Hii hapa TPDC, fahamu kwa nini ndiyo mkono wa Serikali

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Bw.Mussa Makame amesema, shirika hilo ndiyo mkono wa Serikali katika sekta ya mafuta na gesi nchini.

Ameyasema hayo leo Julai 20,2023 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na shirika hilo na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) uliondaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ikiwa ni mwendelezo wa taasisi na mashirika yaliyo chini ya ofisi hiyo kueleza shughuli mbalimbali wanazozifanya kwa ustawi bora wa taasisi husika na Taifa.

"Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania yaani TPDC ukiliangalia ni mkono wa Serikali katika usimamizi wa sekta ya mafuta na gesi. Na shughuli yake kubwa ni kutafuta, pale ambapo tukifatuta tukiona basi tunaendeleza, tunachakata, tunasafirisha na kusambaza nishati ya mafuta na gesi asilia."

Makame amebainisha kuwa, shirika hilo lilianzishwa mwaka 1969 na mpaka sasa ukiondoka shirika hilo mama lina kampuni tanzu mbili ambazo ni Kampuni ya Gesi Tanzania (GASCO) na Kampuni ya Mafuta ya TANOIL.

"GASCO (Gas Supply Company Limited) inashughulika na kusimamia miundombinu ya uchakataji,usafirishaji na usambazaji wa gesi asilia, halafu tuna kampuni tanzu nyingine inaitwa TANOIL ambayo yenyewe ipo katika biashara ya mafuta.

"Vile vile TPDC kuanzia mwaka 2021 kupitia ule mfumo wa uingizaji wa mafuta kwa pamoja, TPDC nayo imeingia katika kushindania zile zabuni za uingizaji yale mafuta safi kutoka nje ya nchi kwa ajili ya matumizi ya magari na matumizi mengine.

TPDC imeeleza kuwa, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, itaendelea kufanya kazi kwa kasi na kiwango cha hali ya juu na kwa weledi mkubwa ili kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa na shirika hilo inafanikisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa.

"Kwa hiyo, kama nilivyosema tuna hizo shughuli kwenye mikondo hiyo miwili tofauti, mkondo wa utafutaji na uendelezaji na usambazaji wa mafuta na gesi, lakini vile vile kuingiza mafuta kutoka nje pamoja na kuyafanyia biashara ya usambazaji humu ndani.

"Mpaka sasa, kwenye upande wa gesi asilia, na wengi mtakuwa mnafahamu kwamba, tayari tuna vitalu viwili ambavyo vipo katika hatua ya uzalishaji, yaani kitalu cha Songogongo ambacho kinazalisha gesi inasafirishwa kutoka kutoka kule kisiwa cha Songosongo kupitia kwenye bomba mpaka inakuja Ubungo kwenye ile mitambo ya Songas.

"Pia, tuna kitalu kingine cha Mnazibay ambacho kipo eneo la Msimbati kule Mtwara nacho kinazalisha gesi vile vile inachakatwa pale eneo la Madimba halafu vile vile nayo inasafirishwa kwenye bomba kuja Dar es Salaam kwenye eneo la Kinyerezi pale kwenye mitambo ya umeme.

"Bado tuna shughulin nyigine za utafutaji ambazo zinaendelea, upande wa uingizaji wa mafuta kama nilivyosema kuanzia mwaka 2021, TPDC ilirudi tena kwenye hiyo biashara ya kuingiza na kusambaza mafuta.

"Ikumbukwe kwamba miaka ya nyuma mpaka kufikia miaka ya 90, TPDC ndiyo ilikuwa mwingizaji pekee wa mafuta ghafi wakati ule mwanzoni, kwa ajili ya kuyachakata pale Kigamboni kwenye ile Refinery ya TIPA na baadae TPDC ndiyo ilikuwa inaendelea na usambazaji wa mafuta ya jumla, kuwauzia wengine.

