NA GODFREY NNKO
MKURUGENZI wa Bandari ya Dar es Salaam,Mrisho Mrisho amesema, ili Serikali iweze kutoa huduma bora kwa wananchi vijijini na mijini kwa wakati, uwekezaji mkubwa unahitaji katika bandari hatua ambayo itaongeza ufanisi na kutunisha mapato ya Taifa.
Ameyasema hayo Julai 21, 2023 wakati wa kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini ambao pia walipata nafasi ya kujionea uendeshaji wa shughuli za bandari hiyo jijini Dar es Salaam.
Mrisho amesisitiza kuwa, katika majadiliano yanayoendelea kati ya Serikali na mwekezaji ili kuongeza ufanisi wa bandari hiyo, gati namba nane mpaka 11 na eneo la mafuta hayapo katika makubaliano ya maboresho ya bandari.
"Gati namba nane mpaka gati namba 11 halipo kwenye majadiliano, eneo la mafuta halipo kwenye majadiliano. Biashara ni ushindani, lakini vile vile biashara ni suala zima la gharama, hivyo ushirikishwaji wa wawekezaji ni jambo jema.
"Tunataka kufanya maboresho makubwa zaidi, ikiwemo kuunganisha magati ili kuendelea kuhudumia shehena ya makasha (makontena), kwa hiyo kuna development ukitazama master plan na bajeti zetu zilizopo, hii bandari itaendelea kujengwa.
"Tukijenga tunatafuta Dubai mwingine, tunamwambia endesha, kwa hiyo tunazungumzia mmoja, hapana, bandari inatakiwa iwe na watu wengi zaidi wa kuongeza huo ufanisi.Yaani siyo Dubai tu,na mwingine na mwingine, ndiyo utendaji."
Uhusiano
"Hauwezi kuizungumzia Bandari ya Dar es Salaam pasipo kuizungumzia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kwa hiyo Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania kwa maana ya TPA ipo kwa mujibu wa Sheria ya Bandari namba 17 ya mwaka 2004.
"Na kwa mujibu wa sheria hiyo, kuna wajibu au kuna majukumu waliyopewa kufanya, moja ni kusimamia shughuli za bandari Tanzania,lakini la pili ni kuendesha shughuli za bandari.
"La tatu ni kuendeleza shughuli za bandari, na la nne kukasimisha baadhi ya majukumu.Lakini, kwenye sheria hiyo niliyoisema inajumuisha sasa, bandari zote zilizopo kwenye bahari na bandari zote zilizopo kwenye maziwa.
"Kwa mtiririko bandari zilizopo kwenye bahari unaanza na Bandari ya Dar es Salaam kwa ukubwa wake, kwa rasilimali zake na kwa ukubwa wa shughuli zake.
"Kwa hiyo, ndiyo bandari kubwa iliyopo sasa. Halafu ya pili ni Bandari ya Tanga kwa ukubwa na Bandari ya Mtwara, lakini kwa namna ambavyo maboresho yanaendelea kwenye Bandari ya Mtwara na Tanga hawa watashindana wenyewe.
"Sijui nani atakuwa mkubwa. Kwa sababu ukitazama Mtwara wanapambana kweli kweli. Ukienda kwenye maziwa tunaanza na Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa. Sasa mwingine anaweza kujiuliza tuko Dar es Salaam mbona tena kuna Bandari ya Bagamoyo, Nyamisati, Kisiju na Mafia.
"Sasa, kila bandari hizi nilizozitaja sita kwa ukubwa pia kuna bandari ndogo ndogo inategemea ipo wapi na inasimamiwa na nani.
"Kwa mfano Bandari ya Dar es Salaam inasimamia bandari ndogo ya Bagamoyo, Bandari ndogo ya Mbweni, Nyamisati, Mafia, Kisiju hizi zinasimamiwa na Bandari ya Dar es Salaam.
"Ukienda kadhalika Mtwara kule utaona Bandari ya Lindi, Bandari ya Kilwa hizo zinasimamiwa na Bandari ya Mtwara. Kwa hiyo huo ndiyo mpangilio, lakini kwa ukubwa wake Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania inasimamia bandari kubwa sita, tatu kwenye bahari na tatu kwenye maziwa."
TPA ni nini?
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ilianzishwa kwa Sheria ya Bandari Na.17 ya 2004 kusimamia shughuli zote za kibandari nchini.
Mamlaka hii inaendesha bandari zinazohudumia Tanzania na nchi zisizo na bandari ikiwemo Zambia, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, Rwanda, Malawi, Uganda na Zimbabwe.
