NA MATHIAS CANAL
MBUNGE wa Jimbo la Bariadi mkoani Simiyu, Mheshimiwa Mhandisi Kundo Mathew amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi kwa wakati.
Amesema kuwa, Rais Dkt.Samia amekuwa kinara kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo ambapo ametaja mafanikio ya miradi mbalimbali ikiwemo kampeni ya kumtua ndoo mama kichwani ambapo upatikanaji wa maji safi na salama katika Jimbo la Bariadi umeongezeka.
Mhandisi Kundo ametoa pongezi hizo mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bariadi lilifanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Alliance leo Julai 15,2023.
Amesema kuwa, kwa mafanikio ya miradi mbalimbali Rais Dkt.Samia anaenda kuandika historia kubwa katika Jimbo la Bariadi na nchi kwa ujumla wake.
Kuhusu Sekta ya Umeme, Mbunge Mhandisi Kundo amesema kuwa, juhudi za wabunge wa Mkoa wa Simiyu wamepeleka ombi kwa Rais Dkt.Samia na tayari shilingi bilioni 76.4 zimetolewa kwa ajili ya kujenga kituo cha kupozea umeme.
"Ndugu zangu haya mambo hayaji hivi hivi ni lazima yaje na kiongozi mwenye maono, lakini Rais hawezi kuota ndoto kwamba Simiyu kuna tatizo la umeme ndio maana mna watoto na mtoto wenu katika Jimbo la Bariadi ni Mhandisi Kundo Mathew akishirikiana na dada yake Ester Midimu, pamoja na mdogo wake Mheshimiwa Lucy Sabu,"amesema Mheshimiwa Kundo.