"Kwa kipindi chote hiki, kulikuwa na mafanikio mengi ambayo tumeona umuhimu wa kuyaelezea kwenu kama wanahabari, lakini kwa umma wa Watanzania, kwa leo mafanikio yetu tumeyajumuisha katika maeneo sita tofauti ikiwemo eneo la uhakika wa upatikanaji wa nishati ya mafuta."

Gesi asilia

"Kwenye suala la hizi gesi kwenye magari na nyumbani hapa Dar es Salaam,sasa hivi tunajenga mradi ule wa kituo mama cha usambazaji gesi iliyoshindiliwa yaani Compressed Natural Gas (CNG), tunajenga katika eneo la Mlimani City, Ubungo pale.

"Kile kituo chenyewe kitakuwa kinafanya kazi mbili, cha kwanza kitakuwa kinashindilia gesi ili itiwe kwenye malori ambayo yatakuwa yanapeleka kwenye vituo dada ambavyo vitakuwa nje ya pale, lakini pia kitakuwa kinajaza magari palepale Mlimani City.

"Kwa sasa, vituo viwili ambavyo vitakuwa vinaanza na vinapokea kutokea pale kimoja kitakuwa Kibaha karibu na kiwanda cha madawa cha Kairuki na kingine kitakuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

"Kutakuwa na vituo vingine ambavyo vinajengwa na kampuni binafsi ambazo tumeingia nazo makubaliano, moja inaitwa TAQA Arabia wao wameshaanza ujenzi katika eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere.

"Na kituo kingine, nao watakijenga bababara ya Sam Nujoma kule kwa sasa, na kingine tunachokifanya kwa sasa ni kutengeneza mpango mkakati wa kuisambaza hii gesi kwenye mji nzima wa Dar es Salaam na pia kuitoa nje ya Dar es Salaam.

"Huu mpango tunautegemea katika miezi minne mpaka sita ijayo utakuwa tayari, tutatoa maelekezo yake na vile vile ndiyo utawawezesha sasa wale wawekezaji ambao wamechukua idhini kwetu kwenda kuwekeza kuweza kujua ni eneo lipi nzuri, soko lake limekaaje ili waweze kuwekeza kwenye maeneo yale.

"Nitolee mfano,katika ule mpango tulikuwa tunazungumza na taasisi nyingine ya Serikali ya manunuzi GPSA ya kujenga kituo cha kwao hapa Dar es Salaam, kingine Morogoro, kingine Dodoma ambapo sisi tutawapa kutokea kile kituo mama cha pale Mlimani City, halafu wao wataweza kujaza kwenye magari ya Serikali yatakayokuwa yamebadilishwa mfumo kwa ajili ya kutumia gesi asilia.

"Na hivyo hivyo, tutaangalia kuhakikisha kwamba kwenye barabara ya kuu zote za Dar es Salaam, kama mnavyojua barabara ya Morogoro, Bagamoyo, eneo la Kigamboni, barabara ya Kisarawe na barabara ya kuelekea Lingi (Kilwa Road) zote tuhakikishe kwamba kila kona ambayo inaingia katika jiji iwe imepata vituo vya kusambazia hii gesi, kwa hiyo, hiyo ndiyo mipango ya muda mfupi.

Mipango ya muda mrefu

"Lakini,mipango ya muda mrefu ni kuangalia namna ambavyo gesi hii itafika mpaka nje ya Dar es Salaam, kama nilivyosema tutaanza na njia kuu ya katikati kwa maana ya Morogoro mpaka Dodoma.

"Tutaangalia na njia nyingine hizo za Kaskazini, ya Kusini ambayo pia hiyo ina namna yake kwa sababu inapitiwa na lile bomba kuu, lakini na njia ya kuelekea Nyanda za Juu Kusini mikoa ya Iringa, Mbeya na Ruvuma."

