Papa Francis amteua Askofu Protase Rugambwa kuwa kardinali Tanzania

NA DIRAMAKINI

PAPA Francis ambaye ni Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani amemteua, Mhashamu Baba Askofu Mkuu Mwandamizi Jimbo Kuu la Tabora, Protase Rugambwa kuwa Kardinali nchini Tanzania.

Protase Rugambwa anakuwa Kardinali wa tatu nchini Tanzania akitanguliwa na Laurean Rugambwa aliyefariki dunia Desemba 8, 1997 na Polycarp Pengo aliyestaafu mwaka 2019.

Papa amemteua Rugambwa kuwa kardinali ikiwa ni takribani miezi mitatu tangu alipomteua kuwa askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo Kuu la Tabora.

Askofu Rugambwa aliwahi kuwa askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma tangu mwaka 2008 hadi mwaka 2012 pamoja na Katibu Mkuu wa Idara ya Uinjilishaji Vatican.

Wasifu

Protase Rugambwa alizaliwa Mei 31, 1960 wilayani Bukoba mkoani Kagera ambapo alisoma katika seminari ndogo za Katoke iliyoko Jimbo la Rulenge-Ngara na Itaga mkoani Tabora.

Rugambwa alipata daraja takatifu la upadri Septemba 2, 1990 ambapo alibahatika kupewa daraja hilo na aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki wakati huo, Papa Yohane wa Pili alipotembelea Tanzania.

Baada ya kupewa daraja hilo takatifu, alipangiwa kuwa Padri wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara.Kuanzia mwaka 2002 hadi mwaka 2008 alifanya utume wake katika Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu Vatican.

Januari 18, 2008 aliteuliwa na Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani wakati huo, Papa Benedikto XVI, kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma.

Miaka minne baadaye Juni 26, 2012 aliteuliwa kuwa Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari na wakati huo huo kumpandisha hadhi na kuwa ni Askofu mkuu.

Utume wa Rugambwa uliendelea hadi Novemba 9, 2017 alipoteuliwa na Papa Francisco kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu alitumikia baraza hilo kwa vipindi viwili hadi muda wake wa kikatiba ulivyoisha.

Pongezi

Kwa nyakati tofauti viongozi wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan wamempongeza Mhashamu Baba Askofu Mkuu Mwandamizi Protase Rugambwa kwa uteuzi huo.

"Nakupongeza Askofu Mkuu Protase Rugambwa kwa kuteuliwa na Baba Mtakatifu Fransisko kuwa Kardinali. Naungana na Watanzania wote kukutakia kheri na kukusindikiza katika sala, unapoendelea na kazi yako ya utume katika hatua hii mpya.

"Mwenyezi Mungu ambaye amekuinua kwa baraka na jukumu hili kwenye wito wako, aendelee kukuongoza katika kulitumikia Kanisa na jamii yetu kwa ujumla,"Rais Dkt.Samia amempongeza Mhashamu Baba Askofu Mkuu Mwandamizi Protase Rugambwa.

Dkt.Mpango

Naye Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Philip Isdory Mpango amefafanua kuwa, "Mhashamu Baba Askofu Mkuu Mwandamizi Protase Rugambwa. Nimepokea kwa furaha kubwa kuteuliwa kwako na Baba Mtakatifu Fransisco, kuwa Kardinali wa Tatu katika nchi yetu ya Tanzania. Uteuzi huu unathibitishwa na maneno kutoka Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (8:28) kwamba:

“Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.” HONGERA SANA,"ameeleza Makamu wa Rais Dkt.Mpango.

Dkt.Mwinyi

Kwa upande wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameeleza kuwa, "Nampongeza Mhashamu Baba Askofu Mkuu Mwandamizi Protase Rugambwa kwa kuteuliwa na Baba Mtakatifu Fransisko kuwa Kardinali wa Tatu wa Tanzania.

"Naungana na Watanzania kukutakia heri kwa majukumu yako mapya katika Kanisa Katoliki nchini.Mwenyezi Mungu aendelee kukusimamia.,"amefafanua Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news