Ni Taasisi ya Moyo, inayotutambulisha

NA LWAGA MWAMBANDE

TANGU ianzishwe Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) mwaka 2015 imekuwa na mchango mkubwa katika utoaji huduma za matibabu, mafunzo na utafiti wa magonjwa ya moyo na mishipa kwa Watanzania na wageni kutoka mataifa mbalimbali.

Mafanikio ya taasisi hiyo yamekuwa yakionekana kila siku huku baadhi ya mataifa hususani Kusini mwa Jangwa la Sahara yakiguswa na utoaji wa huduma na wakati mwingine yamekuwa yakituma wataalamu wake kuja kujifunza mbinu mbalimbali za kitaalamu ili wakazitumie kuwahudumia watu wao huko.

Ni wazi kuwa, ustawi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) katika utoaji huduma unatokana na juhudi za dhati za Serikali kuhakikisha inaendelea kuijengea uwezo wa hali na mali ili iweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, huduma bora za taasisi hizo zinawezesha kulitambulisha vema Taifa letu na hata kuwapunguzia Watanzania gharama za kwenda nje kutibiwa. Endelea;


1.Hili la kujipongeza, hata kwetu Tanzania,
Jinsi tunajiongeza, huduma kutufikia,
Hata wageni kuweza, kuja kwetu jitibia,
Ni Taasisi ya Moyo, inayotutambulisha.

2.Magonjwa mengi ya moyo, ambayo yanatujia,
Ilikuwa ngumu hayo, hapa kwetu kutibia,
Libaki piga miayo, na pengine kujifia,
Ni Taasisi ya Moyo, inayotutambulisha.

3.Waliokuwa na fedha, hizo walizitumia,
Kwenda nje pata ladha, tiba weza jipatia,
Kwa wengine hiyo adha, na vifo kutuzidia,
Ni Taasisi ya Moyo, inayotutambulisha.

4.Enzi Jakaya Kikwete, Rais wa Tanzania,
Hospitali tupate, magonjwa kututibia,
Wagonjwa wengi tupete, na afya kuturudia,
Ni Taasisi ya Moyo, inayotutambulisha.

5.Kwa sasa wagonjwa wengi, hapo inatutibia,
Na kwa hiyo watu wengi, ahueni yarudia,
Twaokoa fedha nyingi, na maisha nakwambia,
Ni Taasisi ya Moyo, inayotutambulisha.

6.Taasisi hiyo yetu, hapo haijaishia,
Hata kwa jirani zetu, tiba wanajipatia,
Hiyo ni huduma yetu, kutokea Tanzania,
Ni Taasisi ya Moyo, inayotutambulisha.

7.Wametangaza majuzi, hili la kufurahia,
Tunazidi panda ngazi, huduma afya sikia,
Imekuwa mkombozi, Afrika yote pia,
Ni Taasisi ya Moyo, inayotutambulisha.

8.Nchi sasa ishirini, wagonjwa wanatujia,
Hapo hospitalini, kuweza kujitibia,
Rekodi kubwa nchini, hapo ilipofikia,
Ni Taasisi ya Moyo, inayotutambulisha.

9.Pongezi tunazitoa, kwa wote Watanzania,
Huduma wanaotoa, kwa wagonjwa wa dunia,
Mnayofanya ni poa, sote tunafurahia,
Ni Taasisi ya Moyo, inayotutambulisha.

10.Tiba pia utalii, jinsi watu watujia,
Uchumi haubakii, pale ulipoishia,
Tuzidishe kazi hii, wengi wakifurahia,
Ni Taasisi ya Moyo, inayotutambulisha.

11.Hongera kwa serikali, hii yetu Tanzania,
Inafanya kazi kweli, huduma kutupatia,
Za afya nyingi ni ghali, kwetu tunajipatia,
Ni Taasisi ya Moyo, inayotutambulisha.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news