ANKARA-Kocha Mkuu, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema amefurahi kiwango kilichooneshwa na wachezaji wa Klabu ya Simba licha ya kupoteza kwa bao moja dhidi ya Turan PFK katika mchezo wa kirafiki uliopigwa Uwanja wa Soğuksu Spor Kompleksi.
Turan walipata bao hilo kwa kichwa mapema dakika ya nne kupitia kwa Rodarik Miller baada ya kuunganisha mpira wa kona.
Baada ya bao hilo, Simba SC waliendelea kushambuliana kwa zamu huku wakifika zaidi langoni kwao ingawa hawakuweza kutumia nafasi walizopata.
Kipindi cha pili walirudi kwa kasi na kufanya jitihada za kutafuta bao la kusawazisha dakika za mapema ili kuwarudisha mchezoni, lakini haikuwezekana.
Dakika ya 60 kiungo mshambuliaji, Willy Essomba Onana alipoteza nafasi ya kutupia bao la kusawazisha baada ya kubaki na mlinda mlango Tamal akashindwa kutumbukiza mpira wavuni.
Kocha Mkuu, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ alifanya mabadiliko ya kuwatoa Sadio Kanoute, Clatous Chama, Onana na kuwaingiza Fabrice Ngoma, John Bocco na Jean Baleke. Robertinho amesema, walicheza vizuri kuanzia kwenye kushambulia, kuzuia pamoja na kumiliki mchezo kwa muda mrefu.
Robertinho ameongeza kuwa, ubora wa kikosi walionao sasa anaamini watafanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na mashindano ya ndani msimu ujao.
“Kwangu siangalii matokeo ya mwisho bali mchezo wenyewe ulivyokuwa. Tumecheza vizuri kuanzia mwanzo hadi mwisho.
“Wachezaji wameonekana wapo timamu kimwili, kimbinu na hilo ni jambo ambalo limenifurahisha. Nawapongeza pia wasaidizi wangu wamefanya kazi kubwa kwa muda mfupi,” amesema Robertinho.