Lusinde afunguka kuhusu uwekezaji bandarini

NA MATHIAS CANAL

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Mheshimiwa Livingstone Lusinde ameitaka Serikali kuyafanyia kazi maoni yaliyotolewa na Watanzania wenye nia njema kuhusu uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salam.

Lusinde amebainisha hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bariadi lililofanyika Julai 14, 2023 katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Alliance.

Amesema kuwa, maoni hayo yanatosha na ni wakati sasa wa serikali kuyafanyia kazi badala yake iachane na mambo mengine ikiwemo kutoa elimu.

"Maoni yametolewa mengi ya viongozi wa dini, ya wanasheria, ya wasomi, serikali iyachukue na kuendelea kufanya kazi ilizojipangia.

"Hivi kama kwenye mpira wa mguu kusingekuwa na refa wa kuamua magoli mpira ungechezwaje, yaani kungekuwa na watu ukifunga goli waanze kujadiliana lile goli ama sio goli,"alibainisha.

Amesema, Serikali imeshasikia maoni hivyo ni wakati wa kuyachuja na yenye nia njema yafanyiwe kazi na kufunga ajenda hiyo ili kuendelee na kazi.

Naye Mbunge wa Viti Maalum Zanzibar, Mheshimiwa Tauhida Cassian Galoss amewataka Watanzania kuhakikisha kuwa hawakubali wala kuthubutu kukubali kutikiswa kwa Muungano wa Tanzania.

"Watanzania kutoka Kigoma mpaka Zanzibar ni wamoja, hivyo hawapaswi kugombanishwa wala kutenganishwa na mtu yeyote,"amesisitiza Mheshimiwa Tauhida.

Amesema kuwa, umoja na mshikamano wa Tanzania unasababisha watu wengine kuona wivu na choyo.

Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Jimbo la Bariadi mkoani Simiyu,Mheshimiwa Kundo Mathew amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mabalozi wazuri wa maendeleo yanayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo mgeni rasmi ambaye ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (NEC), Mheshimiwa Livingstone Lusinde (Mb).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news