Binti usijisahau, wewe pilau ya nyama

NA LWAGA MWAMBANDE

REJEA Biblia Takatifu katika kitabu cha Wimbo Ulio Bora 2:7,"Nawasihi enyi wanawake wa Yerusalemu, kama walivyo paa au swala wa porini, msiyachochee wala kuyaamsha mapenzi, hadi hapo wakati wake utakapofika."

Ukilitazama na kulitafakari neno hilo la Mungu utabaini kuwa, Biblia inawaagiza watu kutokuyachochea mapenzi hadi hapo wakati wake utakapofika yaani hadi ukiingia katika ndoa.

Aidha, neno la Mungu linamkataza kila mmoja ambaye hajaolewa au kuoa kwamba asiyachochee mapenzi. Muda wa kuyachochea mapenzi ni kipindi upo kwenye ndoa yako na utayachochea kwa mwenzi wako tu wa ndoa, na sio vinginevyo.

Kuchochea mapenzi ni kugusagusana kimapenzi na mtu wa jinsia tofauti na yako. Kuyachochea mapenzi ni kufanya mambo yanayokufanya utake kufanya ngono.

Pia, kuyachochea mapenzi ni kufanya vitu vya kukufanya uwake tamaa ya ngono. Kuyachochea mapenzi ni kuhamsha hamu ya ngono.

Biblia inakutaka usiyachochee mapenzi, kwani ukiyachochea mapenzi utajikuta unafanya dhambi mbaya ya uasherati.
 
Rejea katika Biblia Takatifu kitabu cha Waefeso 5:3-5, ''Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu.

"Wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru. Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu."

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,binti unaweza kubaki salama iwapo utatambua thamani na kusudi aliloweka ndani yako Mungu ili uweze kufikia malengo yako, kwani bila kujiingiza katika ngono inawezekana, subiri wakati wako utafika. Endelea;


1.Kuna tabia fulani, walizonazo wanyama,
Kichunguza kwa makini, ndizo zawapa uzima,
Uhasama wa nyikani, wao wabaki salama,
Binti ukiiga hao, utabakia salama.

2.Yale mazingira yao, baadhi hao wanyama,
Na hata tabia zao, zikiigwa hizo njema,
Jinsi wanapona wao, mabinti na nyie soma,
Binti ukiiga hao, utabakia salama.

3.Kule kuwaka tamaa, kwa mabinti siyo vema,
Huweza zua balaa, na hata mbele kukwama,
Ni kwa ayala na paa, wafaa hao wanyama,
Binti ukiiga hao, utabakia salama.

4.Sifa ayala na paa, wako makini wanyama,
Si kizembe wanakaa, katikati ya wanyama,
Hukuti wamezubaa, kirahisi wawe nyama,
Binti ukiiga hao, utabakia salama.

5.Hapa binti wafundishwa, ili ubaki salama,
Uache kukaakaa, kama nazi na mgema,
Mambo ya kwako andaa, si gogo la kusukuma,
Binti ukiiga hao, utabakia salama.

6.Umakini wa ayala, kwenye kundi la wanyama,
Japo majani akula, anawindwa awe nyama,
Kwa hiyo kulalalala, uhai waweza koma,
Binti ukiiga hao, utabakia salama.

7.Nawe binti kama paa, wazungukwa na wanyama,
Wengi wajaa tamaa, ili kwao uwe nyama,
Kama wewe wazubaa, utaliwa nyama choma,
Binti ukiiga hao, utabakia salama.

8.Paa ayala pilau, mlo ambao ni mwema,
Kwa sherehe angalau, kula hiyo huwa vema,
Kamwe hawajisahau, kwa chui wasiwe nyama,
Binti ukiiga hao utabakia salama.

9.Binti usijisahau, waume wengi ni noma,
Wewe sio kaukau, kutafuna meno homa,
Binti usijidharau, wewe pilau ya nyama,
Binti ukiiga hao, utabakia salama

10.Wewe unapita zako, kazini au kusoma,
Wanaume kando yako, tamaa wapata homa,
Akili kichwani mwako, usitegwe ukakwama,
Binti ukiiga hao, utabakia salama.
(Wimbo ulio Bora 2:7)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news