Mashamba ya mirungi, bangi na mali zilizopatikana kutaifishwa

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama imeendesha operesheni maalumu ya kutokomeza dawa za kulevya aina ya mirungi wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro ambapo wameteketeza hekari 535 kwa muda wa siku nane.
Hayo yamebainishwa Julai 9, 2023 na Kamishna Jenerali wa DCEA,Aretas Lyimo ambaye pia ameelekeza pongezi nyingi kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa ushirikiano mkubwa ambao wanaupata kufanikisha operesheni hiyo. 

Pia amefafanua kuwa, kuanzia sasa mashamba na mali zilizopatikana kupitia kilimo cha bangi na mirungi zitataifishwa ikiwa ni utekelezaji wa sheria.

Sheria

"Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imeimarishwa na sasa hivi yeyote ambaye anakamatwa na mirungi au dawa zozote za kulevya kifungo chake cha juu ni miaka 30 au kifungo cha maisha.
"Kwa hiyo, tuwaombe wananchi waanchane na biashara ya dawa za kulevya nchini, kwa sababu tukianza kukamata watu wote, watu wote wataishia magerezani, utakamata baba, utakamata mama, familia itabaki yatima, kwa hiyo wazazi wahakikishe kwamba wanawakataza watoto wao kuendelea na kilimo cha bangi na mirungi katika maeneo yao.

"Tuwaombe sasa wananchi wote,kulingana na adhabu zilizowekwa, miaka 30 au kifungo cha maisha jela ni adhabu kubwa, kwa hiyo tuhakikishe kwamba watu wanaacha na lengo la kuweka hizi adhabu ni kuhakikisha kwamba tunatokomeza dawa za kulevya chini.

"Hivyo,jamii yote kwa ujumla,viongozi wa dini, viongozi wa kimila, viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, kata, wilaya na mikoa tushirikiane wote kutokomeza biashara ya dawa za kulevya katika maeneo yetu.

"Na, Tanzania inawezekana kuwa salama kwa kutokuwa na dawa za kulevya, sheria pia inatutaka tukishakamata shamba lililolima dawa za kulevya,tunataifishwa shamba hilo.
"Kwa hiyo tuiombe jamii, tukianza kutaifisha mashamba yao watakosa hata maeneo ya kulima, kwa hiyo kuanzia sasa hivi tutaanza kutekeleza hiyo sheria,kwamba tukikuta shamba lako limelima bangi, limelima mirungi tunalitaifisha hilo shamba, lakini pia mali yote iliyopatikana kutokana na kilimo hicho cha mirungi au bangi pia na zenyewe zinataifishwa.

"Kwa hiyo tutaanza kusimamia hiyo sheria, kwa hiyo tuwaombe wananchi wote wasije wakaingia kwenye wimbi la umaskini, waachane kabisa na biashara ya dawa za kulevya, waache kabisa kulima bangi, waache kabisa kulima mirungi vinginevyo mali zao zitataifishwa,"amefafanua Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.

Same

Aidha, Kamisha Jenerali Aretas Lyimo amesema, kupitia operesheni hiyo ambayo wameiendesha Kata ya Tae kwenye vijiji vya Tae,Likweni na Ekondi wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro imeonesha mafanikio makubwa.

"Mirungi ni mojawapo ya dawa za kulevya zilizokatazwa nchini, kutokana na kwamba mirungi ina athari nyingi kwa binadamu, inaathari kiuchumi, inaathari kisiasa, inaathari pia kijamii na kiafya pia.
"Kwa sababu, mirungi inasababisha kansa ya koo, kansa ya tumbo, inasababisha uraibu, inasababisha mtindio wa ubongo, lakini pia kiuchumi inasababisha nchi kukosa mapato, kwa sababu wote wanaolima mirungi katika kata hii na katika eneo hili la Same, hawaiingizii mapato yoyote Serikali.