Aidha,TPA inatekeleza jukumu la kuhamasisha matumizi ya bandari, kuziendeleza na kuzisimamia ikiwemo, kuingia mikataba ya kisheria ya kukasimu mamlaka yake kupitia utoaji ruksa za uendeshaji wa huduma za bandari kwa kufuata kanuni na mamlaka iliyonayo kwa mujibu wa sheria.
Mamlaka hiyo inasimamia na kuendesha mifumo ya kibandari katika bandari zilizo mwambao wa Bahari ya Hindi na kwenye maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.
Dar es Salaam, Tanga na Mtwara ndio bandari kubwa huku bandari ndogo zikiwa Kilwa, Lindi, Mafia, Pangani na Bagamoyo katika mwambao wa Bahari ya Hindi.
Bandari ya Dar es Salaam
"Sasa kwa sababu leo tupo Bandari ya Dar es Salaam, mimi nitajikita zaidi kuizungumzia bandari hii ambayo ndiyo ninayoisimamia na kuiongoza.
"Bandari ya Dar es Salaam ni bandari kubwa, bandari kubwa kwa eneo, bandari kubwa kwa shughuli zake kwa sababu ukizungumzia zaidi ya asilimia 90 ya shughuli za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, shughuli kubwa zinatokana na Bandari ya Dar es Salaam hata ukizungumzia kwenye mapato.
"Kwa hiyo ndiyo ng'ombe wa maziwa na ndiyo maana wengi sana tunajadili hapa Bandari ya Dar es Salaam, hata mapato ya kikodi, mapato ya kiforodha asilimia 37 hadi 40 ukisikia ndugu yetu Kidata (Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Alphayo J. Kidata) ametangaza taarifa ya mapato, basi asilimia kubwa yametoka katika eneo hili la Bandari ya Dar es Salaam.
"Kwa hiyo, ukubwa wake ni kwa sababu ya umuhimu wake, sensitivity yake katika uzalishaji wa mapato ya nchi hii, sasa ukitazama Bandari ya Dar es Salaam, shughuli hasa tunazozifanya ni zipi, zamani tulikuwa tunasema shughuli za bandari ni kupakia na kupakua.
"Hapana, katika uendeshaji wa kileo, bandari inapaswa kufanya kazi zaidi ya hapo, kwa hiyo lazima ujue mizigo inatoka wapi, unau-trace mzigo huko uliko unauangalia mpaka unafika katika eneo lako, na kuuangalia kama ni mzigo huo ndiyo unaovuka kwa ajili ya soko la ndani au kutolewa nje ya nchi.
"Kwa hiyo, huo ndiyo uendeshaji wa kileo wa bandari,kikubwa zaidi tunahudumia shehena, tunahudumia meli kwenye bandari zetu.
Uongozi
"Sasa bandari hii ya Dar es Salaam, ina ungozi wake ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu na chini yake kuna mameneja wa bandari ambao wanasimamia vitengo mbalimbali.
"Na jambo la msingi ambalo unapaswa kufahamu ni Bandari ya Dar es Salaam tu ndiyo unampata Mkurugenzi kwa sababu ya ukubwa ambao nimeuelezea awali."
Ikumbukwe kuwa, Bandari ya Dar es Salaam ni lango la kuu la kibiashara, kwani asilimia 95 ya biashara ya Kimataifa ya Tanzania inahudumiwa na bandari hiyo.
Pia, bandari hiyo inahudumia nchi jirani zisizo na bandari kama vile Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, Rwanda, Malawi, Uganda na Zimbabwe.
Bandari ya Dar es Salaam inatajwa kuwa ni kiungo kikuu cha kibiashara si tu kutoka na kwenda nchi za Afrika Mashariki na kati, bali pia na nchi za Mashariki ya Kati, Mashariki ya Mbali, Ulaya, Australia na Marekani.
Mkurugenzi Mkuu, Mrisho ameendelea kufafanua kuwa,"Ukienda Bandari ya Tanga, Mtwara kule utawakuta mameneja wa bandari, hauwezi kumkuta Mkurugenzi wa Bandari kwa hiyo, Bandari ya Dar es Salaam imepewa heshima ya kuwa na Mkurugenzi Mkuu kutokana na umuhimu wake.
"Kwa hiyo, Bandari ya Dar es Salaam ina mameneja wake, mameneja hao, kwa mfano Meneja wa Kitengo cha Shehena Mchanganyiko, Kitengo cha Mafuta na wengineo wanasaidia ili shughuli za bandari kufanyika kwa wepesi."
