sana, tunakupongeza sana Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais, nchi yetu imekuwa kinara kwenye udhibiti wa kemikali bashirifu, hivyo shirika la UNODC kupitia Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (INCB) imetambua mchango wetu na kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya,
Tanzania imepewa heshima kubwa ya kutoa mafunzo ya udhibiti wa kemikali bashirifu katika nchi tisa,"amebainisha Kamishna Jenerali Lyimo.
Alizitaja nchi hizo kuwa ni Rwanda, Burundi, Madagascar, Zambia, Malawi, Ethiopia, Msumbiji, Eritrea na Mauritius.
Huduma za tiba
Katika hatua nyingine, Kamishna Jenerali Aretas Lyimo amesema kuwa, huduma za tiba kwa waathirika wa dawa za
kulevya zilianza rasmi nchini mwaka 2011, ambapo hadi 2016,kulikuwa na kliniki tatu tu nchini ambazo zilihudumia waathirika 3,500.
Pia,amesema tangu kuanzishwa kwa mamlaka mwaka 2017, kumekuwa na ongezeko la kliniki 12 zaidi na hivyo kufanya jumla ya kliniki 15 mpaka sasa zikihudumia waraibu 14,500 kila siku.
Aidha, amesema mamlaka ina jukumu la kusimamia na kuratibu asasi za kiraia zinazotoa elimu kwa jamii juu ya tatizo la dawa za kulevya na kuwaandaa waraibu kwa kuwaunganisha na huduma za tiba katika kliniki zinazotibu waraibu kwa kutumia dawa ya methadoni.
"Hadi sasa, kuna asasi za kiraia zipatazo 100 Tanzania bara zinazoshirikiana na mamlaka katika kufikisha ujumbe kwa jamii juu ya madhara ya dawa za kulevya.
"Aidha, hadi sasa kuna Nyumba za Upataji Nafuu (Sober houses) zipatazo 50 katika mikoa 11 Tanzania bara zinazowahudumia waraibu wa dawa za kulevya wapatao 3,180. Uendeshwaji wa nyumba hizi unaratibiwa na Mwongozo wa Uanzishaji na Uendeshaji wa Nyumba za Upataji Nafuu (sober houses) wa mwaka 2018,"alibainisha Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.
Alifafanua kuwa, mamlaka imeimarisha ushirikiano na taasisi mbalimbali za kitaifa kama nyenzo muhimu ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Katika hili, Kamishna Aretas Lyimo alimueleza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kuwa,mamlaka imeingia makubaliano na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa ajili ya kuunganisha klabu za kupinga rushwa mashuleni na vyuoni ili zijumuishe masuala ya dawa za kulevya.
Lengo kuu amesema ni kuhakikisha elimu sahihi juu ya dawa za kulevya na rushwa inawafikia wanafunzi wote nchini kuanzia ngazi ya chini ya elimu.
Amesema, hatua hii itawawezesha Watanzania kuchukia rushwa na dawa za kulevya tangu wakiwa na umri mdogo na pia kuwa na moyo wa kizalendo.
"Mheshimiwa Rais, mamlaka imeimarisha mahusiano mazuri na taasisi mbalimbali zinazoshughulika na udhibiti wa dawa za kulevya kimataifa kama vile United Nations Office on Drugs and Crime (UNODC), Interpol, Drug Enforcement Administration (DEA), National Crime Agency (NCA), Centers for Disease Control and Prevention (CDC) Walter Reed Army Institute of Research (WRAIR),
"Management and Development for Health (MDH),Tanzania Health Promotion Support (THPS) na AMREF Health Africa katika udhibiti wa dawa za kulevya,"ameeleza Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.
Vile vile, amesema Tanzania ni mshirika wa makubaliano ya muunganiko wa nchi tatu (Trilateral Planning Cell) katika kupambana na dawa za kulevya inayohusisha pia nchi za Msumbiji na Afrika Kusini.
"Miongoni mwa masuala tunayoshirikiana ni kubadilishana taarifa za kiintelijensia na kufanya operesheni za pamoja. Mheshimiwa Rais,mamlaka kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo iliandaa Mwongozo ambao umeanza kutumika kutoa elimu kuhusu tatizo la dawa za kulevya nchini.
