NA GODFREY NNKO
MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),Hamad Abdallah amebainisha kuwa, shirika hilo linaendelea na kasi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa nyumba za kisasa ili kuhakikisha wanafikia matarajio ya kuwapatia Watanzania makazi bora nchini.
NHC wanashiriki Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba kuanzia Juni 28, 2023 hadi Julai 13, 2023 ndani ya viwanja vya Maonesho ya Biashara vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (SabaSaba) vilivyopo Barabara ya Kilwa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Abdallah ameyabainisha hayo leo Julai 5, 2023 katika banda la NHC lililopo karibu na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Bodi ya Kahawa nchini ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki katika maonesho hayo.
"Tangu nilipoingia katika shirika, jambo kubwa na focus yangu ilikuwa ni kuendeleza strategic plan (mpango mkakati), mtangulizi wangu aliyepita Mchechu (Mkurugenzi Mkuu wa NHC wa zamani, Nehemia Mchechu ambaye kwa sasa ni Msajili wa Hazina) alifanya kazi kubwa sana ndani ya miezi 11.
"Kulikuwa na review ya strategic plan yetu, kwa hiyo ilikuwa ni kutia mkazo kwa staffs wetu kuweza kuelewa mwelekeo wetu ni nini.
"Bahati nzuri ramani yetu yote ya mwelekeo ipo kwenye strategic plan, lakini vile vile kikubwa kilikuwa ni kiu ya Watanzania kujua nini kinaendelea, kulikuwa kuna miradi kadhaa ambayo ilisimama muda mrefu, kwa hiyo kazi yangu kubwa ilikuwa ni kuhakikisha tunaimaliza hiyo miradi.
"Na bahati nzuri miongoni mwenu mlikuwepo kwenye ukabidhishaji wa nyumba kwa wanunuzi katika mradi wa Morocco Square, Jumamosi iliyopita ambayo ni evidence moja kubwa kuthibitisha angalau walau zile nyumba ambazo zilikuwa zimekwama kwa muda mrefu na tukapata sapoti kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan sasa nyumba hizo zimeanza kupatikana.
"Lakini, vile vile kuna nyumba ambazo hazijakamilika tunaongea na makandarasi ili waweze kuingia site, mfano tuna mradi wa 7/11 huu ni mradi mkubwa sana huko maeneo ya Kawe (Dar es Salaam).
"Tupo kwenye mazungumzo na mkandarasi na tunatarajia huenda mwezi ujao tukiwa tumemaliza mazungumzo yetu, mkandarasi arejee site kama haitakuwa mwezi ujao basi itakuwa mwanzoni mwa mwezi wa tisa.
"Lakini, vile vile tumekuwa na miradi ya nyumba 1,000 Dodoma,kuna mradi wa Iyumbu nyumba takribani 300, lakini vile vile tulikuwa na mradi wa Chamwino.
"Lilikuwa ni jukumu langu vile vile kuhakikisha miradi hiyo nayo inakamilika, na nina furaha kuwaambia kuwa, kwa kipindi ambacho nimekaa nimesimamia mradi wa Chamwino tumeweza kuumaliza na tumeweza kuuza nyumba zote.
"Lakini, vile vile mradi wa nyumba za Iyumbu unakwenda vizuri sana,mpaka sasa hivi tunaelekea kwenye nyumba 200 kati ya zile 300 ambazo tulikuwa tunazijenga nazo tumeshaziuza, lakini kuna taasisi ambayo tupo nayo kwenye mazungumzo ambayo itachukua nyumba zote zilizobaki katika ule mradi.
"Sasa hiyo maana yake ni nini? Hii inatupa nguvu sasa ya kufanya miradi mingine katika Jiji la Dodoma, tunatarajia katika mwaka huu wa fedha ambao tumeanza juzi, tutajenga nyumba katika eneo la Medeli ambapo itakuwa ni phase 3 Medeli, lakini tutaanza na mradi wa Samia Housing Scheme phase one Dodoma.
'Mmeona kuna Samia Housing Scheme Dar es Salaam, nyumba 560, kwa hiyo tunakwenda kujenga awamu ya kwanza Dodoma ya nyumba 100.