"Lakini, pia tunahakikisha kwamba, kwenye mikataba ya Kimataifa ambapo tumeingia mikata mitatu ya Kimataifa 1961, 1971 na 1986 inatutaka pia nchi yoyote ile ambayo imeingia ile mikataba ihakikishe inafanya operesheni katika maeneo yake yote ili kuhakikisha inatokomeza kabisa suala la dawa za kulevya katika nchi husika.

"Lakini pia, lazima ioneshe juhudi inazozifanya katika kutokomeza dawa za kulevya kwa kwa wananchi na jamii, lakini pia na Dunia iweze kujua kwamba, kazi inayofanywa na nchi husika katika kutokomeza dawa za kulevya.

"Kwa hiyo, tuko katika wilaya hii ya Same, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola likiwemo Jeshi la Polisi, lakini kipekee niwashukuru vijana wa JKT (Jeshi la Kujenga Taifa) baada ya kufika hapa na kukuta mashamba ni makubwa, hekari kwa hekari, ilibidi tumuombe Meja Jenerali Rajabu Mabele (Mkuu wa JKT) atupatie vijana wa JKT kutoka Kikosi 833 Oljoro na kupitia kwa Kamanda wa JKT Oljoro tumeweza kupata hivyo vikosi vya vijana.

"Tumekuja kufanya operesheni huku, tumenunua mashine mpya za kisasa, kwa ajili ya kufanya hii operesheni na hadi sasa hivi tumeweza kuteketeza hekari 535 kwa muda wa siku nane kuanzia tarehe mbili (Julai 2, 2023) hadi leo (Julai 9,2023) tarehe 9 mwezi wa saba 2023.
"Kwa hiyo niwashukuru wote ambao tunashirikiana nao katika kufanikisha operesheni hii, kwa hiyo niwaombe wananchi wote, kama alivyoagiza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, viongozi wote wa Serrikali kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya, kata, vijiji tushirikiane katika kuhakikisha kwamba, tunatokomeza dawa za kulevya hususani mashamba yote yanayolima dawa za kulevya hasa katika eneo hili la Wilaya ya Same.

"Lkaini, pia tunahakikisha kwamba tunaijengea Serikali uwezo wa kufanya shughuli zake, kutokana na ukwli kwamba wananchi ambao wanalima mashamba ya bangi na mirungi hawawezi kuzalisha pato lolote kwa Taifa, na wanaharibu pia mnyororo mzima wa uchumi wa Taifa.

"Kwa sababu, haya mazao ya dawa za kulevya yanayolimwa hayaiingizii Serikali mapato yoyote, tumekuja katika eneo hili, tumeona Serikali ilivyojenga miundombinu, maji yapo ya kutosha, Serikali imeweka miundombinu ya maji, Serikali imeweka miundombinu ya umeme, lakini Serikali pia imeweka miundombinu ya barabara.

"Lakini, inatumia kodi za maeneo mengine kuja kuweka miundombinu huku, wakati huku wao wanalima mirungi na hawaiingizii Serikali pato lolote, lakini ukiachilia mbali hawaiingizi Serikali mapato, lakini madhara yanayopatikana kwa wananchi, kwa jamii na kwa mtu mmoja mmoja ni mzigo kwa Serikali pia.
"Kwa sababu, watu hao wanaenda pia kutibiwa kwenye hospitali zetu ambazo ni gharama kubwa kuwatibu wale watu, kwa hiyo tuwaombe wananchi wote, jamii yote kuhakikisha kwamba, sisi sote tunapiga vita dawa za kulevya, na katika mkoa huu wa Kilimanjaro nitafanya operesheni endelevu hadi kuhakikisha kwamba, hizi dawa za kulevya zinaisha.

"Ili wananchi waanze kulima mazao mengine mbadala badala ya kuendelea kulima mirungi, tumeona hekari nyingi, tumefika hapa, hekari nyingi za mirungi ambazo imetushangaza pia, hatukutegemea hekari nyingi kiasi hiki hadi mpaka tunachukua vikosi vya jeshi, JKT kuja kufanya kazi ya kuteketeza.