Gesi ya nyumbani

"Gesi ya majumbani, tunaiangalia katika namna mbili, namna ya kwanza ni ujenzi wa njia ya mabomba, kama ambavyo baadhi ya wananchi watakuwa wameona, sasa hivi tunajenga bomba linatoka pale Mwenge na kuelekea Mbezi Beach, lile mwanzoni katika hatua ya awali wale wateja ambao tulikuwa tumeshazungumza nao kwanza kabla ya mradi ni hoteli takribani saba na viwanda vitatu.

"Wale watapokea mwnazoni, lakini baada ya pale tutaanza kuunganisha na wananchi na wakazi wa maeneo ambao lile bomba linafika, kwenye ule mpango wa kusambaza kwa kutumia gesi iliyogandamizwa CNG, pia tutaangalia namna ya kufikisha kwenye majumba pale ambapo nyumba nyingi zimekaa sehemu moja,

"Kwamba, unaweza ukafikisha ukajenga kituo kinachopokea halafu ukaweka bomba ndogo ambazo zina uwezo wa kusambaza kwenye nyumba japo kuwa ni gharama kubwa kuwekeza, lakini baadae mpango ambao ni rahisi kusambaza ni kuweka njia ya mabomba kwenye mji mzima."

Inawezekana kununua hisa?

"Nianze na suala la wazawa kumiliki hisa kwenye hizi kampuni (GASCO/Tanoil), ni kitu ambacho kipo, tunakifikiria na kipo kwenye mipango, lakini si sasa hivi, kwa maana gani, kwa maana unapotaka kuwaleta wananchi wanunue hisa ni vizuri ukalitengeneza lile shirika likaenda, likaonesha mwenendo wa faida kwa miaka kadhaa.

"Lakini mnapokuja mnasema, wananchi njooni sasa mnunue hisa kwa mfano GASCO wakisoma rekodi wasione wanapoteza fedha zao, wajue wanaenda kupata faida kutokana na uwekezaji wao.

"Kwa hiyo, ni changamoto ambayo tunayo na tutaifanyia kazi, pengine baada ya miaka kadhaa tutafikia hiyo hatua ya kwamba kampuni hii itamilikiwa asilimia fulani na TPDC na asilimia nyingine zitaenda kwa wananchi watakaojitokeza kununua hisa."

Kampuni tanzu kujisimamia

"Hizi kampuni hazijaanza muda mrefu kama ilivyoelezwa TANOIL ilianza mwaka 2021, japokuwa ilikuwa imesajiliwa miaka mingi, operesheni zilianza 2021 kwa hiyo huu ni mwaka wa pili tu.

"Na GASCO ilianza 2015, kwa hiyo kwa nature ya kazi za GASCO kwa mfano, mambo mengi wanajitegemea wenyewe.

"Kwa sababu, tunaimiliki kwa asilimia 100 kwa hiyo menejimenti yake inasimamiwa na Govern Board ambayo inahusisha watu kutoka nje na wachache kutoka ndani ya TPDC na Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC ndiyo ina mamlaka ya mwisho kwenye uendeshaji wake.

"Kwa hiyo, kiuendeshaji wanajitegemea kwa kiasi kikubwa,GASCO ndiye anayesimamia uendeshaji, matengenezo na marekebisho ya miundombinu yote ya usambazaji wa gesi kutoka kule Mtwara, ya kutoka Songosongo kuja Dar es Salaam.Na miundombinu ambayo tunaiendesha hapa Dar es Salaam."

Ushirikishwaji

Kuhusu, pendekezo lililotolewa na washiriki wa kikao kazi hicho kwamba TPDC iangalia namna ambavyo inawezza kushirikiana na SUMA JKT katika kufanikisha miundombinu ya usambazaji gasi asilia ndani na nje ya Jiji la Dar es Salaam, TPDC wamepokea pendekezo hilo.

"Tumelipokea pendekezo hilo, ni jambo nzuri na tutalifanyia kazi, lakini kama nilivyosema awali ni kwamba hiyo fursa ipo wazi kwa wawekezaji wote wa ndani na wa nje.

