CCM Kinondoni yajiwekea lengo

DAR ES SALAAM-Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam kimesema kuwa kimejipanga vizuri katika kuhakikisha hadi Desemba, mwaka huu kinakuwa na mtaji wa kutosha wa wanachama.

Pia,katika kuhakikisha kinafikia malengo kimesema kuwa, tayari kimewahimiza wenyeviti na viongozi wengine kuhubiri mshikamano, kutatua na kusikiliza kero wanazokumbana nazo wananchi na kuzipatia ufumbuzi.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Shaweji Mkumbula wakati akielezea kuhusu malengo ya chama hicho.

"Kinondoni iko salama, na tumesema Agosti 31, mwaka huu kila nafasi ambayo haina kiongozi yaani iko wazi iwe imekamilika.

"Awali tulifanya ziara kwa lengo la kuweka mambo sawa katika kata na matawi na kuwaambia kufika Desemba tuwe tumefikia idadi ya wanachama tuliojiwekea malengo."

Amesema, uongozi wa wilaya haukuishia hapo badala yake wanazunguka katika kata, matawi na maeneo mengine katika kutaka kutatua changamoto mbalimbali na kwamba hawakuishia hapo badala yake walienda mbali zaidi kwa kuwaagiza wabunge, madiwani na wenyeviti kuwa washuke chini kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa, katika kufikia malengo yajayo kila jambo linalolalamikiwa na baadhi ya wanachama ambalo ni la kukijenga chama linashughulikiwa kwa haraka na kusema kuwa na kama mtendaji yeyote wa kata anajiona mkubwa zaidi ya viongozi wa wilaya basi atakaa pembeni ili chama kiendelee kuwahudumia wananchi.

"Lakini tunamshukuru Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan kwani mbali na hayo pia tumepata Mradi wa DMDP wa Barabara ambapo kila kata ina uwezo wa kupata walau barabara moja ambapo ni sawa na kilomita 57 sawa na asilimia 30.

"Hivyo bado kuna asilimia 70 tukizipata, tutakuwa tumepata barabara kwa asilimia zote, lakini pia nasifu ushirikiano ninaopewa na viongozi walioteuliwa na Rais Dkt.Samia na pia nawapongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mkurugenzi na viongozi wengine kwani tunafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa sana,"amesema.

Amesema, wana Kinondoni wanampenda Rais Dkt.Samia na wataendelea kumuunga mkono kwa hali na mali katika utekelezaji wa majukumu yake nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news