"Hadi kununua mashine za kuteketeza kutokana na ukubwa wa hili eneo, kwa hiyo pia kesho siku ya Jumatatu (Julai 10, 2023) tutakuwa na mkutano mkubwa katika kata hii ya Tae ili kuwaelimisha sasa wananchi juu ya madhara ya kilimo cha mirungi, juu ya madahara ya kiafya yanayotokana na mirungi, lakini pia madhara ya kiuchumi yanayotokana na mirungi ili waweze kuacha.

"Hiki kilimo cha mirungi na kwenda kulima mazao mbadala, kwa sababu eneo hili ni ardhi nzuri,hali ya hewa ni nzuri na linastawi mazao ya aina mbalimbali.

"Kwa mfano huku, kahawa inastawi kwa wingi sana, mahindi yanastawi kwa wingi, maharage yanastawi kwa wingi, lakini pia mazao mbalimbali ya chakula na kibiashara yanastawi huku, kwa hiyo walime hayo mazao mbadala badala ya kujihusisha na kilimo cha mirungi.

"Lakini pia baada ya kuona ile shughuli ambayo tuliifanya kule Wilaya ya Arumeru Mkoa wa Arusha, Kisimiri kule wazazi wametupigia simu kwamba tuje tusaidie kuwaokoa watoto wao, kwamba watoto hawaendi shule, watoto wameacha shule wakaingia kwenye kilimo cha mirungi.

"Wakaomba na sisi tuje huku tukafanye hiyo kazi, na tumekuja tumeshuhudia mashamba makubwa ya kutisha kuhusiana na kilimo cha mirungi, watu wameng'oa kahawa, wameng'oa mazao mengine wamepanda mirungi.

"Na hii mirungi hailingizii pato lolote Taifa, wanauza nchi za nje na wanauza ndani ya nchi, kwa hiyo tuombe vyombo vyote vya dola, Serikali kwa ujumla tusaidiane katika kupambana na zao hili la mirungi katika Mkoa wa Kilimanjaro.
"Lakini pia tusaidiane katika mikoa yote na wilaya zote kuhakikisha tunafanya opereheni wenyewe kama alivyoagiza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwamba, viongozi wote katika maeneo husika wafanye operesheni kuhakikisha kwamba tunatokomeza zao la mirungi na bangi katika maeneo yetu yote,"amesisitiza Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.

Wanavijiji

Kwa upande wake, Janeth Chilambo ambaye kitaaluma ni mwalimu kutoka Kijiji cha Rikwene huko Kata ya Tae wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro amefafanua kuwa,"Sakata hili la dawa za kulevya aina ya mirungi, wananchi wameathirika sana.

"Mwanzoni walikuwa hawajagundua kuwa ni dawa za kulevya, lakini sasa hivi wameshagundua, tunaiomba Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan (Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan) ituletee wataalamu ili wananchi waelimishwe kwamba, zao hili ni zao haramu na ni dawa za kulevya.

"Kwa hiyo waachane na mirungi, wapewe elimu kuhusu kilimo cha mazao, mazao yanakubali, ardhi yetu ni nzuri na ina rutuba, tunaotesha migomba, mahindi yanakubali, viazi ni mazao machache tu ambayo hayakubali.

"Kwa hiyo tunaomba kama Serikali itusaidie ili wananchi wasipate mahangaiko, walime kilimo cha mazao haya mazuri wapate biashara na fedha ili wasihangaike na zao hili (mirungi,"amefafanua Mwanakijiji huyo, Bi.Janeth Chilambo.
Naye, mwanakijiji mwingine wa Kijiji cha Rikweni, Bw. Elisante Sendondo amebainisha kuwa, "Kwa kweli kilimo cha mirungi katika eneo letu, asilimia kubwa ya wanakijiji ni wakulima wa kilimo hiki, na huu mti wameufanya kama mti wa biashara ambao unawaingizia kipato.