"Sisi mipango yetu ili kuweza kuwekeza kwenye maeneo ambayo hawa wawekezaji hawawezi kuwekeza, sisi tunataka kujielekeza kwenye kutafuta, kwenye kutengeneza na kuifikisha sasa katika maeneo ambayo wao wanaweza wakaitumia.

"Katika mpango wetu, tunajaribu kuigawanya Dar es Salaam kimkoa ili pale ambapo mwekezaji anapokuja tusikute tuna wawekezaji wawili katika eneo moja, mfano anajenga kituo Sinza na mwingi anakuja kujenga kituo hapo hapo wanagombania watumiaji hao hao.

"Kwa hiyo, tunatengeneza namna ya kui-zone ili wawekezaji wakija waweze kurejesha gharama zao na kupata faida,"amefafanua Mkurugenzi huyo.

Gesi ya Mitungi

"Hasa, sisi hatukuwa na operesheni kwenye eneo hilo, kwa sababu hiyo ni gesi mfano gesi yote unayoiona kama Taifa Gas na nyinginezo, zote hizo ni gesi ambazo zinatoka nje ya nchi.

"Kwenye uzalishaji wa mafuta,kwenye zile nchi ambazo zinazalisha mafuta wakishatoa mafuta huwa wanakutana na kiwango fulani cha gesi, hii ambayo unaiona kwenye mitungi (LPG) kwa maana ya Liquidified Petroleum Gas, sisi ya kwetu ambayo tunazalisha hapa nchini ni gesi asilia.

"Ndiyo maana Copress tunaita CNG kwa maana ya Compress Natural Gas ni gesi asilia na tunapoipeleka kuwa kimiminika inakuwa Liquidified Natural Gas, kwa hiyo focus yetu ilikuwa tuendeleze hususani gesi hii hii ambayo tunaitoa humu humu ndani.Tuache wengine waendelee huko, lakini, mipango na mikakati kwa ajili ya kuangalia namna ya uhifadhi ipo."

Uongozi wa Samia

Akizungumzia kuhusiana na jambo gani ambalo TPDC wanajivunia katika miaka miwili ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, Mkurugenzi huyo amesema, kuna mengi wanajivunia.

"Tunajivunia mengi, lakini ninaweza kufupisha kwa mambo mawili, la kwanza ni kwamba kiujumla wake, ninadhani mmeona wote, katika mazungumzo yake nadhani anapozungumzia mashirika ya umma na utendaji wake.

"Tunajivunia kwamba, anatoa dira na muongozo wa nini kama mashirika ya umma tufanye, mashirika ya umma unajua ni sehemu ya Serikali.

"Kwamba Serikali ilienda kutafuta gesi, ilienda kuendeleza na ilienda ikasambaza, lakini ukiweka hayo yote kwenye Wizara ya Nishati utawavuruga pale, kwa hiyo inachofanya Serikali ili kutimiza yale inayoyataka kwenye sekta fulani ndiyo inaunda shirika la umma na umiliki wake anakabidhiwa Msajili wa Hazina.

"Kwamba,yeye ndiye anayemiliki zile hisa kwa niaba ya Serikali, halafu sera na uongozi unatoka kwenye wizara ambayo inaongoza ile sekta, kwa hiyo kwa sisi (TPDC) ni Wizara ya Nishati.

"Sasa, shirika la umma kama limewekwa pale kufanya biashara maana yake linatakiwa lifanye biashara, litengeneze mifumo ya uendeshaji na uongozi wa ndani na vile inavyoshirikiana na wizara mama na wizara nyinginezo ili kufanya ile biashara.

"Kwa hiyo, tunachojivunia, ni kwamba ninachoweza kusema sasa hivi kuna dira na maelekezo ambayo yapo wazi ya kwamba wewe unatakiwa kufanya biashara, wewe unatakiwa kutoa huduma, kwa sababu yule ambaye anatakiwa kutoa huduma hawezi kujiendesha sawasawa na yule anayefanya biashara.