Malalamiko
"Niseme kitu kimoja, mwaka 2011 mpaka mwaka 2016 Bandari ya Dar es Salaam ilipita kwenye kipindi kigumu sana cha malalamiko ya wateja wanaohudumiwa na bandari hii, tangu mwaka 2011 mpaka mwaka 2016 malalamiko katika Bandari ya Dar es Salaam yalikuwa mengi hasa kwenye eneo la utoaji huduma.
"Sisi, wateja wetu wamegawanyika katika makundi mawili, wanaoleta meli na wale wanaohudumia mizigo, wamegawanyika katika maeneo hayo, waliokuwa wanaleta meli walikuwa anailalamikia Bandari ya Dar es Salaam kwenye maeneo yafuatayo.
Sababu
"Moja, udogo wa kina cha bandari, kulikuwa na matatizo makubwa, kina kilikuwa kidogo tukitazama kwenye magati yetu kwa wakati ule kina kilikuwa mita nane ni moja tu lilikuwa na angalau kina cha mita 10.
"Kwa hiyo meli zilizokuwa zinakuja katika Bandari ya Dar es Salaam wakati ule zilikutana na tatizo la shallow water. Wakati huo, ukiwa na meli yenye uzito wa tani takribani elfu 30 hadi elfu 40 ilibidi kwanza uichukue hiyo meli uipeleke base namba saba ipunguze mzigo, ndiyo uilete kwenye haya magati mengine, hilo lilikuwa la kwanza.
"Tatizo la pili, ni uduni wa miundombinu ya kuhudumia shehena kwa maana magati yetu yalikuwa na matatizo makubwa, kwa maana ya uchakavu na hayakuwa na ufanisi uliotakiwa.
"Lakini, tatizo la tatu ni uhaba wa vifaa,kwa maana ya vitendea kazi, na tatizo lingine lilikuwa ni tatizo la mifumo kwa maana ya mifumo ya utendaji kazi katika bandari kulikuwa na tatizo.
"Matatizo yale yalitusababishia kwanza kuhudumia shehena ndogo sana kwenye bandari hii, na hata mapato yalikuwa madogo, sasa kilichofanyika mwaka 2016/2017 Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikalazimika kutafuta fedha duniani, yaani Benki ya Dunia na maeneo mengine.
DMGP
"Na kuanzisha mradi mkubwa wa maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam, mradi huo unatambulika kwa jina la DMGP-Dar es Salaam Maritime Gateway Project (Mradi wa Lango la Bahari la Bandari ya Dar es Salaam). Huu mradi ni wa uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam.
"Mradi huu ulianza mwaka 2017, vitu vilivyokusudiwa kufanyika kupitia mradi huu ni kujenga gati jipya kwa ajili ya kuhudumia shehena ya magari katika Bandari ya Dar es Salaam, kwa hiyo component ya kwanza ya DMGP ulikuwa ni ujenzi wa gati jipya la kuhudumia shehena za magari, kazi hiyo ilifanyika.
"Gati lilijengwa la urefu wa mita 300, componet ya pili ni ujenzi wa yadi kubwa kwa ajili ya kuhifadhia shehena ya magari, yadi hiyo ilijengwa na ina ukubwa wa mita za mraba 72,000 na ina uwezo wa kuhifadhi magari 6,000 kwa wakati mmoja.
"Componet nyingine ya tatu ya DMGP ni uboreshaji wa gati namba moja mpaka namba saba, kwa hiyo gati namba moja mpaka gati namba saba yaliboreshwa. Na component ya nne, ni kushimba kina cha bandari kina kilichimbwa kutoka mita nane, saba mpaka kufikia kina cha mita 14.5."
"Na component inayofuata kwenye DMGP ni kupanua mlango wa kuingia meli, ili kuruhusu hata meli ambazo si za kizazi cha chako cha sasa, ziweze kuingia Bandari ya Dar es Salaam, kwa sababu kina umeshaongeza kwa hiyo utakuwa na uwezo sasa wa kuruhusu meli kubwa kuingia kwenye bandari na kuweza kuzihudumia kwa urahisi zaidi.
"Miradi hii ilikuwa inaenda na kila mmoja ulikamilika kwa wakati wake gati la RoRo (Roll-on, Roll-off) ilikamilika mwaka 2018 na kuanza kazi. Base namba moja mpaka base namba nne ulikamilika 2019/20 na gati namba tano hadi namba 7 yalikamika mwaka 2021/22.