"Kwanza niishukuru Serikali, kwa hiki ambacho imekuja kukemea maana Serikali yenyewe ni chombo cha Mungu, ambapo Mungu anakitumia uasi unapokithiri, Mungu anaitumia kama chombo kinachokemea wanaofanya uasi wa ina yoyote si tu wa mirungi, lakini wa aina yoyote kama mauaji na kadhalika.
"Kwa hiyo, ombi langu ambalo ningeiomba Serikali, ingetupa nafasi tukae na watu wetu na Wakristo katika makanisa tuendelee kuwashauri kwa nguvu zaidi ili kwa hiari yao wenyewe waweze kukubali kutokomeza haya madawa ya kulevya (hizi dawa za kulevya)."amefafanua Bw.Senkondo.

Viongozi

Akizungumzia kuhusu hali hiyo, Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Tae wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro, Japhet Msengi amefafanua kuwa, "Mimi pia ni mdau na mshiriki wa shughuli za kimaendeleo katika kata hii ya Tae, hapa leo tupo kwenye operesheni tokomeza madawa ya kulevya (operesheni tokomeza dawa za kulevya) aina ya mirungi.

"Operesheni hii imeanza leo ni takribani siku zisizopungua tatu, ambapo tumekuwa tukipambana kwa ajili ya kusaidia jamii inayotuzunguka juu ya athari ya kilimo hiki cha mirungi.

"Kilimo hiki cha mirungi kwenye kata hii ya Tae kimekuwa ni cha muda mrefu, kwa sababu kama ofisi ya kata tumekwisha pokea barua kutoka kwa mkuu wa wilaya, mkurugenzi kwamba tuungane na viongozi wengine kwa ajili ya kutekeleza madawa ya kulevya (dawa za kulevya) kwa njia kwanza ya kuwapa elimu.
"Kuwaeleza athari za dawa za kulevya, ili mindset (fikra) za wananchi zipate kubadilika, tulijaribu kufanya hivyo kwa miaka takribani isiyopungua sita, tulipoanza hizo operesheni mpaka sasa hivi, lakini wananchi baadhi walipunguza, lakini wengine waliendelea kilimo hiki.

"Kwa sababu, wanadai hili ni zao ambalo wananufaika nalo kupitia biashara huku likiwapatia fedha na mantiki ya wao kulima hiki kilimo wanadai si kwa ajili ya matumizi, wanadai ni kwa ajili ya kuwapatia kipato.

"Kwa hiyo tulijaribu ku-organize na mashirika mengine ya kilimo na taasisi zinazohusika na kilimo ili kuwasaidia zao mbadala litakaloweza kuwasaidia ili waondokane na kilimo hiki, kwa kwanza ni kilimo ambacho Serikali hakitupatii mapato yoyote.
"Kwa hiyo utakuta wananchi wengi wa Tae wanapojiingiza katika kilimo hiki, hatupati mapato na hatuwezi kwenda kwakatia mapato kwa sababu biashara wanayofanya si halali, kwa hiyo unakuta wakati mwingine tunaangaika sana, kwenye kata yetu kupambana na mapato kwa sababu hatuna source (chanzo) hata kama ni mazao tukate risti na Serikali ipate kodi,"amefafanua Kaimu Afisa Mtendaji huyo.

Diwani

Diwani wa Kata ya Tae wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro, Mheshimiwa Samwel Michael Mwambo amefafanua kuwa, "Tushukuru operesheni hii, kwa sababu Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ina nia njema sana na wananchi wa kata hii ya Tae.

"Ni nia njema kwa sababu, lengo lake ni kusababisha wananchi waachane na kilimo hiki cha mirungi ambacho kinasababisha wao wapate madhara makubwa.

"Lakini pia jamii kupoteza mwelekeo, lakini pia katika Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020/2025 imeandika kwamba, utokomezaji wa madawa ya kulevya (dawa za kulevya) ni sehemu ya wajibu wa Serikali.