"Ninaweza kusema, kwamba watu wakiyaangalia mashirika ya umma kutokea nje huwa wanajijengea dhana kwamba, kwa sababu ni shirika la umma basi linaendaenda tu, likipata faida sawa, likipata hasara sawa, lakini ikumbukwe likipata hasara ile hasara inalipwa.

"Inalipwa na kina nani? Ile hasara inalipwa na wananchi, kwa sababu likipata hasara shirika la umma, lazima Hazina wawape fedha za kujiendesha, kwa hiyo ile dira na maelekezo ya namna ya kujiendesha na uhuru wa kujiendesha na mifumo ya kujiendesha ambayo imetolewa chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais inatuwezesha sisi kujua tuko wapi na tunapaswa kwenda wapi. Hilo la kwanza."

"La pili,ambalo lipo kwenye level yetu sisi kama TPDC, pale sasa unapotaka kujiendesha kama shirika la kibiashara, maana yake moja wapo ya kazi unazokuwa nazo ni kuweza kuvutia uwekezaji na mitaji.

"Kwenye sekta ya utafutaji wa mafuta na gesi, sekta ambayo inahitaji mtaji mkubwa, ndiyo maana kila mradia mbao tunataka kutekeleza tunatangaza tunatafuta wabia wa kuweza kushirikiana nao, niwape mfano hata vile visima ambavyo vipo nchi kavu, kwa mfano kule Mnazi Bay au Songosongo, kabla ya kuanza kuchimba kile kisima.

"Kwanza unafanya uchunguzi wa juu ya ardhi, kuangalia ile mitetemo ya ardhi inatoa alama gani kule chini kuna nini. ile yenyewe huwa ukifanya programu ndogo tu, kwa mfano programu tunayofanya sasa hivi ya kitalu cha Eyasi Wembere ni ya kilomita za mraba zaidi ya 10,000 kwenye kile kitalu.

"Lakini, inatugharimu bilioni 10 na zaidi kidogo, hapo unaangalia tu juu kwamba kuna kifaa unaweka juu unapiga mlipuko kidogo ili uweze kupata sauti za kutoka chini, ziweze kukujulisha kwamba kuna nini kule chini.

"Ukiona sasa, eneo hilo ndiyo unataka kwenda kuchimba kisima, unaita ile mashine ya kuchimbia kisima, kama ile ya kuchimbia maji ya kawaida, lakini sasa inakuwa kubwa zaidi kwa wastani kisima cha nchi kavu,kuanzia ukiki-plan mpaka ukimaliza kukichimba siyo chini ya dola za Marekani milioni 20.

"Kwa hiyo unazungumzia takribani bilioni 50 kwa kisima kimoja tu, na mara nyingi ili uweze kufanya programu nzuri inabidi uchimbe visima viwili au vitatu kwa wakati mmoja, kwa hiyo inabidi utekeleze programu ya bilioni 100 mpaka bilioni 150 kwenye uwekezaji.

"Sasa, kwenye kufanya hili, ili kuifanya TPDC yenyewe iweze kufanya pale uwekezaji si mkubwa sana na iweze kuvutia uwekezaji mwingine inabidi kuvuta mitaji, lile jambo la Serikali kuondoa mkopo lile bomba la Mtwara kuja Dar es Salaam na Serikali yenyewe kubeba lile jukumu la kulipa lilikuwa ni jambo muhimu sana, kubwa sana na limewezekana na kukamilika chini ya uongozi wa Rais Samia.

"Lakini, vile vile kupewa uwezo wa kushiriki kwenye hii miradi mingine mikubwa, mradi wa ECOAP ulianza na mazungumzo yake yalianza mapema zaidi, lakini yakakamilika na lile jukumu la kuwezeshw akuchukua zile asilimia 15 limetokea chini ya uongozi wake.

"Mazungumzo haya ya Mradi wa LNG, wengi mtakuwa mnafahamu yalianza toka mwaka 2006 yakakwama, yakaanza tena mwaka 2009 yakakwama, yaka kuanza tena mwishoni mwaka 2021 chini ya uongozi wake, na ndiyo sasa hivi tumefika mahali sasa kwamba yamekamilika, tunaingia kwenda kusaini na kutekeleza ule mradi."

