Asante kwa vitimwendo

NA LWAGA MWAMBANDE

HIVI karibuni, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeanzisha huduma ya kubeba wagonjwa wasioweza kutembea kutoka kwenye kituo cha daladala kilichopo nje ya geti la kuingilia hadi katika maeneo ya kutolea huduma kwa kutumia viti mwendo (Wheel chairs).

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga wa MNH, Bi. Redempta Matindi alisema kuwa, huduma hiyo ni muhimu kwa kuwa wapo wagonjwa wasiojiweza kabisa kutembea wenyewe.

"Sisi kama watoa huduma za tumeona ni vema kuanzisha huduma hii kuwasaidia mwendo wagonjwa ili wafike kwenye maeneo ya kutolea huduma wakishafika huko wanakutana na watoa huduma wa maeneo husika."

Alisema, huduma hizo zinatolewa na waliokuwa waraibu wa dawa za kulenya ambao wanaendelea na tiba ya Methadone ili kuwasaidia kurejea katika maisha ya kawaida. Mshairi wa kisasa,Lwaga Mwambande anabainisha kuwa, huu ni ubunifu ambao ni faraja kwa Watanzania wote. Endelea;

1.Dasalamu Muhimbili, kofia twawavulia,
Hospitali ya ghali, Taifa twakimbilia,
Huduma zafika mbali, katika yetu dunia,
Asante kwa vitimwendo, kituo cha daladala.

2.Wagonjwa wengi wafika, tiba kuikimbilia,
Tembea wataabika, wanabaki wanalia,
Sasa hapo wakifika, vitimaguru tumia,
Asante kwa vitimwendo, kituo cha daladala.

3.Kama mewahi gonjeka, hili litakuingia,
Kuna muda unafika, mwili wote wasinzia,
Bila mtu kukushika, hapo waweza bakia,
Asante kwa vitimwendo, kituo cha daladala.

4.Muhimbili wameona, watu wajitabilia,
Vichwa vyao wamekuna, kuweza wasaidia,
Hili jambo jema sana, furaha kulisikia,
Asante kwa vitimwendo, kutuo cha daladala.

5.Huko ni kujali watu, hali inowazidia,
Wakifika bila mtu, kuweza wahudumia,
Huduma watapata tu, watakapozifikia,
Asante kwa vitimwendo, kituo cha daladala.

6.Muhimbili sante sana, mema mnatufanyia,
Vitimaguru twaona, wagonjwa watatumia,
Zile shida kubebana, hatuwezi zisikia,
Asante kwa vitimwendo, kituo cha daladala.

7.Wasiwasi kwa wagonjwa, huduma kuzifikia,
Kwamba wao watapunjwa, hali ikiwazidia,
Sasa imevunjwavunjwa, vitimwendo kuwadia,
Asante kwa vitimwendo, kituo cha daladala.

8.Wagonjwa ndio wateja, wale yawahudumia,
Muhimbili bora hoja, huduma kuzifikia,
Tuungane kwa pamoja, kuweza washangilia,
Asante kwa vitimwendo, kituo cha daladala.

9.Muhimbili kufanyika, vitimwendo tupatia,
Chagizo inahusika, kwingineko Tanzania,
Fanyeni ya uhakika, wagonjwa kusaidia,
Asante kwa vitimwendo, sipitali Muhimbili.

10.Wote wasiojiweza, tiba wanokimbilia,
Kufikia wakiweza, wapo kuwasaidia,
Waweze kuwasogeza, huduma kujipatia,
Asante kwa vitimwendo, sipitali Muhimbili.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news