NA ADELADIUS MAKWEGA
WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kuwa sasa halmashauri zote nchini na waajiri wote wanayo fursa kubwa ya kuwapata wataalamu wa michezo wanaohitimishwa kila mwaka katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kilichopo Kwimba mkoani Mwanza.
Hayo yamesemwa na Balozi Dkt. Chana alipohudhuria mahafali ya 12 ya Chuo hicho Julai 15, 2023 ambapo alikuwa mgeni rasmi.
“Naziomba halmashauri zote zitambue mahitaji ya walimu wa michezo katika maeneo yao, ili mahitaji hayo yawasilishwe mamlaka husika na nafasi hizo ziweza kujazwa mapema mara baada ya mawasilisho yao.”
Waziri Chana alisema kuwa Bajeti ya 2023/2024 imepitishwa na Bunge letu, hivyo kubwa ni kuimarisha michezo, huku akitoa wito kwa Halmashauri zote nchini kulinda maeneo yote ya michezo ili kutoa nafasi ya Watanzania kuweza kushiriki katika michezo, maeneo hayo lazima yawe na hati na kuwe na programu mbalimbali za michezo kila siku.
“Naashukuru sana kwa kumuona Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana kwa kuwa mgeni rasmi katika mahafali haya na hilo litabakia katika historia ya maisha yangu. Uwepo wa Waziri Chana una maana kubwa kwangu, una maana nzito kwa tasnia niliyosomea na maana kubwa kwa taifa langu la Tanzania.”
Mahafali hayo yalihudhuriwa na viongozi kadhaa akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini na viongozi wengine wa chama na serikali.