NA FRESHA KINASA
KIONGOZI wa mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa kwa mwaka 2023, Abdallah Shaibu Kaim ametoa pongezi kwa Mbunge wa Jimbo la Butiama ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Jumanne Sagini,watendaji wa halmashauri hiyo na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mheshimiwa Mosses Kaegele kwa usimamizi wao madhubuti na kuhakikisha miradi ya maendeleo wilayani humo imetekelezeka kwa ubora na kwa viwango vinavyostahili kwa manufaa ya wananchi.
Akizungumza Julai 5, 2023 baada ya kukagua miradi sita ya Maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.7,Kaim amekiri kuwa miradi yote iliyofikiwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru ambayo ni ya Barabara, Elimu, Vikundi vya Ujasiriamali, Afya, Maji na Nyumba ya kulala wageni yote ina ubora unaotakiwa.
Aidha, Julai 6, 2023 wakati mwenge huo ukikabidhiwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kiongozi huyo wa mbio za mwenge amesema;
"Tumejiridhisha na miradi yote ambayo imefikiwa katika Wilaya ya Butiama, hivyo sina budi kumpongeza Mbunge wa Jimbo la Butiama, Jumanne Sagini ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kufuatilia miradi hiyo kwa umakini mkubwa kwa manufaa ya wananchi,"amesema na kuongeza kuwa.
"Nampongeza pia Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mheshimiwa Moses Kaegele, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Mhe.Peter Wanzagi, Mkurugenzi, Bi. Aziza Baruti, Chifu Japhet Wanzagi na wengine mlioshiriki kwa namna moja au nyingine kuhakikisha miradi hii inakuwa na ubora unaotakiwa,"alisema Kaim.
Kwa upande Wake Mbunge wa Jimbo la Butiama mkoani Mara ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Jumanne Sagini, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inagusa maisha ya wananchi wa Butiama na Mkoa wa Mara kwa ujumla.
Pia, Mheshimiwa Sagini amewashukuru Viongozi wa Halmashauri ya Butiama kwa ushirikiano wao wa dhati katika kuhakikisha wanawatumikia wananchi kuwaletea maendeleo.
Sagini amesisitiza Watanzania kuendelea kuiunga mkono Serikali kwa dhati kwani imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo ambayo inatija katika nyanja mbalimbali na kwamba Serikali ya Awamu ya sita imehakikisha inawagusa Wananchi kwa kuwaletea maendeleo Jambo ambalo linapaswa kupongezwa na kila mwananchi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mhe.Moses Kaegele ameeleza kuwa ,katika Mkesha wa Mwenge wa Uhuru uliofanyika katika Uwanja wa Mwenge Butiama jumla ya watu 355 walifanikiwa kupimwa maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) wanawake wakiwa 99 na wanaume 256 ambapo waliokutwa na maambukizi ni watu watatu, wanaume wakiwa wawili na mwanamke mmoja.
Mwenge wa Uhuru ulifika nyumbani kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere na kuwasha Mwenge wa asili wa Mwitongo pia viongozi hao walitumia fursa hiyo kuzuru kaburi la Mwalimu Nyerere na kuweka mashada ya maua na kuwasha mishumaa.
Kauli mbiu ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 inasema “Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe hai na Uchumi wa Taifa.”
Hata hivyo, Mwenge wa Uhuru tayari umekabidhiwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa ajili ya kuendelea na mbio zake mkoani Mara.