"Kwa hiyo, wananchi wangu ninawasihi sana, msiendelee na kilimo hiki ambacho kitawaletea madhara makubwa, kitawaletea madhara makubwa kwa sababu mtafungwa, lakini kifungo ambacho ni kikubwa sana, lakini pia jamii pia itapoteza nguvu kazi.

"Ni kwa sababu, watu wakienda kwenye kifungo ina maana kwamba nguvu kazi katika jamii imeisha, kwa hiyo ninawaomba sana, tuendelee na vilimo (kilimo kingine) vingine ambavyo vinaweza vikatusaidia katika uchumi wa kusaidia familia zetu.

"Lakini, tuachane na hili ambalo ni tatizo kubwa katika jamii hii, lakini ndugu zangu ninawaomba tutakuwa na mikutano ambayo itakuwa inaendeshwa kwa ajili ya kutoa elimu, ninaomba kila mwananchi ahakikishe anafika katika mikutano hii ili kupata elimu.

"Tukipata elimu hii itatusaidia katika kubadilika, lakini pia niwaombe Serikali, wananchi hawa wanategemea kilimo hiki kwa sababu hawajapewa elimu ya kilimo kingine, sasa ninawaomba Serikali mtusaidie katika kutoa elimu ili tupate mabadiliko makubwa.

"Tupate kizazi ambacho kitakuwa na ustawi mzuri, lakini pia elimu hizi zitusaidie kutubadilisha katika kutoka kwenye kilimo hiki cha mirungi ili kutupeleka kulima mazao mengine, kwa sababu yapo mazao mengine ambayo yanakubali hapa, mazao mengi.

"Hapa ukilima kabichi inakubali vizuri, ukilima nyanya inakubali vizuri, ukilima vitungu vinakubali vizuri, lakini yapo mazao ya kimkakati kama parachichi hizi ambazo zinauzwa bei kubwa sana nchi za nje, sasa kwa nini tusihamishe kilimo hiki tukapeleka kwenye parachichi ambacho, parachichi ni mti kama huu ambao thamani yake ni kubwa sana.
"Kwa hiyo, ninawasihi tubadilike, tuweze kwenda kwenye kilimo kiki (parachichi na mazao mbadala) ambacho ni kilimo kizuri, ambacho hakisababishi watu kukimbia nyumba, kukimbia opereresheni, lakini pia ukikamatwa ni madhara makubwa, kwa hiyo tuachane na haya ili tuwe wananchi wema,"amefafanua kwa kina Diwani wa Kata ya Tae.

MIRUNGI NI NINI?

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), mirungi ni aina ya dawa ya kulevya inayotokana na mmea unaoitwa “Catha edulis”. 

Mmea huo una kemikali za cathinone na cathine ambazo huongeza kasi ya utendaji wa mfumo wa fahamu. 

Mirungi ilikuwa inatumika tangu enzi za mababu kwenye nchi za pembe ya Afrika hususani Ethiopia, Eritrea, Kenya, Somalia pamoja na Rasi ya Arabuni nchini Yemen. 

Mirungi hutumika zaidi kwenye mikusanyiko ambayo hujumuisha zaidi wanaume ingawa katika miaka ya karibuni wanawake wamejiingiza katika matumizi. 

Nchini kwetu mirungi hustawi na hupatikana kwa wingi katika mikoa ya Kilimanjaro- Same, Tanga- Lushoto na Arusha Mlima Meru. 

Kiasi kingi cha mirungi huingizwa nchini isivyo halali kutoka nchi jirani ya Kenya ambako ni zao halali la biashara. Mirungi hufahamika kwa majina ya gomba, veve, miraa, kangeta, mkokaa, colombo, asili, mbaga, alenle, nk.

