NA VERONICA MWAFISI
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka Maafisa Utumishi wote kuhakikisha maombi yote ya watumishi wa umma nchini wanaostahili kupanda madaraja yanawasilishwa katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili yaweze kushughulikiwa kwa wakati kwa lengo la kutenda haki na kuondoa malalamiko yasiyokuwa na ulazima.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (katikati) akisikiliza hoja iliyokuwa ikiwasilishwa kwake na Mtumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo mkoa wa Pwani iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.
Mhe. Kikwete amesema hayo alipokuwa akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji na kutatua kero na changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.
Mtumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani Mwalimu Belloh Mkwazu (Aliyesimma) akiwasilisha hoja kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo mkoa wa Pwani iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.
“Serikali imeshatoa maelekezo ya kuwasilisha maombi ya watumishi wa umma wanaostahili kupanda madaraja ili yafanyiwe kazi, hivyo Afisa Utumishi hakikisha unahakiki vizuri na kuwasilisha maombi ya kupandishwa madaraja kwa watumishi hawa,” amesisitiza Mhe. Kikwete.
Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Mhe. Muharami Mkenge akitoa salamu za wananchi na watumishi wa jimbo la Bagamoyo kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.
Mhe. Kikwete amesema kuwa, Serikali inayoongozwa na Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan haina tatizo katika suala la kutafuta mafungu ya fedha kwa ajili ya kuwapa watumishi wake stahili zao ili waweze kufanya kazi vizuri.
Mhe. Kikwete amesema kuwa, Mhe. Rais Dkt. Samia anataka watumishi wake wawe na ari ya kufanya kazi kwani kukiwepo na manung’uniko itaondoa morali ya kufanya kazi.
Sehemu ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa halmashauri hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Bw. Shauri Selenda, amemshukuru Naibu Waziri Kikwete kwa kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi hao kwa ajili ya kuzifanyia kazi.
Aidha, Mkurugenzi Selenda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa stahiki mbalimbali za watumishi ikiwemo upandishwaji vyeo, ubadilishwaji kada, ajira mpya, vibali vya uteuzi, ulipaji wa malimbikizo ya mishahara, fedha za matibabu, mafao ya uzazi, fidia za watumishi wanaoumia kazini, pamoja na kuboresha vitendea kazi na maeneo ya kazi.
Afisa Utumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani Bw. George Mwalukasa akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) mara baada ya Naibu Waziri huyo kuhitimisha kikao kazi chake na watumishi wa halmashauri hiyo kilicholenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya watumishi wengine, Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Bw. George Mwalukasa ametoa ahadi kwa Mhe. Naibu Waziri Kikwete kuwa watatekeleza maelekezo yote ambayo amewaagiza na kuhakikisha kwamba watumishi wote waliokuwa na changamoto za madaraja wanapatiwa ufumbuzi kama Serikali ilivyoelekeza.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amehitimisha ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Pwani iliyokuwa na lengo ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma, kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma pamoja na kukagua utekelezaji wa Miradi ya TASAF.