NA LUSUNGU HELELA
WANANCHI wa Kata ya Malolo iliyopo Jimbo la Kibakwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa wamepaza sauti zao kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene wakimuomba asaidie kubadili mchakato wa kuwapata walengwa halisi wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) huku wakisisitiza kuwa utaratibu unaotumika kwa sasa umegubikwa na sintofahamu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiwa na wananchi wa Kijiji cha Nzugilo ambao wanakijiji wenzao waliwabaini kuwa wanastahili kuingizwa kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) lakini wameachwa.
Aidha, Wananchi hao wamewataka walengwa wa Mpango huo ambao tayari wameimarika kiuchumi kuwa na utu kwa kujiondoa na kuwapisha wengine wanaostahili kuingizwa kwenye Mpango.
Hayo yamesemwa na Wananchi mbalimbali kwa nyakati tofauti kupitia mikutano ya hadhara ya Waziri huyo anayoendelea kuifanya katika Vijiji vya Jimbo la Kibakwe ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambapo wananchi hao wameomba ubainishaji huo wa walengwa ufanyike kwa uwazi ikiwezekano kupitia mikutano ya hadhara ili waweze kuwapata walengwa halisi.
Wamesema kuwa mchakato huo katika ngazi za vijiji haufanyiki vizuri hivyo kupelekea wale ambao sio maskini halisi kuwa wanufaika ilhali wale maskini halisi wakiendelea kutaabika.
Malalamiko hayo ya wananchi yalitokana na maswali ya Mhe. Simbachawene ya kutaka kuwatambua walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Kata hiyo ya Malolo na namna walivyopatikana ili kujiridhisha na minongóno aliyoisikia juu ya upatikanaji wa walengwa hao.
Akijibu malalamiko hayo, Waziri Simbachawene amesema tayari ameshatoa maelekezo kwa Menejimenti ya TASAF Makao Makuu kuangalia namna bora ya kuwapata walengwa halisi wa Mpango.
Ameongeza kuwa TASAF msingi wake ni mpango shirikishi wa kuondoa umasikini uliokithiri kwa wananchi, hivyo ni lazima kutafuta njia sahihi ili kutimiza azma ya kuanzishwa kwake.
Tags
Habari
Jimbo la Kibakwe
Jimboni Leo
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)
Ruzuku TASAF
TASAF
TASAF Tanzania