"Kwa hiyo ni mambo mengi, lakini niseme hayo machache TPDC tunajivunia kwa kiasi kikubwa,"amefafanua kwa kina Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC.

Gesi mwendokasi

"Niseme kwamba, tulikuwa na changamoto kama taasisi mbili za Serikali kwa maana ya ule mradi kuanzia mwanzoni, tumekuja kushirikiana ikiwa tayari wenzetu wameshasaini mkataba wa kutumia mafuta, kwenye ile awamu ya kwanza, wakati sisi tulikuwa tunataka watumie gesi.

"Sasa, hiyo ndiyo changamoto ambayo ilitokea kwamba sehemu moja ya mradi imetangulia na sehemu nyingine imechelewa, kwa hiyo hatujaweza kubadilisha ile mifumo ambayo ipo.

"Lakini, nini ambacho tunakifanya, katika mazungumzo yetu wakati tunajadiliana nao, tulichokubaliana na tunaendelea kufanya kazi ni kuhakikisha kwamba awamu inayofuata, kama mnavyojua DART ni kwa awamu ninadhani.

"Kwamba, awamu zinazofuatia basi wakubali kurudi kutumia gesi na pale ambapo mikataba yao ya mafuta itakuwa imekamilika tunaweza kufanya utaratibu wa kubadilisha mifumo ya yale magari ambayo bado yapo yanatumia Diesel ili yarudi kwenye gesi.Lakini, jambo ambalo bado tunaendelea kulifanyia kazi."amesisitiza Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC.

TEF wanasemaje?

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatius Balile amesema kuwa, Tanzania haina budi kuharakisha upatikanaji wa nishati ya gesi hususani katika matumizi ya magari ili kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuongeza mapato kutokana na kuwepo kwa watumiaji wanaohitaji huduma hiyo.

“Asilimia 50 ya uchumi wa Tanzania sasa hivi unakwenda kupatikana kupitia TPDC, Tanzania sasa hivi inatumia sio chini ya trilioni 8 kuagiza mafuta ya dizel, petrol na mafuta ya taa.

"Tukitumia gesi tunaweza tukajikuta kwamba tunapunguza gharama za uagizaji wa mafuta angalau kwa trilioni 7, tunabaki kuagiza mafuta ya mitambo mizito na ya uendeshaji wa viwanda, kuna uwezekano wa nchi yetu sasa kuwa na kiwanda kikubwa cha kubadilisha magari ambayo yanatumia dizel na petrol kwenda kutumia gesi.

"Tutaweza kutengeneza ajira, lakini pia tutatengeneza soko la gesi yetu kwenda katika nchi zitakazokuwa zinabadilisha magari.”

Pia, amesema TPDC washirikiane na sekta binafsi katika kuharakisha utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia, na kuendelea kuongeza mtandao wa usambazaji wa gesi asilia kwa njia ya mabomba na gesi iliyoshindiliwa (CNG) kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya gesi asilia katika magari na kupunguza uagizaji wa mafuta ya magari kutoka nje ya nchi

Mipango mikakati

Akizungumzia kuhusiana na mipango mikakati ya shirika hilo, Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa TPDC,Derick Moshi amefafanua kuwa, wana mipango thabiti ambayo inalenga kulifanya shirika hilo kuwa la Kimataifa.

"Ni kweli hapa tumeelezea mpango mkakati wa miaka mitano, lakini tuna mpango mkakati wa miaka mitano, miaka 10 na miaka 25.

"Nafikiri kwamba, kama nilivyoelezea dhamira yetu ya kuwa kampuni ya Kimataifa ya nishati ikiwa ni kampuni ya umma, maana yake tuna dira tayari ambayo tumei-set ya kuwa kampuni ya nishati ya Kimataifa na vile vile tunapokuwa tunaenda mbele,tunakuwa tunajipima kila baada ya miaka mitano kwa kuangalia balance sheet yetu, kuangalia core business ilivyo na.

