Fauluni tufurahi

NA LWAGA MWAMBANDE

JULAI 13, 2023 Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya Kidato cha Sita mwaka 2023 huku yakionesha ufaulu wa jumla umeongezeka kwa asilimia 0.26 ikilinganishwa na mwaka jana 2022.
Katibu Mtendaji wa NECTA, Dkt.Said Mohamed amesema, jumla ya watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani ni 106, 883 huku wasichana wakiwa ni 47, 340 na wavulana 59, 543.

Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande licha ya kuwatakia kila la heri wanafunzi wote kwa hatua inayofuata nchini, pia ameendelea kusisitiza bidii darasani kwa matokeo bora zaidi. Endelea;


1.Ni wazazi pande mbili, kwa mwonekanao wao,
Wengine furaha kweli, wakiwaenzi wanao,
Wengine hawana hali, matokeo ya wanao,
Watoto wetu tambua, elimu yenu ni yetu.

2.Watoto wetu tambua, elimu yenu ni yetu,
Hatua tumechukua, kwa hizi gharama zetu,
Kufanya kuwainua, shuleni mpate kitu,
Mnapofanya vizuri, nasi mwatufurahisha.

3.Mnapofanya vizuri, nasi mwatufurahisha,
Tunatamba siyo siri, matokeo twaonesha,
Lakini zenu sifuri, kweli mwatusononesha,
Mnapokuwa shuleni, fikiria na wazazi.

4.Mnapokuwa shuleni, fikiria na wazazi,
Bidii ni ahueni, hata kuwe matumizi,
Uzembe mwachoma ndani, maumivu kwa wazazi,
Kama kweli mwatupenda, hebu tupeni furaha.

5.Kama kweli mwatupenda, hebu tupeni furaha,
Msitufanye kukonda, matokeo ya kijuha,
Ndiyo hivi twawafunda, soma achene kuhaha,
Tupeni raha wanetu, kwa matokeo mazuri.

6.Tupeni raha wanetu, kwa matokeo mazuri,
Huko shule chota kitu, mzidi kuwa mahiri,
Hata kwenye vyuo vyetu, michezo siyo mizuri.
Mahafali zikifika, nasi tuje tuwapambe.

7.Mahafali zikifika, nasi tuje tuwapambe,
Tubaki hangaika, mlivyofeli kizembe,
Tutazidia kuchoka, haraka macho tufumbe,
Elimu yenu ni yetu, tusonge mbele pamoja.

8.Elimu yenu ni yetu, tusonge mbele pamoja,
Ninyi ni watoto wetu, kwa hili tuwe wamoja,
Laleta heshima kwetu, wa bara hata Unguja,
Hebu fanyeni bidii, msizembeezembee.

9.Hebu fanyeni bidii, msizembeezembee,
Maelekezo mtii, ya kielimu pekee,
Yasofaa yote zii, wala msisogelee,
Elimu ni ufunguo, wa kuyaweza maisha.

10.Elimu ni ufunguo, wa kuyaweza maisha,
Hilo la kwenu chaguo, vema kulithibitisha,
Someni bila kituo, hadi mwisho wa maisha,
Fauluni tufurahi, tuongezee miaka.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news