DAR ES SALAAM-Ujumbe kutoka Kenya ukiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini wa nchi hiyo Elijah Mwangi umefika nchini kujifunza kuhusu namna bora ya usimamizi wa Sekta ya Madini ambapo Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali ameupokea ujumbe huo.
Mahimbali amesema Wizara ya Madini ina Taasisi tano ambazo ni Tume ya Madini, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Taasisi ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) pamoja na Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) ambazo hutekeleza majukumu yake kwa ushirikiano.
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Madini kutoka Kenya Elijah Mwangi ameipongeza Wizara ya Madini kwa usimamizi bora wa sekta hiyo na kumuomba Mahimbali kuendelea kushirikiana katika nyanja mbalimbali ikiwemo tafiti na usimamizi wa biashara ya madini.
Katika kikao hicho mada mbalimbali zimewasilishwa ambapo Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba amewasilisha mada juu ya madini yapatikanayo Tanzania na aina za tafiti zilizokwisha fanyika.
Dkt. Budeba amesema kwa sasa GST imejikita zaidi kwenye tafiti za madini ya kimkakati ambapo mpaka sasa Tanzania imefanyiwa tafiti za Kijiolojia kwa asilimia 96.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Ally Maganga amewasilisha mada juu ya shughuli za Tume ya Madini ikiwemo uwepo wa Masomo na Vituo vya Ununuzi wa Madini, Mfumo wa Leseni pamoja na shughuli za wachimbaji wadogo.