"Lengo la mwongozo huo ni kuyawezesha makundi mbalimbali ya kijamii nje ya mfumo rasmi wa elimu kupata elimu juu ya dawa za kulevya ili kuiepusha jamii dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya. Hii ni hatua nzuri katika kuzuia madhara ya dawa za kulevya kwa jamii,"amesisitiza Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.
Tushirikiane
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Aretas Lyimo ametoa wito kwa wadau mbalimbali nchini kushirikiana na mamlaka hiyo kupiga vita dawa za kulevya kwa ustawi bora wa jamii na Taifa.
"Mheshimiwa Rais, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, nichukue nafasi hii kuwaomba viongozi wa dini zote, taasisi za Serikali,mashirika binafsi (NGOs),wanasiasa,mihimili ya Bunge na Mahakama, wananchi wote kwa ujumla, tuendelee kushirikiana kupiga vita dawa za kulevya ili kuwa na jamii bora yenye maendeleo endelevu,"alifafanua Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.
Aidha, Kamishna Jenerali Aretas Lyimo amefafanua kuwa, mbali na mafanikio ambayo wameyapata ndani ya kipindi kifupi kuna changamoto mbalimbali ambazo Serikali imeendelea kuzishughulikia.
"Mheshimiwa mgeni rasmi, ukirejea mafanikio haya yaliyoelezwa, ni dhahiri kuwa utekelezaji wa malengo ya
kuanzishwa kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya una muelekeo mzuri ndani ya kipindi kifupi licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali ambazo Serikali imeendelea kuzishughulikia.
"Mheshimiwa Rais, Tanzania inakabiliwa na tatizo la dawa za kulevya zinazozalishwa nchini ambazo ni bangi na mirungi na zinazoingizwa kutoka nje ambazo ni heroin, cocaine na methamphetamine."
Bangi tatizo
Kamishna Jenerali Aretas Lyimo amesema, bangi imeendelea kuwa tatizo kubwa, kwani hutumiwa kwa wingi na rika la vijana, ikifuatiwa na heroin ambayo pia huongoza katika kusababisha uraibu,matatizo ya afya ya akili,maradhi na vifo kwa watumiaji.
Amesema, bangi hulimwa zaidi kwenye mikoa ya Arusha, Manyara, Mara, Morogoro,Njombe, Iringa na Ruvuma huku mikoa inayolima mirungi zaidi ni Tanga na Kilimanjaro.
"Mheshimiwa Rais, kuanzia mwezi Aprili 2021, Tanzania ilianza kukamata dawa aina ya methamphetamine ambayo hutengenezwa kwa wingi kwa kutumia kemikali bashirifu, madhara ya matumizi ya dawa hii ni makubwa sana,"alisema.
Pia, alisema changamoto nyingine ni upungufu wa kliniki za kutoa huduma kwa waathirika wa dawa za kulevya. Hadi sasa,kuna kliniki 15 za methadone (Medically Assisted Theraphy-MAT) wakati hitaji halisi kwa sasa ni kliniki 25.
Maeneo yenye uhitaji zaidi wa kliniki hizo ni Muheza, Chalinze, Kahama, Morogoro, Mtwara,Shinyanga Mjini, Katavi, Iringa, Njombe,Moshi na Singida.
"Mheshimiwa Rais, nchi yetu inakabiliwa na tatizo la matumizi ya dawa tiba zenye asili ya kulevya. Changamoto hii imeongezeka baada ya kuimarika kwa udhibiti wa dawa za kulevya.
"Katika kukabiliana na tatizo hili, mwezi Januari hadi Mei 2023, mamlaka kwa kushirikiana na TMDA, Baraza la Famasi Nchini na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) ilifanya uchunguzi ili kubaini na kutathmini uchepushwaji wa dawa tiba zenye asili ya kulevya katika mikoa ya Mwanza, Geita, Arusha na Mbeya.
Dawa nyingine
"Dawa zilizobainika kutumika zaidi ni pamoja na valium, tramadol, phenobarbital, Amitryptiline na Maprotiline.Mheshimiwa Rais, utafiti mwingine unaofanywa na mamlaka kwa kushirikiana na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Rais,umebaini kuwepo kwa matumizi ya dawa za kulevya kupitia shisha.
"Uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya watumiaji huchanganya shisha na dawa za kulevya kama vile bangi, heroin na cocaine. Hii pia ni changamoto kwa kuwa matumizi ya shisha yanaendelea kuongezeka bila kuwa na udhibiti mahususi na hivyo kuchangia kuwepo kwa ongezeko la biashara na matumizi ya dawa za kulevya,"amebainisha Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.
