Barabara ya Kidatu hadi Ifakara yafikia asilimia 87

MOROGORO-Ujenzi wa Barabara ya Ifakara-Kidatu wilayani Kilombero yenye urefu wa kilomita 66.9 ambayo imewahi kusababisha Mbunge wa Jimbo la Kilombero Abubakari Asenga kupiga magoti kwenye tope na kuiomba Serikali kuijenga kwa kiwango cha lami, sasa umefikia asilimia 87.
Muonekano wa Barabara ya Ifakara-Kidatu yenye urefu wa kilomita 66.9 ikiwa imekamilika kwa asilimia 87 kwa kiwango cha lami mkoani Morogoro.

Awali barabara hiyo ilikuwa ikiwafanya Wananchi watumie masaa matatu hadi manne kutoka Kidatu mpaka Ifakara, lakini baada ya kujengwa kwa kiwango cha lami sasa kunaifanya safari iwe ya kati ya dakika 45 hadi dakika 60.

Akizungumzia katika mahojiano Maalum na kipindi cha TANROADS mkoa kwa mkoa Mbunge huyo wa Jimbo la Kilombero, Abubakar Asenga, amesema awali barabara hiyo ilikuwa na changamoto nyingi, lakini Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan alisikia kilio cha Wananchi wake, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi,
Wizara ya Fedha na TANROADS wakaungana na kuanza ujenzi na sasa zaidi ya kilometa 47 kati ya 67 zimeshakamilika kwa kiwango cha lami na kipande kilichobaki kilomita 20 kutoka Signali kwenda Ifakara kinaendelea kujengwa.

‘’Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt.Samia maana tangu ameapa ndio tulipata kilometa ya kwanza, leo tunazungumza km 47 tayari zimejengwa, sisi huku ni wakulima,Ulanga, Mlimba na Malinyi wote ni wakulima wakubwa sana wa mazao mbalimbali ya chakula, ikiwemo mpunga na miwa kukamilika na barabara hii kutasaidia sana
kupunguza gharama za kusafirisha mazao na pembejeo za kilimo na hivyo kuongeza faida na uzalishaji kwa wananchi,"ameeleza Asenga.

Ameongeza kuwa, barabara hiyo ni muhimu kwani inaufungua mkoa wa Morogoro na kuunganisha kata zote za Wilaya ya Kilombero ikiwemo kata 14 za jimbo la Kilombero,pia Mlimba kuna barabara nyingine itajengwa mkataba wa ujenzi utasainiwa hivi karibuni ambayo itaungana na hii ya Kidatu-Ifakara kwenda mkoani Njombe.

Wakizungumza kwa niaba ya wananchi wenzao Bwana Timtim Izack na Razulu Hussein wamesema tangu kupata uhuru zaidi ya miaka 60 iliyopita, Kidatu-Ifakara hawakuwahi kuwa na barabara ya lami lakini ndani ya miaka miwili ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan madarakani amefanikisha, hivyo wameishukuru Serikali na viongozi wote waliowezesha kujengwa kwa barabara hiyo iliyopo Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news