NA DIRAMAKINI
BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) imetangaza matokeo ya Kidato cha Sita mwaka 2023 huku yakionesha ufaulu wa jumla umeongezeka kwa asilimia 0.26 ikilinganishwa na mwaka jana 2022.
Katibu Mtendaji wa NECTA, Dkt.Said Mohamed amesema, jumla ya watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani ni 106, 883 huku wasichana wakiwa ni 47, 340 na wavulana 59, 543.
Dkt.Mohamed ameyasema hayo leo Julai 13, 2023 wakati akitangaza matokeo hayo katika ofisi za baraza hilo jijini Zanzibar.
"Jumla ya watahiniwa 104,549 sawa na asilimia 99.23 ya watahiniwa waliofanya mtihani wa kidato cha sita 2023 wamefaulu," amesema.
Katika hatua nyingine, Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limefuta matokeo ya watahiniwa 11 wa Kidato cha Sita baada ya kubainika kufanya vitendo vya udanganyifu katika mtihani huo uliofanyika Mei, mwaka huu.
Pia, idadi ya waliofutiwa matokeo mwaka huu imepungua ikilinganishwa na 15 waliofutiwa mwaka jana na 27 waliofutiwa mwaka 2021.
“Baraza limefuta matokeo ya watahiniwa 11. Nane wa shule na watatu wa kujitegemea wa mtihani wa Kidato cha Sita ambao walibainika kufanya udanganyifu,”amesema Katibu Mtendaji wa NECTA.
Bofya Link Hapa Chini
MATOKEO YA MTIHANI WA KIDATO CHA SITA (ACSEE) 2023
MATOKEO YA MTIHANI WA UALIMU (GATSCCE) 2023
Wakati huo huo, Dkt.Mohamed amesema, masomo ya sayansi kwa kidato cha sita mwaka huu yameongoza kwa ufaulu asilimia 74.9.
“Kwa kuzingatia idadi ya watahiniwa zinazoonyesha kuwa idadi kubwa ya waliopata daraja la kwanza na la pili ipo katika tahasusi ya sayansi ikifuatiwa na tahasusi za sanaa,”amesema Dkt.Mohamed.
Kwa mujibu wa matokeo hayo wanafunzi 28,236 waliofanya mitihani ya tahasusi za PCM (Fizikia,Kemia na Hesabu), PCB (Fizikia Kemia na Biologia), na PGM (Fizikia Jografia na Hesabu) wamefaulu kwa daraja la kwanza na la pili.
Aidha, kati ya hizo tahasusi ya PCM ina ufaulu mzuri zaidi ambapo asilimia 45 ya wanafunzi waliofanya mitihani ya masomo hayo wamepata daraja la kwanza ikifuatiwa na tahasusi ya PCB na PGM zilizopata ufaulu wa asilimia 35 na 34 mtawalia.