Aidha, alimweleza Rais Dkt.Samia kuwa, mamlaka inahitaji kufungua ofisi za kanda na mikoa ili kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya. Hata hivyo, amesema ili kutekeleza hilo mamlaka itahitaji ongezeko la rasilimali watu na vitendea kazi vya kisasa.
"Mheshimiwa Rais, katika kukabiliana na changamoto kama zilivyoainishwa, mamlaka ikishirikiana na wadau wengine inatarajia kushirikiana na Wizara ya Kilimo na wadau wengine kufanya tafiti na kutoa mapendekezo ya kilimo cha mazao mbadala hususan kwenye maeneo yanayolimwa bangi na mirungi ili wananchi waanze kulima mazao mbadala yakiwemo ya chakula na biashara na kuacha kulima mazao haramu.
"Kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuona namna bora ya kuingiza maudhui yanayoelimisha wanafunzi wa ngazi zote za elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya hasa katika kipindi hiki cha maboresho ya mtaala wa elimu nchini ili kuwaepusha wanafunzi na jamii kujiingiza kwenye janga hili linalodidimiza nguvu kazi ya Taifa,"amefafanua Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.
Pia, amesema kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kuhakikisha wanaboresha na kuongeza kliniki ambazo zitatoa huduma za matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya nchi nzima.
Sambamba na kuimarisha ushirikiano na taasisi zote za haki jinai, ili kuboresha mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Ushirikiano huo amesema ni pamoja na kubadilishana taarifa za utendaji kazi kwa wakati na kuimarisha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA
Wadau
Ally Kayange ambaye ni Mwakilishi wa Mashirika ya Kimataifa yanayofanya kazi chini ya Mfuko wa Dharura wa Watu wa Marekani alimshukuru Rais Dkt.Samia kwa kazi kubwa anazozifanya kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini.
Mwenyekiti kutoka Kijiji cha Kisimiri Juu,Mbayani Kuresoi alisema bangi ni zao haramu, hivyo watu waache kulima na aliomba miundombinu ya barabara katika vitongoji vitatu ili kufikia wananchi kwa haraka ili biashara wanayofanya ziweze kufika kwa wakati.
Pia alisema, wao wapo mlimani na wanahitaji miundombinu ya maji ili waweze kuwa na uwezekano wa kunyeshea mboga mboga na kuachana na zao la bangi.
Aidha, aliomba wawe na mazao mbadala kama mahindi,maharage,pareto badala ya kulima bangi na aliishukuru Serikali katika kaya ya Uwiro na King'ori na kuongeza kuwa uongozi wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (DCEA) wameanza ili kuachana na dawa za kulevya.
Kuresoi alisema, wameteua kamati ya watu 60 ili kuhakikisha bangi inaisha ndani ya miaka mitatu ijayo, kwa sababu bangi iking'olewa inaota tena kutokana na rutuba ya udongo."Kilimo cha bangi kilitufanya tukimbie polisi na watu wa Kisimiri Juu hawavuti bangi ila wanauza."
Shuhuda
Judith Uruki mkazi wa jijini Arusha katika kilele hicho cha maadhimisho anasema,ndoa ilimfanya akaingia katika matumizi ya dawa za kulevya aina ya heroin baada ya mumewe kumpa sigara avute.
Aliyasema hayo alipokuwa akitoa ushuhuda wa maisha yake mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.
“Mchumba alinifanya nikaingia kwenye maharibiko, sikujua kama anatumia alinifundisha kuvuta sigara nikawa navuta, lakini nikinunua mwenyewe dukani naona hainitoshelezi isipokuwa ile anayonipa yeye.
“Kumbe ile sumu inaniingia taratibu, nilipata msiba Moshi, huko nilikaa siku mbili ghafla nilipata homa kali niliumwa natetemeka naskia maumivu makali, hali ilikuwa mbaya nilipimwa maradhi yote hayaonekani."
Uruki anasema, siku ya tatu akahisi zahanati za huko haina huduma nzuri hiyo akarudi mkoani Arusha na baada ya kurudi nyumbani kwa mumewe na kumweleza hali hiyo akampa avute na baada ya kuvuta dakika tatu alijihisi mzima.
“Mume wangu aliniambia hutakiwi ukae bila kukosa hii kitu, aliniambia ni dawa za kulevya na hapo ndipo nilipojua kumbe nimeingia huko.
