DODOMA-Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kwa kupata Hati safi za Ukaguzi kwa Hesabu zilizoishia Juni 30, 2022 kwa miaka sita mfululizo tangu mwaka wa Fedha 2016/2017 hadi 2021/2022.
RC Senyamule amesema, kitendo hicho kimeipa heshima kubwa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Mkoa wa Dodoma na nchi kwa ujumla.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akitetea jambo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Mhe. White Zuberi Mwanzalila katika kikao cha Baraza la Madiwani kikao kilichojadili hoja za ukaguzi kwa Wilaya ya Kongwa mwishoni mwa wiki na kufanyika katika ukumbi wa VETA Kongwa.
Senyamule ameyasema hayo wakati wa Mkutano wa Baraza Maalumu la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kujadili Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2022/23.
Amesema, Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa ina jumla ya hoja 54 ambapo katika hoja hizo 39 ni za miaka ya nyuma na hoja 15 ni hoja za mwaka wa ukaguzi 2021/2022, ambapo kati ya hoja 54 hoja 16 zimeshafungwa hivyo kubakiwa na hoja 38.
Kufuatia hoja 38 zilizosalia, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Dkt. Omary Nkullo kuwasilisha kwake Mkakati wa ujibuji wa hoja hizo ifikapo Julai 30,2023.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt. Omary Nkullo akizingumza katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichojadili hoja za ukaguzi kwa Wilaya ya Kongwa. Wengine katika picha ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mhe. White Zuberi Mwanzalila na Makamu Mwenyekiti Mhe Richard Mwite.
Amesema, uwepo kwa hoja nyingi za Ukaguzi kila mwaka, ni kutokana na kuwepo kwa udhaifu mkubwa wa mifumo ya udhibiti wa ndani katika Halmashauri unaosababisha baadhi ya shughuli za Halmashauri kutekelezwa pasipo kuzingatia ipasavyo Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali iliyopo katika uendeshaji wake jambo ambalo huibua hoja zisizokuwa na lazima.
“Mkurugenzi hapa niagize watumishi wote waliochukua masurufu na hawajafanya marejesho kwa wakati warejeshe fedha hizo mapema iwezekanavyo,” Senyamule ameagiza.
Senyamule pia amesisitiza agenda endelevu ya mazingira na kuwataka wana Kongwa kuendelea kukijanisha Dodoma, kuhamisha elimu kwa kukemea utoro kwa wanafunzi mashuleni pia kutoa msukumo wa agenda ya kilimo.
Mwenyekiti wa Halmashauri Wilaya ya Kongwa Mhe. White Zuberi Mwanzalila akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani kikao kilichojadili hoja za ukaguzi kwa Wilaya ya Chamwino. Wengine katika picha ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule (kushoto) na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt. Omary Nkullo.
“Anzeni kuandaa vitalu vya miche ya miti katika maeneo yenu ili maelekezo ya Serikali ya kupatanda miti milioni moja na laki tano kwa kila Halmashauri yaweze kutimia. Pia, mkadhibiti utoro katika shule zetu, Serikali inajenga miundombinu hii ya shule kwa gharama kubwa hivyo tuna wajibu wa kuhakikisha watoto wanakwenda shule,” Senyamule amesisitiza.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Bw. Ally Gugu ametoa rai kwa watumishi wote kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni za utumishi wa umma ili kuepuka hoja za ukaguzi ambazo zinaweza kuepukika.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema amesema Wilaya yake imekamilisha kwa wakati ujenzi wa madarasa kupitia mradi wa boost ambapo wilaya ilipokea kiasi cha Shilingi Bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa Shule 2, Vyumba vya madarasa 26, madarasa ya awali 2, darasa la elimu maalumu 1 na matundu 18 ya vyoo.