Mwinjilisti Temba kuwaburuza wamiliki wa mabasi mahakamani kwa kuikwepa Magufuli Bus Terminal?

NA DIRAMAKINI

HUENDA Mwinjiliti wa Kimataifa, Alphonce Boniface Temba akawaburuza mahakamani wamiliki mbalimbali wa kampuni za mabasi kwa kile ambacho amedai ni kuanzisha vituo alivyoviita vya ovyo ovyo mitaani kwa ajili ya kupakia abiria wa mikoani jijini Dar es Salaam.

Temba ambaye ameonesha kuwa na uzoefu wa nchi nyingine zaidi ya 13 duniani, amesema hajawahi kushuhudia mabasi ya abiria yakipakia abiria hadi vituo vya mafuta kama ilivyo Dar es Salaam wakati Serikali imetumia gharama kubwa kujenga Kituo cha Kimataifa cha Mabasi cha Magufuli kilichopo Mbezi katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.

"Hivi karibuni,niliitisha mkutano wa waandishi wa habari Dar es Salaam na mkutano ule uliweza kuhudhuriwa na waandishi wa habari wapatao 25.

"Karibu televisheni zote zilikuwa na wawakilishi, baadhi ya redio, mitandao ya kijamii pamoja na waandishi mbalimbali wa magazeti.

"Nilizungumza kwa hisia ya juu sana na kwa ushawishi mkubwa na huenda kuzungumza kule kunaweza kukatafsriwa na watu wachache, huenda nami nimelambishwa asali au yuko mtu nyuma yangu ananitaka nifanye hili.

"Nataka niwaambie Watanzania, hakuna asali yoyote niliyolamba, hakuna mtu yeyote yuko pembeni wala nyuma kwa yale yote niliyoyazungumza kwa sababu, mimi ni mmoja wa Watanzania wachache waliobahatika kufanya kazi za kimishenari nje ya nchi na nikakaa nchi 13.

"Na katika kukaa huko na kuishi huko,nilijifunza vitu vingi, niliona maisha mengi na kurudi Tanzania kulinipa fursa ya kuona baadhi ya makosa ambayo pia ni ya kisheria.

Mfano

"Lakini tunayanyamazia kimya, tukifiri Serikali ina wajibu mkubwa wa kupambana na yote ambapo siyo kweli. Kwa mfano sasa hivi ukifika Gaborone nchini Botswana ukamuita Mswana yoyote kwa sababu walishaweka sheria, hakuna Mswana yeyote atakayeruhusiwa kukutwa au kuchimba almasi.

"Ni kosa la jinai na lilitungiwa sheria, hivyo mtu yeyote akikutana na Mswana yeyote, sehemu yoyote akamuonesha almasi hata kama umetoka nayo Tanzania au Congo ukamuonesha almasi kereti moja.

"Kereti mbili anaweza akajifanya kanakwamba anakwenda kutafuta maji ya kunywa, kana kwamba anafanya chochote kwa ajili ya kuitetea sheria iliyotungwa, atakuwa wa kwanza kuripoti kwenye kikosi maalum cha polisi.

"Kwamba, kuna mtu hapa anauza almasi au amebeba almasi au ana mawe yanayoashiria kwamba ni almasi kwa sababu wa Botswana wengi hawajui almasi, wanaziona tu, japo kuna ofisi maalum ya ghorofa ipo Gaborone inaitwa ORAPA Hall (ORAPA House).

"ORAPA Hall, ni jumba la makumbusho la kibiashara la Serikali, linaloonesha almasi yote iliyopatikana Botswana, michakato yake, bei zake mkiasi kilichopo, kiasi kilichouzwa na sample Watswana wazione pale Gaborone.

"Kwa hiyo unaweza kuziona hivi kwa kioo, kwa macho, kwa hiyo na hiyo walifanya makusudi ili pia wananchi wajue almasi inafananaje ili biashara hiyo isifanyike kwa njia yoyote ile ambayo ni kinyume cha sheria.

"Hivyo basi, dakika si tatu utakuta umshazungukwa na jeshi maalum la polisi na kukupiga pingu na almasi yako unakwenda kushtakiwa moja kwa moja, hakuna rushwa.