'Lakini, vile vile tumeangalia fursa kubwa sana, Serikali inajenga mji wa kisasa kabisa, tunaita Goverment City Dodoma.
"Sisi bahati nzuri ni wakandarasi kwenye hiyo miradi, ni wakandarsi kwenye wizara nane,lakini vile vile ni washauri wa wizara hizo,tumeona fursa kwamba Serikali inajenga ofisi au majengo ya Serikali, tukasema wale wafanyakazi wanakwenda kukaa wapi?.
"Maana yake watakuwa wanaenda takribani kilomita 20 hadi 25 kwenda kwenye makazi, kwa hiyo sisi tumeiona kama fursa na kule angalau tumeona tuanze kujenga nyumba takribani 100 kwa ajili ya makazi ya wafanyakazi ambao wapo katika Mji wa Serikali.
"Pia, tumeweza kuongeza nguvu katika Mji wa Serikali, walau uweze kukamilika kwa wakati, lakini vile vile kwa viwango vizuri, na ninajivunia toka nimeingia miezi yangu minne hii nimesisitiza sana kuhusiana na viwango vya nyumba ambayo unaweza kujenga.
"Mfano kidogo, ujenzi wa nyumba za National Housing kule Dodoma zimejengwa kwa viwango bora sana na tumeweza kufikia hatua nzuri, vile vile timu zetu zimeanza kufanya kazi usiku na mchana.
"Kuhakikisha tunafikia dhamira ya Serikali kuona sasa ofisi zote za Serikali za wizara zipo katika ule mji wa Serikali, lakini vile vile nidhamu kwa wafanyakazi.
"Suala la nidhamu, ni kitu ambacho nimekuwa nikisisitiza sana katika kipindi changu tangu nimeingia ofisini, nidhamu vile vile, lakini na weledi kwa kazi tunazofanya, mfano tunataka kazi ambayo inafanywa na mfanyakazi wa shirika (NHC) iwe ni tofauti na taasisi nyingine.
"Tuwe ni watu wa kutolewa mfano mzuri, si mfano mbaya, tunataka tutoe huduma nzuri kwa wateja wetu, na ndiyo maana sasa tunashiriki katika maonesho haya, kuwaonesha watu huduma zetu tunazitoa na tunazitoa kwa kiwango gani.
"Kutoa elimu, lakini vile vile mnafahamu kuwa,shirika sasa limeenda kwenye awamu ya tatu ya Sera ya Ubia ambayo imezinduliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu mwaka jana mwezi Novemba, tulitangaza hiyo miradi na sasa hivi tupo kwenye hatua ya mwisho kabisa ya kufanya uhakiki.
"Ili tuweze kusaini mikataba sasa na wabia ambao tulikuwa tumewapata,eneo la Kariakoo peke yake tuna miradi takribani 16 ambayo tutakuwa tunaifanya kwa njia ya ubia.
"Mtu anaweza kujiuliza kwa nini? Tunaingia ubia wakati shirika linaweza kufanya miradi, tunataka kuleta maendeleo ya haraka katika Taifa letu, na ukitaka kusema tufanye kila kitu sisi peke yetu hatuwezi, lazima tuweze kushirikiana na sekta binafsi.
"Kwa hiyo, ni fursa nzuri vile vile kwa sababu sisi tunamiliki sehemu kubwa ya vitovu vya miji na si vibaya hayo maeneo yakaboreshwa kwa ushirikiano kati ya National Housing na sekta binafsi.
"Kuna miradi ambayo tutaendelea kuifanya sisi wenyewe, miradi mikubwa, kama ilivyo Morocco Square ambayo hata sekta binafsi ukimwambia tufanye mradi ule inawezekana ikawa shida kwake, kwa sababu ni mradi wa zaidi ya shilingi bilioni 100.
"Kwa hiyo, hayo ni mambo muhimu ambayo tunayafanya kama shirika la nyumba kwa kipindi hiki, na ninafurahi kusema kwamba tunapata ushirikiano mkubwa sana kutoka serikalini, lakini vile vile wafanyakazi wa Shirika la Nyumba la Taifa.
