NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amehitimisha ziara yake ya siku tano nchini China ambayo imeonekana kuwa na mafanikio zaidi.
Akiendelea na ziara ya nchini China, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi alihudhuria Maonesho Makubwa ya Tatu ya China na Afrika yaitwayo China- Africa Economic and Trade Expo katika jiji kubwa la Changsha na baadae mkutano maalum katika sekta ya afya uliogusia ushirikiano mzuri uliopo wa afya baina ya Tanzania na China.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesema atawasaidia wawekezaji wanaokumbana na vikwazo na changamoto mbalimbali ili waweze kushiriki kikamlifu kuwekeza katika miradi mbalimbali nchini.
Aliyasema hayo alipozungumza na wawekezaji wa kampuni mbalimbali za China waliofika kuzungumza naye kuhusiana na fursa za uwekezaji zinazopatikana Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Akizungumza na Mwenyekiti wa Kundi la Kampuni za Liyu Group,Yuefeng Wang wanaojishughulisha na utengenezaji viatu na kuzalisha umeme, amemwambia nishati kwa sasa inahitajika zaidi Zanzibar kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya viwandani. Muhimu ijulikane gharama zao na aina ya umeme ambapo kuhusu biashara ya viatu, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi aliwashauri wawekezaji hao kuangalia soko pana la Afrika.
Pia, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi alikutana na Bw.Quan Chen wa Kampuni iliyopo Tanzania, iitwayo Tanzania Binjiang inyoshughulika na usindikaji wa nyama na kumweleza soko la nyama lipo kubwa. Ila afuate tu taratibu.
Mheshimiwa Rais Mwinyi alikutana na Bi.Xiaoli Zhou mwekezaji wa utalii wa michezo na akamkaribisha kuwekeza Zanzibar na anawakaribisha pamoja na kundi la wafanyabiashara wanawake kuitembelea Zanzibar.
Vilevile Mheshimiwa Rais Dk.Mwinyi alihojiwa na vituo viwili vikubwa vya China vinavyorusha matangazo kwa lugha ya Kiingereza.Vituo hivyo ni China Global TV Network na baadae Shirika la Habari la China-XINHUA.
Mahojiano hayo yalijikita zaidi juu ya uhusiano wa China na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla na sera za China barani Afrika.
Silent Ocean
Awali Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi alifungua rasmi ofisi za Kampuni ya Silent Ocean maarufu Simba wa Bahari, inayojishughulisha kusafirisha mizigo kutoka China kuja Tanzania.
Dkt.Mwinyi alisema kuna biashara kubwa kati ya Tanzania na China na kwa kuifungua ofisi hiyo ushirikiano wa kibiashara utaongezeka zaidi baina ya nchi mbili hizo.
Pia aliwahimiza wawekezaji wa China kuwekeza zaidi Zanzibar na angependa kampuni za China zije Tanzania kuangalia fursa zaidi za kuwekeza.
Akimkaribisha Rais Dkt.Mwinyi kufungua rasmi kampuni hiyo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini China, Mheshimiwa Mbelwa Kairuki alisema, kufunguliwa kwa Kampuni ya Silent Ocean iwe ni chachu kwa kampuni nyingine za Tanzania kuendeleza ushirikiano wa biashara na China.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Silent Ocean, Salaah Said Mohamed alisema wanahudumia na kupeleka mizigo kutoka China kwenda nchi zote za Afrika Mashariki na Kati kwa miaka 19 sasa.
Mohamed alibainisha uwezo wa kampuni yake kuusafirisha makasha 600 hadi 1000 kwa mwezi na kupongeza uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan na Xi Jing Ping wa Jamhuri ya Watu wa China kufungua njia ya ushirikiano kati ya China na Afrika.
Makamu
Pia, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi alikutana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Han Zheng.
Katika mazungumzo yao viongozi hao wawili walipongeza ushirikiano unaoendelea kushamiri baina ya Tanzania na China na Zanzibar kwa upande mmoja.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi aliipongeza Serikali ya China kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika miradi ya maendeleo kwa miaka 59 sasa tangu Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964..
Alibainisha uamuzi wa hivi karibuni wa viongozi wakuu wa nchi hizo mbili, Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na Xi Jing Ping wa kufungua zaidi njia kuu za uhusiano umesaidia kuimarisha uhusiano.