"Wako very smart, angalia kutoka Gaborone kwenda Mafikeni border au Tukweni border ni kilomita 15 kutoka Jiji la Gaborone pale lilipo Bunge au ilipo stendi ya mabasi pale Gaboroine ufike Tukweni border ni kilomita 15.

"Na upande huu wa pili ambao ni wa Afrika Kusini, ambao kwa uhalifu inaongoza duniani, bado Afrika Kusini ndiyo nchi yenye uhalifu mkubwa kuliko nchi yoyote ikifuatiwa na Somalia duniani.

"Na Somalia haiandikwi kama nchi kwa sababu pia maisha ya Somalia yanajulikana, lakini kwa nchi ambayo inaongozwa ina mabunge ina mawaziri, ina mifumo yote ya nchi Afrika Kusini inaonekana ndiyo nchi ya kwanza yenye uhalifu ndani ya nchi, lakini imeshindwa kuingia Botswana, pamoja na Botswana kuwa na mazuri, mvuto mzuri wananchi wanajaliwa vizuri.

"Kwa mfano mabinti wakiwa na miaka 13 na kuendelea wanapata zile pedi wanasema taulo, wanapewa bure nchi nzima, mfumo umewekwa vizuri sana, wanafunzi wa vyuo vikuu ndani ya Botswana, Gaborone University na vyuo vingine vilivopo Botswana, wanafunzi wanapewa zaidi ya laki tatu na nusu kila mwezi.

"Kwa ajili ya chakula, usafiri na kadhalika kwa hiyo ni nchi ambayo imejipanga vizuri, lakini uovu umeshindwa kuingia Botswana si kwa sababu wana jeshi nzuri, si kwa sababu wana polisi na usalama wa Taifa mzuri ni kwa sababu wana Watswana waliowaelimisha na Botswana inatumia gharama kubwa sana.

"Kila siku inatoa maelekezo kupitia gazeti la Serikali linaloitwa Daily News kugaiwa kwa wananchi wote nchi nzima bure, kwa hiyo unakuta kwamba watu wanaiona Botswana, wanasema Botswana ni nchi nzuri, Botswana jamani nimekaa miaka mitano.
 
"Botswana imetumia gharama kubwa kuelimisha wananchi, gaharama kubwa kulinda rasilimali za Taifa ndiyo maana sasa hivi wanaona matunda na matokeo ya ile nchi inasifiwa na mataifa mbalimbali.
"Lakini Watswana wenyewe wanagharamika sana, wakati wa janga la Corona, UVIKO-19 Botswana ndiyo iliyokuwa nchi ya mwisho ambayo ilikuwa imeathirika na UVIKO kuliko nchi yoyote duniani, lakini iliweza kuwaweka Watswana wote ndani.

"Ikawafungia na ikawapa chakula, unafika nje ya geti lako unakuta mfuko wa mchele upo pale, chupa ya lita tano ya mafuta ipo pale, vitunguu na nyanya zipo pale, na chenchi unapokea kwa muda wa zaidi ya miezi mitatu mpaka pale baadaye na mimi nilikuwa mmoja wapo kwenda kuitisha maombi ya Kitaifa Botswana.

"Na baada ya yale maombi ya Kitaifa Botwana kulikuwa hamna tena lile suala la UVIKO-19 nimejaribu tu kutoa mfano wa nchi moja ili kuonesha ni namna gani mataifa yanalindwa na watu siyo Serikali, siyo wafanyakazi wa Serikali kwa sababu hata wafanyakazi wa Serikali na wenyewe wanavunja sheria.

"Ndiyo maana unakuta kuna watu wamefungwa kwa kesi za uhujumu uchumi, watu wamefungwa kwa kesi za utakatishaji fedha, watu wamefungwa kwa kesi mbalimbali na walikuwa wakiitumikia Serikali, wako mahakamani, wako magereza.

Rasilimali

"Hivyo basi, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza kila Mtanzania ni mlinzi wa rasilimali ya nchi.

"Kwa sababu hiyo, mimi kama Mtanzania ninawajibika kulinda rasilimali za nchi na ndiyo maana kwa mantiki hiyo hiyo, kuna rasilimali watu, kuna rasilimali vitu, kuna rasilimali fedha.

"Kuna rasilimali nyinginezo mfano mazao, miti ya mipingo, mbuga za wanyama ile miti iliyopo kule hauwezi ukafika ukaanza kukatakata ovyo ovyo, mtu akikuona anaripoti kwa watu wa idara husika unashughulikiwa, unazuiwa na ndiyo maana ya hifadhi zetu.