Fursa ya Ubia
"Fursa ya ubia,ipo wazi kwa nchi nzima, bahati nzuri Shirika la Nyumba kwa Tanzania bara tuna viwanja, tuna ardhi maeneo yote ya Tanzania, ukisema Masasi tuna viwanja, ukisema Kigoma tuna viwanja hata pembezoni kabisa mwa nchi tuna viwanja, mpaka Mtukula kule ambako ni mpakani tuna viwanja.
"Na tumetoa fursa ya uwekezaji katika maeneo mbalimbali, sasa inategemea na mvuto vile vile wa wawekezaji wanataka maeneo gani, lakini maeneo ambayo yameonesha mvuto mkubwa sana ni maeneo ya Kariakoo.
"Lakini, vile vile tumepata wabia Mwanza, maeneo ya Arusha vile vile, na tulitangaza maeneo ya ubia mpaka Shinyanga na mikoa mingine, lakini ambapo tumepata mwitikio wa awali ni mikoa ya Dar es Salaam, tumepata Arusha na tumepata na Mwanza.
"Je? Awamu ya kwanza ndiyo mwisho, hapana. Inawezekana tukawa tunakwenda kwenye phases kwa baadhi ya maeneo mfano sasa hivi maeneo kama Kariakoo miradi 16 tunaweza kusema kwa kuanzia miaka miwili ya kwanza inatosha, ili sasa iweze kutoa fursa miradi hiyo ifanyike.
"Tunapofanya awamu ya pili, kuwe tayari na maeneo ya kuweza kuwahamishia wale wapangaji ambao wanatumia hayo majengo ambayo tutayabomoa, kwa hiyo wale wa kwanza watakuwa wanatumia, kwa sababu itabidi watafute njia mbadala ya kufanyia biashara.
"Lakini, awamu ya pili kwa sababu tutakuwa, mfano miradi 16 tunaweza kupata maeneo ya biashara takribani 1,500 ambayo itakuwa ni fursa kubwa sana, leo hii tunazungumzia tuna maeneo ya biashara takribani 150 na kidogo kwa sababu wapangaji ambao wataathirika kwenye miradi hiyo ni takribani 200.
"Siyo ile 10,000 au 1,000 ambayo watu walikuwa wakizungumza na kuwa kuna mtu mmoja amechukua miradi yote, hapana wamechukua makampuni ya Kitanzania ambayo yamepatiwa miradi.
"Kwa hiyo fursa ya uwekezaji kwa National Housing inaendelea na baadhi ya plots mpaka sasa hivi zipo wazi, kwa watu ambao wanahitaji kwa ajili ya uwekezaji wanatakiwa walete tu maandiko yao, tutayapitia na kama yatakuwa na tija kwa shirika na Taifa, tunaingia mikataba.Kwa hiyo maeneo yapo Tanzania nzima si Dar es Salaam peke yake.
Samia Housing Scheme
"Mradi tunaouita Samia Housing Scheme, ukisoma Sheria ya Shirika la Nyumba la Taifa, moja ya mandate yake ni kuanzisha schames mbalimbali, kwa miaka mingi tulikuwa hatufanyi schemes mbalimbali, tulikuwa tunajenga tu, sasa kipindi hiki na kwa kutambua kazi nzuri ambayo anaifanya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita.
"Sisi kama Shirika la Nyumba la Taifa tuliona tufanye mradi maalumu ambao ndiyo hizo schemes ambazo tunapaswa kufanya kwa mujibu wa sheria yetu, na huu Mradi tukauita Samia Housing Scheme, ni mradi ambao utakuwa na nyumba bora, lakini vile vile bei zake zitakuwa kidogo nafuu.
"Kwa mfano,tuna studio ambazo tunaita studio appartment ni nyumba ya chumba kimoja, lakini ina sebule na choo na ina sehemu ya jiko, bei yake ni shilingi milioni 37 tu.
