Mahakama yakataa ombi la Serikali kupiga marufuku wimbo wa maandamano Glory to Hong Kong

HONG KONG-Mahakama ya Hong Kong imetupilia mbali ombi la Serikali la kupiga marufuku kuuondoa katika mtandao wimbo usio rasmi wa vuguvugu la kuunga mkono demokrasia kisiwani humo, wimbo huo ulianza kuvuma wakati wa machafuko dhidi ya Serikali mwaka 2019.
Waandamanaji wakiimba nyimbo, ikiwa ni pamoja na Glory to Hong Kong, wakati wa maandamano ya 2019 kwenye jumba la maduka la IFC huko Hong Kong. (Picha na NYTIMES).

Katika kuzuia zabuni ya kusitishwa, Mahakama Kuu mnamo Ijumaa ilisema uchapishaji na usambazaji wa Glory to Hong Kong tayari ulikuwa na adhabu kwa mujibu wa sheria zilizopo, na kuongeza marufuku huenda isilazimishe kampuni kubwa ya utafutaji wa mtandao wa Google na makampuni mengine ya teknolojia kufuta wimbo huo.

Mtendaji Mkuu, John Lee Ka-chiu alisema ameiomba Idara ya Haki kuchunguza hukumu hiyo na kuzingatia hatua za kufuatilia haraka iwezekanavyo.

Aidha, Jaji Anthony Chan aliamua kwamba kutoa marufuku hiyo kunaweza kuwa na athari za kusikitisha katika uhuru wa kujieleza.

Vyombo mbalimbali vya habari vya Kimataifa vimeeleza kuwa,wenye mamlaka wamekasirishwa kwa kusikia Glory to Hong Kong ikichezwa badala ya wimbo wa taifa wa China wakati wa matukio ya michezo ya kimataifa.

Hong Kong ni sehemu ya Serikali ya Watu wa China, lakini imekuwa na uhuru wa kujitawala tangu mwisho wa utawala wa Uingereza mwaka 1997. Wanaharakati wanasema kuwa, uhuru wa kidemokrasia umeminywa hatua kwa hatua tangu wakati huo.

Pia, wanasema majaribio ya kuupiga marufuku wimbo huo ni ishara nyingine ya Beijing kukandamiza upinzani dhidi ya Serikali ya China.

Aidha, inadaiwa mamlaka imejaribu kufuta au kuficha alama zote za wimbo huo mtandaoni kwa miezi kadhaa na Glory to Hong Kong pia imepigwa marufuku shuleni tangu 2020.

Serikali ya Hong Kong pia imetoa ombi kwa Google kuondoa wimbo huo au kuorodheshwa chini katika matokeo ya utafutaji, ombi ambalo inadiwa kampuni hiyo imekataa mara kwa mara.

Waziri wa Sheria, Paul Lam Ting-kwok aliomba mnamo Juni kwamba mahakama itoe amri ya muda ya kupiga marufuku wimbo huo kukuzwa, kusambazwa, au kuimbwa kwa nia ya kuwachochea wengine kujitenga au kwa nia ya uchochezi.

Lakini katika uamuzi wake, jaji alinukuliwa akisema,"Ninaamini kwamba kuingilia uhuru wa kujieleza hapa, hasa kwa watu wa tatu wasio na hatia, ndiko kunakotajwa katika sheria za umma kama athari mbaya,"alieleza Jaji ingawa bado wengi hawakuweza kupata jibu sahihi kuhusu alimaanisha nini anavyosema watu wasio na hatia.

Wimbo huo ambao ulivuma zaidi mwaka 2019 wakati wa maandamano umebeba maneno, "Mapinduzi ya nyakati zetu. Watu watawale, wenye kiburi na huru, sasa na milele. Utukufu uwe kwako Hong Kong."

Hata hivyo, katika kujibu maandamano hayo, China iliweka sheria kali ya usalama wa taifa ili kurejesha utulivu katika jiji hilo. Wakosoaji walisema, sheria hiyo ilibuniwa kukandamiza upinzani na kupunguza uhuru wa Hong Kong.

Mwaka jana, mchezaji wa harmonica alikamatwa kwa kucheza wimbo huo nje ya ubalozi mdogo wa Uingereza huko Hong Kong kuomboleza kifo cha Malkia Elizabeth II. (BBC/Mashirika)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news