Hii hapa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA)

MWANZA-Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) imeendelea na mikakati mbalimbali kuhakikisha wananchi wote wanapata maji safi na salama kwa saa 24.

Sambamba na kupata huduma ya uondoshaji wa maji taka kwa wakati ili kuendelea kuyafanya mazingira kuwa bora kwa ustawi bora wa wananchi na Jiji la Mwanza.

MWAUWASA ambayo imesheheni timu ya wataalamu wenye weledi na uzoefu wa muda mrefu kwenye sekta ya maji,wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zaidi jijini humo.

Leo, Julai 29,2023 ungana na Mohamed Saif, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kukupa majawabu ya baadhi ya maswali yako.Endelea;
 
MWAUWASA nini?

"Mamlaka ya Maji Safi na Mazingira kama tulivyotanguliza jina lenyewe linahakisi kazi yenyewe ambayo inafanywa na mamlaka, ni mamlaka ya maji safi yaani tunahusika na usambazaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi, na pia tunahusika na huduma ya uondoshaji wa maji taka.

"Ni vitu viwili tunafanya, tunahusika na kupeleka maji safi kwa wananchi na kuondoa maji taka kwa wananchi, hasa ikumbukwe kwamba yale maji safi unayopelekewa wewe baadaye yanageuka kuwa maji taka, kwa hiyo tunayaondoa tena."

Hali ya huduma ya maji Mwanza ipoje?

"Huduma ya maji kwa ujumla kwa sasa hivi, labda nieleze kwa upana zaidi ili tuweze kwende sawa, ni kwamba kwa sasa tunacho chanzo kikubwa hapo maeneo ya Capri Point cha maji,tuna dakio letu pale ndipo tunapochukulia maji kwa wakazi wa Mwanza.

"Sasa pale, chanzo chetu uwezo wake ni kuzalisha lita milioni 90 kwa siku, na mahitaji kwa sasa ni zaidi ya lita milioni 160, kwa hivyo hadi hapo ninafikiri utakuwa umeelewa hali ya huduma ya maji ikoje kwa jiji letu la Mwanza."

Hali ipoje maeneo ya pembezoni?


"Kutokana na uhitaji kuwa mkubwa kuliko kile ambacho sisi tunazalisha, hii imepelekea tuwe tuna migawo kwa baadhi ya maeneo, hususani maeneo ya pembezoni mwa jiji letu la Mwanza.

"Na, hususani maeneo ya miinuko tunakuwa tuna migawo kama unavyoona hapa tuna migawo yetu ya maji ambayo tuliiainisha kwa wananchi, na yote hii ni kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na huduma ya maji safi na salama."

Vipi kuhusu wale ambao wanakaa muda mrefu bila maji?


"Ni kweli, lakini tumejipanga kuhakikisha kwamba wananchi wote tunaowahudumia wanafikishiwa huduma ya maji safi na kama nilivyosema hapo awali ni kwamba uzalishaji wetu umekuwa ni mdogo ukilinganishwa na mahitaji na ndiyo maana kumekuwa na migawo.

"Migawo hii imelenga kuhakikisha kwamba wananchi wote wananufaika na huduma ya maji, ni kweli wakati mwingine migawo imekuwa ni changamoto kwenye baadhi ya maeneo.

"Changamoto hiyo, kuna sababu ambazo zipo nyingi ambazo zinasababisha migawo,ya kwanza kabisa ni suala la umeme, ikumbukwe kuwa jiji letu la Mwanza limebarikiwa kuwa ni jiji la miamba, tuna maeneo mengi yenye miinuko.

"Kwa hivyo, na maji siku zote hajapandi milima, hivyo basi zinahitajika nguvu za ziada kuhakikisha maeneo yote yanapata maji, nguvu zipi ambazo hizi ninaziongelea? Ni busta station, tuna mitambo ya kusukuma maji.

