Mheshimiwa Simbachawene asisitiza jambo kwa wananchi

NA LUSUNGU HELELA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene, amewataka wananchi kuibua miradi ya kimkakati katika maeneo yao ili Serikali iweze kusaidia katika ukamilishaji wa miradi hiyo.

Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi kwa nyakati tofauti katika Kata ya Luhundwa, Lufu, Wangi na Wotta, Wilayani Mpwapwa, Mkoani Dodoma kupitia mikutano ya hadhara katika Vijiji vya Jimbo la Kibakwe, ikiwa ni muendelezo wa kuelezea mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Amesema, Serikali inavutiwa na uongozi wenye maono na mtazamo wa kimapinduzi kwa kuanza kusaidia pale nguvu za wananchi zilipoishia ili kuistawisha jamii hiyo.

Ametolea mfano wa miradi hiyo ya kimkakati kuwa ni ujenzi wa shule, zahanati, nyumba za watumishi pamoja na ujenzi wa kumbi za mikutano.

“Viongozi na watendaji mna kazi kubwa ya kuhakikisha wananchi wanashiriki katika ujenzi wa miradi ya maendeleo, kwani wenye uhitaji ni sisi hatutegemei kuona nyie mpo nyuma katika kutekeleza miradi hiyo. Kila mmoja ana wajibu wa kuchangia na kuona miradi inakamilika kwa wakati na kusimamia matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali,”amesisitiza Mhe.Simbachawene.
Wananchi wa Kijiji cha Kidenge wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene alipokuwa akizungumza nao wakati ziara yake ya kikazi katika Kata ya Luhundwa Wilayani Mpwapwa, Mkoani Dodoma, Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma uliolenga kuwahamasisha wananchi katika kuibua miradi ya kimkakati katika maeneo yao ili Serikali iweze kusaidia katika ukamilishaji wa miradi hiyo na kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Amefafanua kuwa, Serikali ina vipaumbele vingi, hivyo nguvu za wananchi katika kuchangia miradi ya maendeleo haiepukiki.

Ameongeza kuwa, jamii inayojitegemea hujipatia heshima, hivyo kitendo cha vijiji hivyo kubuni na kutekeleza miradi ya maendeleo yake kunaleta heshima kwa viongozi na wananchi kwa ujumla.

Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Simbachawene amepongeza jitihada za viongozi na watendaji wa Kata ya Wangi na Wotta kwa kubuni miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa zahanati na ofisi za Mwenyekiti wa Kijiji, kisha kuiomba Serikali isaidie kukamilisha ujenzi huo.

“Wananchi mkileta ndoo ya maji au mchanga inahesabika mmechangia, mchango sio lazima fedha," amesisitiza.

Amesema, Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kusaidia kukamilisha kwa haraka miradi iliyobuniwa na wananchi kwani kwa kufanya hivyo kutachochea ushindani wa maendeleo katika jamii.

Katika hatua nyingine, Mhe.Simbachawene ametoa wito kwa Viongozi wa Kata nyingine kubuni na kutekeleza miradi kwa kutumia nguvu za wananchi katika maeneo yao ili kuichochea Serikali kuwaongezea nguvu katika hatua za ukamilishaji.

Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Mhe. George Fuime amesema wataangalia uwezekano wa kutenga fedha za kumalizia ujenzi wa ofisi ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Lwihomelo kwa nia ya kuunga mkono shughuli zinazofanywa na wananchi wa Kijiji hicho.

"Mhe. Waziri tutajitahidi katika kuhakikisha fedha zinatengwa kwa ajili ya kuunga mkono nguvu za wananchi katika masuala ya maendeleo yaliyobuniwa na wananchi wenyewe,"amesema Mhe. Fuime.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news