“Nilitamani kuacha nilishindwa, baada ya miaka michache hata nyumba za urithi mume wangu alipoteza tukawa hatuna pa kuishi tumedhuulumiwa nyumba sababu ya dawa za kulevya.
“Mume wangu akaenda kuchukua mzigo Dar es Salaam yeye akaanza kujificha sababu anauza mimi nikawa natembeza mzigo basi nikawa naongeza dozi zaidi nikaharibika zaidi nimetumia dawa za kulevya miaka 16,” alibainisha Judith ambaye kwa sasa anaendelea na matibabu ya kuachana na dawa hizo jijini Arusha.
Kuhusu DCEA
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015. Sheria hii iliifuta Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Kuanzishwa kwa Mamlaka Kulitokana na mapungufu yaliyokuwepo katika mfumo wa udhibiti wa dawa za kulevya.
Mapungufu hayo yalikuwa ni pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya iliyoanzishwa na Sheria ya ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995 kukosa nguvu ya kisheria ya kupeleleza, kufanya uchunguzi na kukamata wahalifu wa dawa za kulevya.
Kutokana na mapungufu hayo, Baraza la Mawaziri katika kikao chake cha tarehe 8 Novemba, 2007 (Waraka Na 60/2007) liliagiza, kurekebisha au kufuta Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995, ili kukidhi matakwa na changamoto za udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
Baraza la Mawaziri liliagiza kuundwa kwa chombo cha kupambana na dawa za kulevya chenye uwezo kiutendaji kwa kukipa mamlaka ya ukamataji, upekuzi na upelelezi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa dawa za kulevya nchini.
Kufuatia agizo hilo, tarehe 24/03/2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kupitisha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015 na kuanza kutumika rasmi tarehe 15 Septemba, 2015 kupitia tangazo la Serikali namba 407 (GN NO.407/2015).
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilianza kutekeleza majukumu yake kikamilifu tarehe 17 Februari, 2017 baada Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Kamishna Jenerali.
Majukumu
Majukumu ya Mamlaka ni kufafanua, kuhamasisha, kuratibu na kutekeleza hatua zote zinazoelekezwa katika udhibiti wa dawa za kulevya. Katika kutekeleza majukumu hayo Mamlaka inafanya kazi zifuatazo:
i.Kusimamia utekelezaji wa mikataba ya kimataifa, maazimio na makubaliano katika kudhibiti dawa za kulevya.
ii.Kuandaa na kutekeleza mpango wa Taifa wa kudhibiti dawa za kulevya.
iii.Kutengeneza miongozo inayoelezea tatizo la dawa za kulevya na madhara yake katika jamii;
iv.Kuboresha na kurekebisha sheria na kanuni za udhibiti wa dawa za kulevya;
v.Kuhamasisha udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya ikiwemo kutoa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya, kusambaza taarifa kwa umma na juhudi nyingine za udhibiti;
vi.Kuchukua hatua stahiki za kupambana na biashara ya dawa za kulevya zikiwemo kukamata, kupekua na uchunguzi wa masuala yanayohusiana na dawa za kulevya.
vii.Kuzuia, kupeleleza na kuchunguza uchepushaji wa dawa za tiba zenye madhara ya kulevya pamoja na kemikali zilizosajiliwa kutoka kwenye vyanzo halali wakati huo huo kuhakikisha dawa hizo zinapatikana kwa matumizi ya tiba, biashara na mahitaji ya kisayansi;
viii.Kuanzisha mfumo thabiti wa ukusanyaji taarifa na uchambuzi katika ngazi ya taifa kuhusu matumizi na biashara ya dawa za kulevya;
ix.Kuhamasisha, kuratibu na kuhakikisha jitihada za ushirikiano wa kimataifa katika kudhibiti wa dawa za kulevya zinaimarishwa;
x.Kufanya, kuwezesha na kuratibu tafiti zinazohusiana na dawa za kulevya;
xi.Kuratibu na kuwezesha wadau wanaojihusisha na udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya;
xii.Kuelimisha na kuhamasisha jamii kushiriki katika mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya;
xiii.Kutoa mafunzo kwa watendaji wanaojihusisha na udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya, fedha haramu na kemikali bashirifu.
xiv.Kufanya uchunguzi wa sayansi jinai.
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Makala
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)