Musoma Vijijini waendelea kuandaa wanasayansi wengi

NA FRESHA KINASA

WANAVIJIJI wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara wamedhamiria kujenga maabara tatu za masomo ya sayansi kwenye sekondari zao za kata ili siku zijazo wawe na wanasayansi wengi ambao watakuwa na mchango chanya kwa jamii na Taifa kwa ujumla. 
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Julai 2, 2023 na Ofisi ya Mbunge Jimbo la Musoma Vijijini, Prof.Sospeter Muhongo ambapo imefafanua kuwa, maabara hizo ni za masomo ya Fizikia, Kemia na Baiolojia.

"Jimbo letu lenye kata 21 zenye vijiji 68 na vitongoji 374 lina jumla ya sekondari 25 za kata, na mbili za binafsi kwa maana ya Kanisa Katoliki na SDA,"imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa, vyanzo vya michango ya ujenzi wa maabara hizo ni fedha taslimu kutoka kwa wanavijiji na Mbunge wao wa jimbo, Prof. Sospeter Muhongo

Pia, kuna nguvu kazi za wanavijiji - kusomba mawe, kokoto, mchanga, maji na kuchimba misingi ya majengo zikiwemo fedha za Mfuko wa Jimbo.

Aidha, kuna fedha kutoka Serikali Kuu kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Wizara ya Elimu na wadau wa maendeleo zikiwemo Benki za NMB, CRDB, NBC na Posta na baadhi ya wazaliwa wa Musoma Vijijini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, sekondari zenye maabara tatu za masomo ya sayansi zilizokamilika na zinazotumika ni (1) Mugango, Kata ya Mugango, (2) Bugwema, Kata ya Bugwema, (3) Kiriba, Kata ya Kiriba, (4) Nyakatende, Kata ya Nyakatende, na (5) Ifulifu, Kata ya Ifulifu.

(6) Makojo Sekondari ya Kata ya Makojo, itakamilisha maabara ya tatu kabla ya Julai 30, mwaka huu na sekondari nyingine 19 za kata zinaendelea na ujenzi wa maabara tatu, na lengo ni kukamilisha ujenzi huo mwakani, kabla ya Julai 2024.

Aidha, sekondari nne mpya zinazojengwa ya Nyasaungu, Muhoji, Wanyere na Rukuba Kisiwani wameazimia majengo ya maabara tatu za masomo ya sayansi yawe sehemu ya ujenzi wa sekondari hizo.
"Halmashauri yetu (Musoma DC) inaendelea kushawishiwa na kuombwa nayo ianze kuchangia, kwa kutumia mapato yake ya ndani, ujenzi wa maabara na maktaba kwenye shule zetu.

"Musoma Vijijini inaomba ipewe High Schools za Masomo ya Sayansi. Sekondari sita zilizotajwa hapo juu ziko tayari kuanza kupokea wanafunzi wa Form V (Kidato cha V) mwakani, Julai 2024.
"Masomo ya Hisabati na Sayansi kwa ngazi ya awali ya shule za msingi na sekondari ndiyo msingi imara wa taaluma mbalimbali za kiufundi zinazotoa, kwa uharaka, ajira ndani na nje ya nchi,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.
Katika hatua nyingine, wanafunzi wa Sekondari za Kata za Musoma Vijijini, wazazi na viongozi wao wa ngazi zote, wanaishukuru Serikali chini ya uongozi mzuri wa Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuchangia ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya elimu jimboni humo.
Picha zilizoambatanishwa zinaonesha wanafunzi wa Kiriba Sekondari wakiwa wanafanya mazoezi kwenye Maabara yao ya Kemia (Chemistry practical class) na maabara mbili (Chemistry & Biology laboratories) za Makojo Sekondari zilizokamilishwa ujenzi hivi karibuni. Ujenzi wa maabara ya tatu (Physics laboratory) ya sekondari hii utakamilishwa kabla ya Julai 30,2023. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news