NA GODFREY NNKO
NAIBU Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo,Mheshimiwa Hamis Mwinjuma amesema, lugha ya Kiswahili inapawa kupewa hadhi na ukubwa wake na mahali bora zaidi pa kuanzia ni Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ambao wanafanya kazi ya kutoa mwelekeo wa lugha na mambo mbalimbali kwa kusoma, kutazama na kusikiliza.
Mheshimiwa Mwinjuma amesema hayo Julai 4, 2023 katika Kongamano la Wahariri lililoandaliwa na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) ambalo liliangazia juu ya nafasi ya wahariri katika kusimamia matumizi ya Kiswahili sanifu kwenye vyombo vya habari nchini.
Kupitia kongamano hilo, mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdullah ambapo limefanyikia Ukumbi wa Sheikh Idris Abdul Wakil uliopo Kikwajuni jijini Zanzibar.
Aidha, kongamano hilo ni maandalizi ya kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani ambayo yatafanyika Julai 7, 2023 huku kauli mbiu ikiwa ni “Kiswahili Chetu; Umoja Wetu”.
"Mimi huwa na sababu mbili wakati wote ambazo zinanipa msisimko kuelekea mambo mbalimbali, kila tukio ninakuwa na sababu mbili, sababu kubwa na sababu ndogo.
"Sababu kubwa, kwenye tukio hili (kongamano na wahariri) ni kukipa hadhi na ukubwa wake Kiswahili, na hakuna mahali bora zaidi hilo linaweza kuanza kama kwenye Jukwaa la Wahariri, kwa sababu.
"Wahariri ndiyo wanafanya kazi kubwa ya kutupa uelekeo wa wapi lugha inatakiwa kuelekea kama ambavyo,wanatupa uelekeo wa mambo mengine mbalimbali ambapo sisi huwasoma, huwasikiliza na kupata njia ambayo tunatakiwa kupita.
"Sasa sababu yangu ndogo kwenye tukio hili la leo,ni hamu yangu ya kukaa kwenye hili tukio lote ambalo litachukua saa kadhaa,bila kusikia neno la Kiingereza hata moja.
"Mimi, ninatoka Tanga na sikuwahi kuamini, kwanza ninaamini kwamba kama Mkuu wa Mkoa wa Magharibi anavyoamini Kiswahili ni cha Mjini Magharibi (chimbuko), mimi ninaamini Kiswahili kizuri zaidi kinachotakiwa kutumika ni cha Ki-Tanga.
"Hilo ni moja, na nilikuwa ninaamini ninajua Kiswahili sana, mimi ni mpenzi wa lugha ya Kiswahili, na ushaidi upo katika kazi ambayo nilikuwa ninaifanya (muziki) kabla ya kuangukia huku kwenye siasa.
"Nilikuwa ninaamini kwamba, ninafahamu sana Kiswahili,lakini jinsi Kiswahili kilivyopiga hatua kikafika maeneo mbalimbali, sikuwa ninaamini kwamba ninaweza kufundishwa Kiswahili na mama wa Kichaga (Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Bi. Consolata Mushi ).
"Ipo siku moja alikuwa ananipitisha kwenye jambo fulani mahususi hivi, na tukatumia kama saa mbili, na mimi vile vile sababu kubwa ilikuwa ni lile jambo lenyewe, lakini sababu ndogo nilitaka kujihakikishia kama huyu mama atatumia muda wote bila kusema neno la Kiingereza?.
"Yaani nimesikiliza, nimefungua macho yangu yote mpaka ndani ya kichwa sijasikia neno la Kiingereza kwa saa mbili, kwa hiyo kila wakati huwa ninampa maua yake, kwamba mama kwenu hakuna bahari, Kiswahili hakikuingia kule Uchagani, lakini bado tuna mambo ya kujifunza hata kutoka kwenu.
"Tukio hili, linafanyika lipo na limeanzishwa na sababu ya Mkutano wa 41 wa UNESCO ambao ulifanyika mwezi wa 11 mwaka 2021 ambao uliitaja tarehe saba mwezi wa saba ya kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani kote.
"Sasa, sisi ndiyo Waswahili wenyewe, sisi ndio wenye Kiswahili chetu, na UNESCO pamoja na kwamba hawaishii tu kuitaja tarehe saba na matukio mengi yanayozunguka siku hiyo, lakini sisi kama Waswahili tuna jukumu la kulibeba la kulishika moja kwa moja kuliweka kwenye ungo.
"Bibi yangu alikuwa anasema aidha unaweka kwenye kapu ama kwenye ungo, kwenye kapu unakuwa umelificha kwenye ungo watu wote walione, sasa sisi tuna jukumu la kuibeba tarehe saba mwezi wa saba ya kila mwaka kwenye ungo ili kuhakikisha Dunia nzima inaona.
"Nimevutiwa na dada kutoka Urusi ambaye amejifunza Kiswahili nchini Urusi, lakini ninaamini miongoni mwa sababu zilizomfanya awepo leo Zanzibar ni hiki Kiswahili, kwa hiyo tuna uwezekano wa kutengeneza mpaka utalii wa Kiswahili.
"Lengo letu kubwa ni kukibidhaisha Kiswahili sasa, kuna kazi nyingi, kuna fursa nyingi ambazo pamoja na kazi nyingi ambazo wahariri wetu wanazifanya zinaweza kupatikana kupitia Kiswahili kama ukalimani, tafsri na kadhalika.
"Kwa hivyo, niwaombe ndugu wahariri, pamoja na mambo yatakayojadiliwa leo, lakini nyuma ya vichwa vyenu muwe mnaweka namna ambavyo mnaweza kutumia fursa nyingi ambazo zinaweza kupatikana kwenye Kiswahili kwa ajili ya kukiendeleza.
"Hii itasaidia si tu ninyi binafsi,lakini nchi kwa ujumla, na ile dhana ya kwamba sisi ndiyo wenye Kiswahili hasa inatakiwa kuendelea kubaki.
"Na Serikali zetu mbili hizi, Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinafanya mambo mengi miongoni mwa mambo haya ni haya ya kwenye Utamaduni na haya ya Kiswahili na kuhakikisha kwamba Kiswahili kinakuwa miongoni mwa nembo za taifa kama ambavyo inatakiwa kuwa.
"Nina hamu ya kuona na kusikia yote ambayo yatajadiliwa na kuwasikia wahariri wetu maazimio ambayo watayafikia ili kuhakikisha Kiswahili kinapata hadhi na sifa inayostahili,"amefafanua kuwa kina Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo,Mheshimiwa Hamis Mwinjuma.
Novemba, 2021 Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lilipitisha Julai 7 ya kila mwaka kuwa siku ya kuadhimisha lugha ya Kiswahili kote duniani.
Uamuzi huo ulifikiwa kupitia mkutano wake wa nchi wanachama ambao ulifanyika makao makuu ya UNESCO jijini Paris, Ufaransa hivyo kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha pekee kutoka Bara la Afrika kupewa siku yake maalum ya utambulisho na kuadhimishwa duniani.