MADHARA YA MIRUNGI

  • Huongeza kasi ya mapigo ya moyo hivyo kuweza kuongeza shinikizo la damu, kiharusi na hata kusababisha kifo.
  • Husababisha vidonda vya utumbo mdogo, saratani ya mdomo, koo na tumbo
  • Husababisha upungufu wa msukumo wa kufanya tendo la ndoa, kumaliza haraka na kutoweza kudumu kwenye tendo la ndoa kwa muda mrefu
  • Hupunguza ubora wa mbegu za kiume na kuvuruga mfumo wa utokaji wake na hata kusababisha ugumba
  • Mtumiaji hukosa usingizi na ulevi ukiisha mwilini husababisha usingizi mzito unaoweza kusababisha ajali hasa kwa madereva
  • Huchochea ukatili, fujo, ugomvi, kuongea sana masuala ya kusadikika na kuhangaika.
  • Mtumiaji hukosa kabisa hamu ya kula na kupungua uzito.
  • Mirungi husababisha upungufu wa maji mwilini na kuleta tatizo la kukosa choo pamoja na ugonjwa wa bawasiri
  • Mtumiaji mirungi akiikosa mirungi hupata uchovu, sonona, hasira za ghafla, kutetemeka, kushindwa kutulia na njozi za kutisha (night mares)
  • Utumiaji mirungi huozesha meno na yale yanayosalia hubadilika rangi, fizi kuuma na harufu ya mdomo.
  • Mirungi huharibu ufanisi wa ini mwilini katika kuchuja sumu za mwili
  • Mirungi huamsha magonjwa ya akili yanayojitokeza kwa vipindi “mwezi mchanga” kwa watumiaji wenye tatizo hilo
  • Wanawake wanaotumia mirungi kipindi cha ujauzito wana hatari ya kupata maumivu ya kifua, kuongezeka kwa mapigo ya moyo na msukumo wa damu
  • Matumizi ya mirungi yanaweza kusababisha kuzaliwa kwa watoto wenye uzito mdogo ambao huweza kukataa kunyonya kutokana na ladha ya maziwa kubadilishwa na viuatilifu vinavyotumika kwenye kilimo cha mirungi
  • Watumiaji mirungi hujikuta wakipenda kuvuta sigara au kunywa pombe wanapokosa usingizi hivyo kudhuru zaidi afya zao.
  • Mtumiaji wa mirungi hutumia fedha ambazo zingekidhi mahitaji ya familia kununulia mirungi hivyo kusababisha migogoro
  • Utafunaji mirungi hutumia muda mwingi na hufanyika muda wa kazi au muda ambao mtumiaji hutakiwa kujumuika na familia yake hivyo kushusha uzalishaji na ukaribu wa familia.

Sheria inasemaje kuhusu mirungi?

Mirungi katika taifa letu ni haramu.

Kujihusisha kwa namna yoyote na mirungi (kulima, kuuza, kuhifadhi, kutumia, nk)ni KOSA LA JINAI na adhabu yake inafikia hadi kifungo cha maisha

Baadhi ya nchi za Ulaya ambazo awali ziliruhusu matumizi ya mirungi zimeanza kuiharamisha baada ya kuona madhara yake

Utamsaidiaje mtumiaji wa mirungi

Mtumiaji anaweza kupunguza kiasi anachotumia taratibu na hatimaye kuacha.Aidha, asasi za kiraia huwasaidia watumiaji kuacha kwa kuwapa unasihi. Nyumba za upataji nafuu ‘sober house’ ambako hupitishwa kwenye hatua 12 za upataji nafuu. Kwa msaada zaidi tembelea tovuti www.dcea.go.tz

Ujumbe kwa jamii

  • Mirungi HAIONGEZI ufanisi kazini, ufaulu katika masomo, udereva wala nguvu za kiume
  • Wazazi na walezi wawalee watoto katika maadili mema ikiwemo kuwa nao karibu na kuwasikiliza
  • Vijana wajifunze na kuzingatia stadi za maisha
  • Epuka kutumia dawa za kulevya pamoja na kujiepusha na makundi hatarishi yanayoweza kukuingiza kwenye utumiaji

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news