"Kwa hiyo maeneo hayo yalikamilika na sisi tunaendelea kuyatumia kuhudumia shehena, kwa hiyo gati namba saba hatukuwa na eneo la kuhifadhi makasha, kwenye mradi huu tumepata eneo maalum la kuhifadhi makasha (makontena)
"Na makasha yanaweza kuwekwa katika eneo hilo, zaidi ya makasha 10,000 kwa wakati mmoja. Kwa hiyo mradi kwa maana ya Serikali ilichukua hatua hizo ili kuboresha bandari, ikiwemo maboresho makubwa zaidi kwa upande wa usalama,na kwa sasa hauwezi kusikia kelele kama wakati ule."
"Miradi hii, ilirejesha imani kwa watumiaji wa Bandari ya Dar es Salaam, hivyo walirudi na waliendelea kuitumia na mizigo iliongezeka.
"Tulitoka tani milioni 14, kwa wakati ule bandari zote zilihudumia tani milioni 18 mwaka 2021/22,kwa hiyo taasisi nzima kwa maana ya TPA kupitia bandari zote zilihudumia tani milioni 18 kutoka kwenye zile tani milioni 14 kushuka chini.
"Kwa kituo ambacho mimi ninakiongoza 2021/2022 tulihudumia tani milioni 15, jambo nzuri la kufurahisha, tumefunga mwaka kwa maana ya mwezi Juni, mwaka 2023 Bandari ya Dar es Salaam tumehudumia tani milioni 21,271,000."
Mkurugenzi Mkuu huyo wa Bandari ya Dar es Salaam amesema, mafanikio hayo yamevuka lengo walilowekewa na Serikali la kuhudumia mizigo tani milioni 19.6.
Mrisho tena
"Sasa ukitazama tani milioni 21.27 kutoka kwenye tani milioni 18 na pia kutoka kwenye lengo tulilopewa la tani milioni 19.6, nadhani unaweza kuona hiyo asilimia iliyoongezeka hapo, na ukifanya tathimni ya mizigo tuliyohudumia katika Bandari ya Dar es Salaam ni chini ya tani milioni 10 tulizohudumia ambazo ni za nchi jirani.
"Kama, tunasema hivi sasa ukichukua kwenye market shares kwenye zile nchi tunazohudumia anza Burundi, Rwanda, Uganda, Congo, Zambia, Malawi na sasa tupo Zimbabwe kuna makadirio kwamba katika hizi nchi ambazo tunahudumia jirani kuna tani zaidi ya milioni 70 kwa mwaka.
"Ni zaidi ya tani milioni 70 kwa mwaka, kwa hiyo soko lipo kwenye hizi nchi jirani, kama tuna tani milioni 21 huku chini ya tani milioni 10 ndiyo transit ina maana huku ndani tunatumia sana, kwa maana yake tuna tani zaidi ya milioni 60 sisi hatuzihudumii hapa Bandari ya Dar es Salaam
"Kwa nini hatuzihudumii?, Sijui kama nimeeleweka vizuri, kwamba soko ni kubwa, lakini bado hatufanya vizuri katika soko linalotuzunguka.
"Ifahamike kuwa, Bandari ya Dar es Salaam imekaa kimkakati sana kwani inahudumia corridors mbili, Dar es Salam corridor na Central corridor.
"Hii ni ruti fupi zaidi ukilinganisha na ruti ya Kaskazini ambayo inahudumiwa na Mombasa, hapa ni karibu zaidi kwenda Uganda,kwenda Congo, sasa unaweza kujiuliza zile tani milioni 60 ambazo hatujafanya vizuri kule, nani anazihudumia?.
"Maana yake, ushindani ni mkubwa basi Mombasa na bandari zinginezo ndiyo wanazihudumia, kwa hiyo unaona soko tayari lipo, watumiaji tayari wapo, mfano Congo DR ni soko kubwa kila mmoja anagombania hilo soko, anafungua migodi kila siku.
"Mpaka anakimbilia huko Lobito, kwa nini, kwa sababu ya changamoto ya bandari yetu,tunazungumzia maboresho je yametatua matatizo kwa asilimia 100? Congo tunahudumia, tunajipongeza mwaka huu tumelihudumia soko la Congo tani milioni 3.5, mwaka 2021/2022 soko la Congo tumehudumia tani milioni 2.9, mwaka huu tumejivuta tumehudumia tani milioni 3.5.
"Nje ya tani milioni 15 au tani milioni 20 tumeenda tukachukua market share ndogo. Uganda kwa sasa tunahudumia tani chini ya asilimia tatu, kwa nini tunamuhudumia chini ya asilimia tatu, kwa sababu anatumia Bandari ya Mombasa hatumii Bandari ya Dar es Salaam,kipindi fulani walifika hapa kuangalia fursa ya masoko, lakini changamoto walizokutana nazo hawakurudi tena."