"Kwa kuangalia mazingira ya kwanza kwamba tumejitosheleza katika suala la nishati, halafu vile vile tunaangalia mazingira kwamba, tunavotanuka kwenda nje,mazingira ya balance sheet ikoje nafikiri kwa sasa hivi tuna balance sheet ya zaidi ya trilioni 4.2.

"Lakini tunaangalia kwamba, utakavyoendelea kukuwa maana yake una attracts asset zaidi na tunategemea balance sheet kuwa kubwa zaidi, na vile vile kuna kuwa na uwezo wa kukaa meza moja na makampuni makubwa zaidi, maana yake na sisi tutakuwa wakuba.

"Kwa hiyo, dira yetu ndiyo kama tulivyosema ina miaka mitano, miaka 10 na miaka 25 lakini ni kwamba tunaiweka miaka mitano ili kuweza kujipima ili hata mkija baada ya miaka mitano muweze kutuambia mlisema hiki, sasa mpo wapi."

Mradi wa LNG

Akizungumzia kuhusu mradi wa kusindika gesi asilia na kuwa kimiminika (LNG), Mkurugenzi wa Utafiti, Maendeleo na Uzalishaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),Kenneth Mutaonga amesema, huo ni mradi muhimu na Serikali inaupa uzito mkubwa.
.
"Huu mradi ni mradi mkubwa sana, ni mradi wa Kitaifa, kwa hiyo maandalizi ni ya Serikali kwa ujumla, labda nianze kwa upande wa TPDC kwanza.

"Kwa upande wa TPDC,ushiriki wetu katika huu mradi unaanza katika mazungumzo, TPDC imekuwa ikihusika katika huu mradi tangu mwanzo katika shughuli za kiutafiti, ambapo watu wetu wa mambo ya utafiti wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu sana na hawa wawekezaji, wakati shughuli za utafiti zikiendelea.

"Kwa hiyo kuanzia mwanzo mpaka tulipofikia leo, tumekuwa tukifanya kazi pamoja, kwa hiyo kujenga ujuzi wa ushiriki katika mradi ni shughuli endelevu.

"Kwa hiyo, tulianzia huko nyuma, tumekuwa tukifanya nao kazi kwa pamoja katika utafiti, kuchakata taarifa zilizokuwa zikitoka katika utafiti, wakati tulikuwa tunafanya drilling kule Mtwara na Lindi, timu zetu zilikuwa zinaenda.

"Kwa hiyo, wataalamu wetu wamekuwa wakifanya hizi kazi kwa pamoja, muda wote mpaka sasa, na siyo sisi tu ni muhimu kutambua kuwa, katika kusimamia huu mradi sisi TPDC tupo mbele kwa sababu ni jukumu letu, lakini tunafanya kazi kwa karibu sana na wenzetu wa PURA wenye dhamana ya kusimamia mkondo wa juu wa hii sekita katika huu mradi wa LNG.

"Ingawa kuna components mbili moja kule baharini na nyingine nchi kavu, kwa hiyo PURA wamekuwa wakishiriki tangu mapema katika shughuli za kuusimamia huu mradi tangu huko awali na pia wenzetu wa wizarani pia tumekuwa tukifanya nao kazi mpaka tulipofikia sasa."

"Kwa hiyo, sisi kama TPDC tumejipanga na kuna maeneo sita ambayo ni muhimu kwa sasa hususani kuhakikisha kwamba, tutakaposaini mikataba na hatua zitakazofuata mradi unatekelezwa kwa ufanisi.

"Mambo hayo sita ambayo TPDC tupo tayari na tumeshaandaa timu katika hayo maeneo la kwanza ni katika eneo la mkataba, ikumbukwe tu kwamba huu mradi, itasainiwa mikataba mama ambayo ndiyo msingi wa uendeshaji wa mradi huu."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news