Mwaka mmoja wa mradi wa kuzuia kuzama kome,Busekera wavuvi wabadili tabia

NA FRESHA KINASA

MRATIBU wa Shirika la EMEDO Mkoa wa Mara linalojishughulisha na mazingira, Majura Maingu amewataka wavuvi katika Halmashauri ya Musoma mkoani Mara kuendelea kutekeleza majukumu yao ya uvuvi kwa kuzingatia usalama majini. 
Shirika la EMEDO lilianza kutekeleza mradi mwaka 2022 ujulikanao kwa jina la 'Kuzuia kuzama majini Ziwa Victoria' Katika Wilaya ya Musoma limejikita kutoa elimu ya usalama kwa wavuvi ili kuhakikisha kwamba hata ikitokea ajali majini wanaokolewa wasipoteze maisha kwani ni rasilimali muhimu katika kuujenga uchumi wao na uchumi wa nchi kwa ujumla. 

Maingu ameyasema hayo Julai 25, 2023 katika maadhimisho ya siku ya kuzuia kuzama maji duniani iliyofanyika katika Kijiji cha Kome Kata ya Bwasi Wilaya ya Musoma ambapo imewakutanisha wavuvi kutoka Kata ya Bwasi na Bukumi, viongozi wa Serikali, viongozi wa BMU na wananchi kwa ujumla. 
Huku, kauli mbiu ya mwaka huu ikisema 'Mtu yeyote anaweza kufa kwa kuzama, hakuna anayepaswa kufa kwa kuzama.'

Maingu amesema kuwa, kuzingatia usalama majini ni jambo muhimu sana katika kulinda maisha yao na hivyo amewasisitiza wavuvi hao kuendelea kuvaa maboya (life jacket) wakati wote. 

Pia amewasihi kuendelea kutumia mitumbwi imara sambamba na kuzingatia utabiri wa hali ya hewa unaotolewa na Serikali ili wawe salama wanapotekeleza majukumu yao. 

Kwa upande wake Afisa Uvuvi Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, Augustino Costabtine amesema kuwa, kwa asilimia kubwa mapato ya halmashauri hiyo yanatokana na uvuvi. Hivyo elimu wanayopewa na Shirika la EMEDO ni muhimu katika kuongeza ufanisi na tija. 

Ameongeza kuwa, kwa kutambua jambo hilo Serikali na wadau mbalimbali wameendelea kuweka mazingira rafiki kwa wavuvi kusudi watekeleze kazi hiyo kwa ufanisi unaotakiwa.

"Serikali inakusanya mapato kutokana na uvuvi, lakini pia wavuvi wanapata kipato kuendesha maisha yao na kufanya maendeleo. 
"Hivyo lazima niwaombe kuzingatia usalama wenu iwapo mvuvi akizama athari ni kubwa muda mwingi hutumika kumtafuta, lakini pia huacha watu ambao wanamtegemea na hivyo nguvu kazi ya taifa kupotea."amesema Costantine. 

Kwa upande wake Fabian Bwire mvuvi katika Mwalo wa Kome Kata ya Bwasi amelishukuru Shirika la EMEDO kwa kuwapa elimu ya usalama wavuvi kwani hatua hiyo imeendelea kuwafanya wavuvi kuwa salama na kuchukua tahadhari kunapokuwa na hali mbaya ya hewa kuokoa maisha yao. 

Veronica Paulo ambaye pia ni Mvuvi katika Mwalo wa Busekera uliopo Kata ya Bukumi amesema, kutolewa kwa elimu ya usalama majini kwa kiwango kikubwa imewapa wavuvi kujiamini na kuwa na uwezo wa kuepuka kuzama ingawa bado amesema baadhi ya wavuvi bado hawazingatii uvaaji wa maboya hivyo amehimiza elimu izidi kutolewa zaidi kwao. 

Paul Patrick mbali na kulipongeza Shirika la EMEDO kwa kufanya kazi nzuri, pia ameliomba kuendelea kutoa elimu hiyo kusudi iweze kuwafikia wavuvi wengi wa Mkoa wa Mara.

Kuhusu WDPD

Aprili 2021,Umoja wa Mataifa ulipitisha Julai 25 ya kila mwaka kuwa Siku ya Kuzuia Kuzama Maji Duniani (World Drowning Prevention Day) inayolenga kuangazia athari za ajali hizo na kuweka mikakati ya kuzizuia

Uamuzi huo ulifikiwa, ikiwa kuzama kunatajwa kuwa tatizo kubwa la afya ya umma duniani, na inakadiriwa watu wapatao 236,000 huzama kila mwaka. 

Vile vile inaelezwa kuwa,nchi za uchumi wa chini na kati huchangia zaidi ya asilimia 90 ya vifo vya kuzama majini bila kukusudia.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, kuzama majini ni miongoni mwa sababu kuu za vifo kwa watoto na vijana wenye umri kati ya mwaka mmoja hadi 24.

Aidha, ili kukabiliana na ajali za kuzama majini katika jamii, inashauriwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuweka vizuizi katika maeneo ya maji ili kuepusha watoto kuyafikia pasipo uangalizi maalum na kuzuia vifo vinavyoweza kuepukika

Sambamba na kuhimiza mafunzo ya kuogelea,usalama wa majini na uokoaji ambayo yanatajwa kuokoa maisha ya makundi mbalimbali ya watu duniani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news