"Kuna miti mikubwa sana hata ya mbao ipo kule ndani, haikatwi ovyo kwa hiyo Watanzania hatua zile tabia za kugundua hayo, sisi tumegundua tu eneo moja la wizi, vibaka wa mitaani tunawapigia simu polisi, kuna wezi hapa, kuna majambazi hapa, kuna matapeli hapa wanakamatwa wanapelekwa mahakamani wanafungwa.

"Hivyo hivyo, tunapaswa kutoa taarifa, tunapotoa taarifa kuna Wasomali wamejificha hapa Vigwaza kwenye shamba la NARCO, kuna Wasomali wamejificha hapa Mikumi, Wasomali wamejificha kwenye Mlima Kilimanjaro hapa wanakamatwa wanapelekwa na Uhamiaji, polisi na wanapelekwa mahakamani.

"Hivyo hivyo, tunapomuona mtu anang'oa madaraja, mataruma ya reli ameegesha gari lake amefanya yadi kwenye service road ya Serikali barabara ambayo watu wanatakiwa wapite pale, mtu anageuza kuwa stendi kama walivyogeuza pale Eugen mkabala na Ubungo Plaza.
 
"Watu wanavyokaa pale Manzese kuweka stendi pale Manzese barabarani hata kama amekaa ndani yale magari yanapakia watu kwenye services road yanazuia wengine kupita kwa usalama.

"Ninataka niwaambie Watanzania hivi, unavyoendesha gari hauendeshi peke yako, unapoendesha gari unaendesha magari yanayokuja pamoja na watu wanaovuka njia, kwa hiyo unavyoendesha gari kwa mfano unatoka Ubungo unaenda Kariakoo, unapotoka Ubungo kwenda Kariakoo ukiendesha gari ndiyo maana kuna mpaka wa TANROADS wa jiwe lao.

"Thelathini huku thelathini huku unavyoendesha unatakiwa macho yako si kuangalia mbele tu unapishana na nani, unatakiwa pia uangalie pembeni, unatakiwa pia uangalie kioo chako uone nyuma mathalani mtoto mdogo anaweza akatoka anatambatambaa akaingia kwenye gari yako kama unaangalia tu mbele kama treni.

"Matokeo yake ukamgonga, kichaa anaweza akakimbia hivi hatimaye ukazuia breki usimgonge, sasa magari yanavyoegesha, mabasi yameegesha mpaka services road hebu fikiria yameegesha services road mabasi matatu hadi manne wakati wanatokea watu huko, wewe hauoni kipengele kingine zaidi ya kilomita moja kutoka barabarani.

"Ni makosa, hakuna taifa lolote katikati ya mji mkuu au mji mashuhuri au mji wa kibiasdhara vitu kama hivyo vinafanyika, ni Tanzania peke yake.

"Ni Tanzania peke yake, yanavyopaki hivi inaweza ikawa hata mtoto anatambaa tu pale, yaani mita mbili na kuingia kwenye gari, gari ipo kwenye spidi ya 30 , 40 hata 50 lazima agongwe afe, inawezekana labda mlemavu wa akili, inaweezekana hata ni bibi, inawezekana hata ni mtu wa kawaida, inawezekana hata ni mwendesha baiskeli na kadhalika, mita mbili ni chache sana.

"Kwa maana hiyo, ndiyo maana nilisimama nikamuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aingilie kati, ninashukuru tumemuona Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Chalamila (Albert Chalamila) amekuja akazungumza na wananchi na wafanyabiashara na walipiga makofi mengi sana kumsapoti alichokisema, kwa sababu Chalamila kwa asilimia 99 alionesha uwazi, naye anachukizwa na kitendo ambacho kinafanyika cha mabasi kuegesha kila mahali.

"Na hilo ndilo nilikuwa nimesema, mimi Alphonce Boniface Temba, ujasiri huu ni watu wachache wanao na kwa kuwa, tunao ujasiri huu na hata Serikali nayo itambue ujasiri wa watu wanaojitoa na isitufiche majina yetu, niliambiwa kwenye simu kwamba, jamaa wanakutafuta wamechukia, nikasema mimi Alphonce Temba hakuna aliyezaliwa anaweza kunigusa.