"Niseme jambo, wakati fulani kwa asili ya matatizo ya Bandari ya Dar es Salaam ni kama vile unaweza kusema, Mwenyenzi Mungu anasema hizo meli zije.
"Meli hazitakiwi kuja kwa bahati mbaya ndugu, meli zinatakiwa kuja kwa mpango, mzigo unakuwa consolidated duniani, halafu unaustreem line kwenye bandari unayoitaka.
"Wakati fulani Bandari ya Dar es Salaam inahudumia hizi meli kwa sababu no option wanasema waje tu Bandari ya Dar es Salaam kutokana na jografia yake. Kwa hiyo, ufanisi wa bandari zetu ndiyo unaongeza mapato ya nchi hii,"amefafanua kwa kina Mkurugenzi Mkuu wa Bandari ya Dar es Salaam.
TPA
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),Mhandisi Juma Kijavara amesema kuwa,Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kujenga na kufanya maboresho makubwa ya bandari ili kuongeza ufanisi.
"Kwa hiyo, hili eneo la mafuta mnaloliona hapa si sehemu ya ule mkataba au kile ambacho kinatangazwa au kusemwa kuwa bandari yote wamepewa, kwa hiyo kuna vitu ambavyo tutaendelea kuendesha wenyewe.
"Mkurugenzi Mkuu kwenye bandari ile alisema kabisa, maximum ya meli ambayo inaweza kuingia pale, baada ya mlango ule kufunguliwa, itakuwa ni mita 305 za urefu wa meli ambapo meli kama hiyo, ina uwezo labda wa kubeba kontena 6,000.
"Lakini, duniani kwa sasa kuna meli moja inabeba kontena 24,000 kuna meli inabeba kontena 18,000 na kuna meli inabeba kontena 12,000 sasa hiyo inatupelekea sisi kama Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuiweka kwenye mipango yetu ya ujenzi Bandari ya Bagamoyo.
"Ambayo tunakwenda kuijenga kuanzia mwaka huu wa fedha, mpaka mwezi wa tisa tutakuwa tayari tumeitangaza kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa ujenzi, kwa sasa tuna tunakwenda moja kwa moja inajengwa na Serikali, tunaanza kuijenga Serikali.
"Sasa pale Bandari ya Bagamoyo ndipo ambapo tutapata kama alivyosema Mkurugenzi wa Bandari hapa kwamba, bandari zote duniani zina maeneo yale ya uchumi, ambayo inagenerate mzigo utoke na malighafi zitumike, lakini hapa tupate final products hayo yatafanyika pale Bandari ya Bagamoyo na ambayo itakuwa sasa na uwezo wa kuingiza hizo meli kubwa.
"Meli ambazo zina ukubwa huo, tutakwenda kuchimba kina mpaka cha mita 17,maji yakiwa yametoka. Tutaanza kujenga gati la mita 300 na mpaka hapo tutaendelea kuongeza mpaka tupate kilomita tatu za magati.
"Yaani tunakwenda kujenga bandari kubwa sana pale Bagamoyo, lakini sasa hii yote, sisi kama TPA tutaanzisha, lakini uwekezaji mkubwa kama huo hauwezi kuufanya peke yako, kwa hiyo bado tunaendelea na utaratibu wa kuangalia nani tutasaidiana naye, kwenye ujenzi mkubwa kama huo ili tupate matokeo makubwa.
"Kwa hiyo pale makadirio mpaka ikamilike tunahitaji takribani rilioni tatu kwa haraka haraka, sasa hivyo ni vitu ambavyo, vinahitaji ushirikiano.
"Mkurugenzi wetu wa Bandari amesema, tani milioni 21.27 hizo zimehudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam pekee, toka tani zilizohudumiwa na bandari zote zote za mamlaka ambazo ni sita. Lakini kwa mwaka huu, tunavyoongea Bandari ya Dar es Salaam pekee imehudumia tani milioni 21.27
"Kwa hiyo, kelele lazima ziwepo, Dar es Salaam hii kuna shamba? Dar es Salaam hii kuna mtu mwenye shamba la hekari 300, hekari 400? Shamba hilo hapo, lazima kelele ziwe nyingi.
"Kwa hiyo, Serikali inaendelea na juhudi mbalimbali za kufanya maboresho na uendelezaji wa bandari ili ziweze kuwa na tija kwa uchumi wetu.
Mbali na hayo amesema, Serikali imedhamiria kuifanya Bandari ya Dar es Salaam iweze kuhudumia me;li nyingi zaidi kwa wakati mmoja.
Tags
Bandari ya Bagamoyo
Bandari ya Dar es Salaam
Habari
Makala
Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Tanzania