"Si kwamba tu maji yanafunguliwa kule yanakwenda, hapana. Yanahitaji msukumo wa ziada, kwa maana hiyo kwa mfano, maji leo tunayaelekeza upande wa Kusini, mathalani mitambo yetu tunai-set kuelekea huko, lakini bahati mbaya sana ikatokea labda limetokea katizo la umeme, kukitokea katizo la umeme ina maana mitambo haiwezi kufanya kazi.

"Kwa maana hiyo, usukumaji wa maji kwenda kwenye eneo fulani ambalo lilipaswa kupata maji siku hiyo, yaani ni siku ya mgawo, wa eneo hilo unashindwa kufanyika kiufanisi, kwa sababu umeme hakuna.

"Hiyo ni moja ya changamoto ambayo inachangia, lakini tunajitahidi, ikitokea umeme hakuna tunawafahamisha wananchi, na tunajitahidi kuhakikisha kwamba tunafidia huo mgawo.

"Mgawo wetu, kwa mfano ulikuwa labda tunapeleka maji Nyegezi mfano, ikatokea tumepata hitilafu yoyote ile iwe ya mitambo yetu, iwe ya umeme au hitilafu yoyote ambayo inaweza kujitokeza tunahakikisha tunafidia huo mgawo. Ndivyo tunavyokwenda."

Kuna jitihada zozote za kukabili changamoto?


"Ndiyo zipo, kuna jitihada ama harakati tulizonazo za kuhakikisha kwamba tunakwenda kuimarisha huduma ya maji. Nini kinafanyika? Kwanza, awali ya yote tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan.

"Wametambua kwamba, jiji letu la Mwanza lina upungufu na wametupatia fedha zaidi ya shilingi bilioni 69 kwa ajili ya kujenga mradi mwingine, tunashukuru sana mradi huu ulikwishaanza na hivi tunapozungumza upo zaidi ya asilimia 86 ya utekelezaji.

"Nazungumzia hapa ujenzi wa chanzo ama dakio jipya la maji eneo la Butimba ambalo tunatarajia litanufaisha zaidi ya wananchi laki nne na hamisini wa maeneo mbalimbali kama Nyegezi, Mkolani, Buhongwa, Lwani, Mafu, Magila, Sawa, Igoma, Kishiri, Nyamongoro na,

"Kwa upande wa Misungwi tuna eneo la Usagara, Nyashishi, tuna Fela, lakini upande wa Magu kwa sababu tuna baadhi ya maeneo pia tunayahudumia ambayo ni Kisesa, Bujora na Isangiro, haya yatanufaika ni kwamba chanzo chetu hiki kipya tunachoendelea nacho sasa hivi,ambacho kimefikia asilimia zaidi ya 86 kinajengwa kwa awamu.

"Awamu ya kwanza ambayo hii tunaendelea nayo itatupa lita milioni 48 (kwa siku), kwa hivyo zile tisini ukiongeza na 48 tutakuwa tumepunguza kwa kiasi kikubwa sana, lakini mbali na hivyo, uwezo wote wa chanzo hiki ni kuzalisha lita milioni 160, huo ni mkakati wa kwanza ambao tunaendelea nao na hivi karibuni mambo yatakwenda kuwa vizuri.

"Na mkakati wa pili ambao tunaendelea nao ni mazungumzo na wadau, mazungumzo na washirika wa maendeleo ya ujenzi wa chanzo kingine kipya, kikubwa zaidi kuliko vyote ambavyo tunavyo, matarijio kwamba chanzo hiki kitatupa zaidi ya lita milioni 200.

"Kwa hiyo tutakuwa vizuri sana, mbali na hivyo tuna harakati ambayo tunaendelea nayo sasa hivi ya utanuzi wa chanzo chetu cha Capri Point, tunatarajia kitakuwa na uwezo zaidi, kwa hiyo tunakwenda vizuri zaidi,"amefafanua kwa kina Mohamed Saif.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news