Rais Dkt.Mwinyi alimweleza Makamu huyo wa Rais wa China kuhusu Sera Kuu ya Zanzibar ya Uchumi na kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchi hiyo kusaidia katika uwekezaji.
Sekta hizo ni utalii, mradi wa ujenzi wa Bandari Kubwa ikiwemo ya Mangapwani itakayonufaisha mataifa mengine ya Afrika, uchimbaji wa mafuta na gesi, uvuvi na usafiri wa baharini.
Zhang
Naye Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, alimhakikishia Rais Dkt.Mwinyi kwamba nchi yake imejizatiti kuiunga mkono Zanzibar kufikia hatua kubwa ya maendeleo ambapo alisema kwa sasa Serikali yao inawahimiza watalii wengi wa China kuitembelea Zanzibar.
Mheshimiwa Zhang alimpongeza Rais Dkt.Mwinyi kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya ya maendeleo na kusema chini ya uongozi wake Zanzibar imepiga hatua kubwa ya maendeleo.
Shukurani
Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi aliishukuru Serikali ya China kwa misaada ya kitabibu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rais Dkt.Mwinyi alieleza kwamba hadi sasa China imekwishaleta Tanzania matabibu zaidi ya 2,000 kwa kipindi cha miongo sita ya uhusiano baina ya nchi mbili hizi.
Aliyaeleza hayo katika mkutano maalum wa Sekta ya Afya kwa ushirikiano uliopo baina ya China na Tanzania, uliofanyika katika jiji la Changsha jimboni Hunan.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi alieleza kufurahishwa na kazi kubwa inayofanywa na madaktari hao kutoka Jimbo la Hunan nchini China.
Ametaka kuendelezwa zaidi ushirikiano baina ya watu wa sekta za Afya wa China na Tanzania, China waendelee kutoa misaada ya mafunzo ya kitabibu, pia aliwahimiza Wachina washajihishwe kuwekeza katika maduka ya dawa na kuwepo ushirikiano zaidi wa kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.
Karibuni
Aidha, katika hatua nyingine, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amezikaribisha kampuni nyingi za China kuwekeza katika Bara la Afrika, kwani kuna ardhi ya kutosha, nguvu kazi nyingi na Afrika ina uthubutu wa kufanya biashara.
Mheshimiwa Dkt.Mwinyi aliyasema hayo wakati wa sherehe za ufunguzi wa mkutano wa tatu wa ushirikiano wa Biashara Kati ya China na Afrika, uliofanyika katika Jiji la Changsha jimboni Hunan.
Pia, alisifu ushirikiano baina ya China na Tanzania ambao sasa umetimiza miaka 60 na akaonesha matumaini yake ushirikiano huo utazidi kukua na kuimarika.
Alisema, katika miaka miwili iliyopia Afrika imeshuhudia ushirikiano mkubwa na China ambapo biashara imeongezeka kwa zaidi ya dola bilioni 74.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi alifurahi kuona wawekezaji wakubwa wa China wamehudhuria mkutano huo na akabainisha hiyo ni fursa kwa Afrika kukaribisha wawekezaji hao barani humo.
Mapema akifungua mkutano huo kwa niaba ya Afrika, Rais wa Malawi, mheshimiwa Lazaro Chikwera alitaka kuwe na mbinu madhubuti za kuzuia jaribio lolote la kupunguza kazi ya ushirikiano baina ya China na Afrika.
Alisema, China na Afrika hazina tena muda wa kuzorotesha uhusiano huo na kuwataka Waafrika kutumia kwa vitendo yale yote waliyojifunza kwa muda wote wa ushirikiano na China.
Mheshimiwa Rais Chakwera aliwataka Waafrika kutumia kipindi hicho kutangaza zaidi bidhaa zake mbalimbali. Pia, aliitaka China kufikiria kuanza kusamehe mikopo yake kwa Afrika hali itakayosaidia bara hilo kuendelea kupiga hatua za maendeleo.
Hunan
Mbali na hayo, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi alisema, ushiriki wa Tanzania katika Mkutano mkuu wa Tatu wa China na Afrika umeimarisha zaidi uhusiano wa watu bara hilo na China.
