NA SIXMUD J.BAGASHE
NYUMBA ya asili ya kabila la Wazanaki iliyojengwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia taasisi yake ya Makumbusho ya Taifa, imekuwa kivutio kikubwa kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba.

Mhifadhi mila mwandamizi wa Makumbusho ya Taifa, Bi. Flora Vincent amesema kuwa, sababu ya kuwa na Onesho la Nyumba ya asili kwenye maonesho hayo makubwa ni kuipa fursa jamii kujifunza umuhimu wa kurithisha kizazi kilichopo mila na desturi za makabila mbalimbali ili kuimarisha Mshikamano wa Kitaifa, Umoja, Upendo, amani kwa maendeleo endelevu nchini.
Akizungumzia maonesho hayo,Debora Danishashe amesema, ameamua kuwaleta wajukuu zake kwenye nyumba hiyo ili wapate uelewa juu ya urithi wa utamaduni, wa makabila mbalimbali ya Tanzania.

Katika nyumba hiyo ya asili ya Wazanaki watu wamepata fursa ya kujifunza kucheza bao, kukumbushwa maadili, aina za vya kula,mavazi ya asili na jinsi ya kuhifadhi mazao kiasili.