NA JAMES MWANAMYOTO
OR-TAMISEMI
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Deogratius Ndejembi amemuagiza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuunda timu maalum ya kukagua matumizi ya fedha kwenye ujenzi wa shule ya Sekondari ya wasichana Kwembe inayojengwa katika Manispaa ya Ubungo kupitia mradi wa SEQUIP.
Muonekano wa moja ya jengo linaloendelea kujengwa katika shule ya Sekondari ya Kwembe ya wasichana kupitia mradi wa SEQUIP.
Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo akiwa katika Manispaa ya Ubungo mara baada ya kutoridhishwa na hatua ya ujenzi iliyofikiwa katika Sekondari hiyo ya Kwembe, licha Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa fedha nyingi ili kukamilisha ujenzi wa shule hiyo maalum ya wasichana ya sayansi.
Mhe. Ndejembi amesema, hajaridhishwa na hatua ya ujenzi iliyofikiwa ikizingatiwa kuwa awali Serikali kuu ilitoa shilingi bilioni 3 na kuongeza bilioni 1.1 na Manispaa ya Ubungo ikaongeza tena bilioni 1.2 ili kukamilisha ujenzi wa miundombinu katika shule hiyo.
“Nilichokiona hapa ni dalili za matumizi mabaya ya fedha iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo ofisi ya Rais-TAMISEMI haiko tayari kuona fedha ikichezewa na ndio maana nimeelekeza uchunguzi ufanyike,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Aidha, Mhe. Ndejembi ameutaka uongozi wa Manispaa ya Ubungo kuongeza usimamizi na kumtaka mkandarasi kuongeza idadi ya mafundi ili shule hiyo ikamilike na kuwapokea wanafunzi zaidi ya 200 waliopangiwa kuripoti katika shule hiyo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi akisisitiza jambo kwa viongozi wa Manispaa ya Ubungo, wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua ujenzi wa shule ya Sekondari ya Kwembe ya wasichana inayojengwa katika Manispaa ya Ubungo kupitia mradi wa SEQUIP.
Akizungumzia kusuasua kwa ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu ya elimu mkoani Dar es Salaam, Mhe. Ndejembi amesema wataalam na wakandarasi wameikwamisha Serikali kutekeleza lengo la kuboresha miundombinu kwa wakati hivyo amewataka kubadilika kiutendaji ili wawe na tija katika maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Hashim Komba ameahidi kuwa atahakikisha anawasimamia wakandarasi na mafundi kufanya kazi usiku na mchana ili shule hiyo ikamilike na kupokea wanafunzi waliopangiwa kuripoti katika shule hiyo.
Tags
Elimu
Habari
Ofisi ya Rais-TAMISEMI
OR TAMISEMI
OR-TAMISEMI
Sekondari ya Wasichana Kwembe
TAMISEMI
Ubungo Manispaa