"Kwa sababu mimi nimepakwa mafuta na Mungu mpaka uyaondoe mafuta niliyopakwa ndiyo uniguse, kwa hiyo huyo ajazaliwa kabla ajanikuta macho yake yatakuwa kipofu tayari, Bwana atamshughulikia hilo sina wasiwasi nalo.

"Kwa hiyo wasijisumbue na ninaomba waguswe na ushuhuda, sasa mimi ninamshukuru Waziri Mkuu kwa sababu ninaamini Waziri Mkuu niliyemuomba alilifanyia kazi, na tukaiona sura ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam.

"Lakini, cha ajabu katika mazungumzo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ameonesha kuna vipengele vingi sana kule, yamkini yamkini...yamkini na wafanyabiashara wa mabasi wanajulikana, ninataka nimshihi na kumuomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ninakumbali, ni jasiri na yuko vizuri.

"Wakati huu, lakini nimuobe aliowataja wanaweza kujipanga, figisu zikaingia, kwa sababu amekwishaeleza kila kitu, mambo yanaweza kutengenezwa katikati hapo, akatuletea majibu tofauti.

Mawakili

"Ninataka nimwambie kwamba, baada ya kuiomba Serikali na kumuomba Waziri Mkuu kuingilia kati mimi Alphonce Bonifance Temba nilikuwa nimeshazungumza na jopo la mawakili watatu na wiki ijayo siku yoyote tulikuwa tunaingia Mahakama Kuu ya Tanzania kwenda kuomba tafsri kwa kile kipengele cha kisheria cha kulinda rasilimali za nchi.

"Inipe tafsri kwa nini mabasi haya na haya, machache nimeshachukua picha, mabasi yanajulikana yanaamua kwenda kuharibu service road iliyojengwa kwa zaidi ya shilingi bilioni moja kwa kilomita, kama stedi wakati hapo hapo kilomita tano kutoka pale kuna stedi iliyogharamiwa zaidi ya bilioni 50 kutengenezwa na ni fedha za walipa kodi.

"Nikiwemo mimi na wewe unayenisikiliza, kwa hiyo nilikuwa kwenye hizo harakati tulikuwa tunaenda Mahakama Kuu kuomba tafsri na kuomba kama wamefanya makosa,Mahakama Kuu ieleze wazi na tulikuwa tunaomba fidia ya bilioni tatu.

"Na nilitaka nitoe mchanganuo mzima kwa sababu nimeamua kulizungumza hili, kwamba katika fidia hiyo ya bilioni tatu ambayo tungeenda kupewa na mabasi hayo, makampuni yaliyopo matano yaliyoamua kuasi, mwanzo yalitoka Ubungo vizuri wakaingia kisanii vizuri, wakashangilia baadae wakaanza kutoka mmoja mmoja.

"Wanaenda wanabadilisha maeneo siyo makazi ya stendi anasababisha yeye kusema ni makazi ya stendi, hayana miundombinu wala nini, watu wanakaa barabarani wanapigwa na vumbi, kuna wazee kuna watoto, magari wengine wako kwenye vituo vya mafuta, vikilipuka ni hatari.

"Kwanza kwa sheria na taratibu za Kimataifa hairuhusiwi abiria kuwa kwenye basi, basi linaanza kuweka mafuta kwenye kituo cha mafuta limejaza abiria, lakini Tanzania tunafanya kiholela tu.

"Hivi ni vitu haviruhusiwi, sasa leo kama basi hairuhusiwi kisheria na kitaratibu kujaza mafuta wakati abiria wako ndani, inakuwaje leo abiria wanakuwa pembezoni karibu kabisa, yaani mita tano na pampu ya mafuta, wanavuta sigara eti wanasubiria basi, halafu Serikali haifanyi kitu.

"Watanzania tumekaa kimya? Tunasubiri utokee mlipuko kama uliowahi kutokea maeneo ya Kiluvya magari saba yakateketea palepale, Watanzania wengi wakafa, sasa hatutaki kurudi kwenye hizo historia tena.

"Ndiyo maana mimi Alphonce Temba nikasema hili sitalifumbia macho,sitaliogopa na Katiba inanipa mwanya wa kuwa mlinzi wa rasilimali za Taifa, nikagundua mataifa mengine yanafanya hivyo ndiyo maana yanaendelea.