Aliyasema hayo alipokutana na Gavana wa Jimbo la Hunan jijini Changsha nchini China, Mheshimiwa Mao Weiming kwa mazungumzo.
Jimbo la Hunan lenye watu milioni 73 ndipo alipozaliwa Mwenyekiti wa kwanza wa Chama cha Kikomunisti cha Watu wa China, marehemu Mao Tse Tung ambapo, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi alisifu kazi kubwa ya utabibu inayofanywa na Jimbo la Hunan katika Hospitali ya Mnazi Mmoja.
Alionesha matumaini yake kwamba ushirikiano huo utazidi kuimarika ambapo kwa upande wake Gavana Mao ametaka uhusiano uzidi kuimarishwa katika nyanja nyingine ikiwemo biashara.
Wawekezaji
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameendelea kuhimiza wawekezaji wa China kuangalia fursa zilizopo za kuwekeza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Aliyasema hayo alipokutana na wawekezaji na wenye kampuni mbalimbali za China ambapo pia, alikutana na Kampuni kubwa za kiufundi za KVS Chemical, Hunan Communications, Economic Engineering, Afri Greencrops Group na Sino Tech Kibaha Industrial Park.
Katika mazungumzo yao, Rais Dkt.Mwinyi alisisitiza ushirikiano wa China na Tanzania ni wa kihistoria na wawekezaji hao aliwaambia sera kuu na muhimu ya Zanzibar ya uchumi wa buluu ambapo vipengele vinne vilivyomo waangalie namna fursa zitakazowafaa wazichangamkie.
Aliwafahamisha chini ya mwamvuli wa Sera ya Uchumi wa Buluu kuna utalii ambapo angependa kuona watalii wengi zaidi kutoka China wanatembelea Zanzibar na kwa wawekezaji kuangalia fursa za kujenga hoteli kubwa za watalii.
Kwa upande wa uvuvi aliwakaribisha kuwekeza katika eneo la uvuvi wa bahari kuu na uvuvi wa kawaida kwani soko la bidhaa za bahari ni kubwa hata kwao.
Pia aliwaalika kuangalia uwezekano wa kushiriki katika mradi wa mafuta na gesi kutokana na ubobezi wao katika sekta hiyo.
Maeneo mengine, Rais Dkt.Mwinyi aliyowaalika wawekezaji hao ni katika ujenzi wa Bandari kubwa ya Mangapwani itakayohudumia nchi nyingi za Afrika. Kwa upande wa Tanzania Bara aliwaalika wawekezaji hao kwenye kilimo, kwani kuna ardhi kubwa yenye rutuba.
Hata hivyo, wawekezaji hao walivutiwa zaidi na sekta ya mafuta na gesi na wameonesha utayari wao kujitosa kwenye mradi huo kwani kwa China kampuni yao ni ya tatu kwa ukubwa kwenye sekta ya mafuta.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi alikutana na Rais wa Kampuni ya China Civic Engineering Construction Corporation- CCECC.Hii ni kampuni kubwa ya ujenzi yenye miradi 27 ya ujenzi wa barabara Tanzania.
Rais Dkt.Mwinyi alionesha kuridhishwa na kasi na uwezo mkubwa wa kampuni hiyo kwenye miradi ya barabara Zanzibar akitolea mfano barabara ya Kaskazini Unguja ambayo ni bora sana.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi aliiomba kampuni hiyo kusaidia kurudishwa kwa mikopo kutoka taasisi za fedha zikiwemo benki.
Mke wa Rais
Wakati huo huo, Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mama Mariam Mwinyi amewahimiza wanawake kushikirikiana katika jitihada za kujikwamua kiuchumi ili kujenga maisha bora kwa jamii.
Mama Mariam Mwinyi aliyasema katika mkutano wa kwanza wa Ushirikiano wa Wanawake wa China na Mataifa ya Afrika uliofanyika jijini Changsha.
Mkutano huo ulioandaliwa na Taasisi ya ALL China Women Federation pia ulihutubiwa na wake wa Marais wa China, Malawi na Burundi.
Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwa na ujumbe wake walirejea nchini Julai 2, 2023 baada ya kukamilisha ziara yake ya kikazi nchini China aliyoianza Juni 27, 2023.
Picha mbalimbali zikionesha ziara ya Rais Dkt.Mwinyi nchini China. (Picha zote na Ikulu).