"Leo hii ukimwambia Mtanzania aende maeneo ya Kawe kule ambapo yapo karibu kabisa na bahari atafute kiwanja na ajenge nyumba yake hata kama ni ya chumba kimoja.
"Hawezi kupata kwa shilingi milioni 37, lakini shirika la nyumba kupitia huu mradi ambao tunauita Samia Housing Scheme tunaweza kuwawezesha Watanzania sasa kuweza kumiliki nyumba za kisasa.
"Lakini, pia kwa gharama nafuu sana, lakini vile vile hatufanyi Samia Housing Scheme kwa Dar es Salaam tu,tumeanza na nyumba 560 na mpaka leo hii tumeshaweza kuuza nyumba asilimia 81 tukiwa bado tunaendelea na ujenzi.
"Kwa hiyo, utaona jinsi gani Watanzania wanavyochangamkia fursa, lakini tunaenda kufanya mradi kama huo Dodoma,lakini dhamira yetu ni kuweza kufanya mradi kama huo maana yake, housing scheme yenyewe ina jumla ya nyumba 5000.
'Kwa hiyo tutafanya Arusha, tufafanya Mwanza, tutafanya mikoa mingine ambayo tutaona ina soko, kitu cha msingi vile vile iwe na soko, kwa sababu tunatakiwa tujiendeshe kibiashara.
"Miradi yetu mingine tunakopa ili tuweze kurejesha hizo fedha lazima tuuze, kwa hiyo tutakuwa tunafanya uchambuzi wa kila eneo ili kuweza kubaini ni eneo gani lina uhitaji.
"Lakini vile vile kuna soko, kwa hiyo Samia Housings Scheme nyumba 5000 awamu ya kwanza ambayo unaweza kusema ni asilimia 10 ya hizo nyumba, zipo Dar es Salaam, lakini huenda tukaanza phase two ya nyumba nyingine 500, huenda hata kabla ya kumaliza mradi ambao ni phase one, tutakawa tunaanza phase two kwa sababu uhitaji umekuwa ni mkubwa sana.
NHC Sabasaba
Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw.Hamad Abdallah amesema, ameridhika na ushirika wa shirika hilo katika Maonesho ya Sabasaba mwaka huu na huenda mwakani wakaboresha zaidi.
"Sabasaba tumeshiriki mwaka huu, tuna wajibu wa kufanya hivyo, kwa sababu tunapaswa kuwafahamisha Watanzania tunafanya kazi gani, unaweza kuona banda letu sisi ni ndogo, lakini lina taarifa zote muhimu ambazo unapaswa kuzipata, mfano kuna taarifa ya nyumba ambazo shirika linazimiliki takribani 18,000 Tanzania nzima.
"Kwa hiyo, zile nyumba tunazisimamia sisi wenyewe kuna wapangaji, huduma ambazo tunatoa kwa wapangaji, kuna maswali na chochote ambacho unakitaka utakipata hapa, kwa hiyo hata ambao wanahitaji nyumba za kupanga, taarifa zao watazipata hapa.
"Wanataka kuomba nyumba za kupanga, taarifa zao watazipata hapa, na maombi yao yatapokelewa hapa, kuhusiana na kuhusiana na miradi yetu ambayo tunafanya mfano Dodoma, Dar es Salaam na maeneo mengine nchini.
"Taarifa zote utazipata katika banda la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kwa hiyo unaweza kuona banda ndogo lakini lina taarifa zote muhimu na tumeweza ku-display baadhi ya miradi ambayo tunafanya.
"Kwa hiyo, mwaka huu niseme nimeridhika, tumefanya vizuri, lakini huenda mwakani tukafanya vizuri zaidi kuliko mwaka huu.
"Sijasema kwamba mwakani tutafanya kama tulivyofanya mwaka huu, hapana, lakini kila mwaka tunatakiwa tuboreshe.
"Kwa hiyo ni matarajio yangu kwamba mwakani huenda tukapata banda kubwa zaidi ambalo maandalizi yetu tunaweza kufanya mapema zaidi na wakati huo huenda tukawa tuna bidhaa nyingi zaidi za kuweza kuonesha,"amefafanua kwa kina Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw.Hamad Abdallah.