"Nikasema nitafungua mlango kwa Watanzania, kwa vitendo, kuwaambia hapana, tusikubaliane na vitu kama hivi na waniunge mkono, ninashukuru Watanzania wengi waliniunga mkono na ndiyo maana mbele ya Mkuu wa Mkoa walipiga makofi makubwa sana na wengine walidiriki kutaja hata jina langu.

"Kwa sababu wanajua kabisa kuwa mimi ndiye mwasisi wa jambo hili, na sifanyi kwa kutafuta umaarufu, mimi nimekuwa maarufu, nimekuwa mshauri wa Rais wa Zambia, Michael Satta kwa miaka mitatu, nimekaa nchi zaidi ya 13 duniani.

"Ni umaarufu gani, nimekuwa karibu na JK kwa miaka 10, ni umaarufu gani zaidi ya huo na ni mfanyabiashara pia wa vyombo vya habari na pia nina shughuli zangu, ni kiongozi wa dini kwa mataifa mbalimbali.

"Sihitaji umaarufu zaidi ya huo, kwa sababu haunisaidii kabisa na hakuna nchi hii mtu wa kunihonga huyo ajazaliwa, kwa hiyo nimeyazungumza haya wazi, nikielezea jamii na Watanzania kwa ujumla kwa nia moja kuwa tuwe walinzi wa rasilimali za Taifa.

"Iwe rasilimali mali, iwe rasilimali vitu na fedha na kadhalika. Kwa hiyo nimefungua njia na ninaamini hii njia itaendelea.

"Kwa hivyo, kama Mkuu wa Mkoa alivyosema tumpe muda, mimi bado nipo makini tayari nimeongea na jopo langu la wanasheria wasubirie kwanza tumruhusu mkuu wetu wa mkoa ambaye na mimi ninamkubali amalizie kipengele alichosema mwenyewe.

"Lakini, kwa tahadhari endapo itakwenda kinyume na hivyo, tutakwenda mahakamani na endapo mahakamani hatutakwenda iwapo mkuu wa mkoa atamaliza, basi ipo fedha ambazo nilikuwa nimeitenga kwa ajili ya shughuli za mahakamani, nitazitoa ama kwa mama wajane na yatima, au kwenye kituo cha walemavu, kituo cha yatima.

"Nitaita waandishi wa habari, tutavitafuta vituo na tutavifanya vitu hivi kwa uwazi, ni kiasi gani tutatoa pale, nitakachotoa kama ni keshi, kama ni chakula au kama ni nini tutafanya na nitawaambia Watanzania kuwa huu ni mwendelezo ili ionekane wazi kuwa, sijatumwa na mtu yoyote kufanya haya.

"Tunafanya haya kwa sababu ya utii wa sheria inayotuelekeza tuyafanye na ndiyo maana ningekuwa nimetumwa, fedha fedha za kuwalipa mawakili nisingezipeleka kwenda kuwagawia yatima, ningezitumia mwenyewe au nigezirudisha kwa yule ambaye amenituma.

"Kwa hiyo,leo nimeamua kutulia na kuangalia namna mchakato unavyoendelea, lakini bado ninasisitiza kitendo cha wafanyabiashara wenye mabasi kuegesha kiholela mjini, pia alichoongeza mkuu wa mkoa wanaongeza foleni jijini Dar es Salaam, hakikubaliki.

"Na sasa hivi nipo kwenye kampeni nyingine ya kuhakikisha ninaisaidia Serikali kuondoa malori katikati ya Jiji la Dar es Salaam.Mungu awabariki Watanzania, Mungu ibariki Tanzania, Amen,"amefafanua kwa kina Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba.
 
Temba kwa ufupi
 
Mwinjilisti Temba licha ya kukirimiwa karama maalumu ya Kiungu pia ni mshauri wa masuala mbalimbali ya kisiasa na kiuchumi ambapo ameendelea kuwa na mchango mkubwa kwa taasisi, mashirika na viongozi wa ndani na nje ya Tanzania.

Mathalani mwaka huu wa 2023 alipata mwaliko kutoka kwa mwanasiasa kinara nchini Kenya, Mheshimiwa Raila Odinga katika Ukumbi wa KCC jijini Nairobi ambapo pia aliweza kushiriki maombi maalum kwa ajili ya Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news