Rais Dkt.Mwinyi: Uturuki kuna fursa, na sisi zile fursa tunazitaka hapa nchini

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amekutana na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uturuki, Mheshimiwa Idd Seif Bakari aliyefika Ikulu jijini Zanzibar leo kumuaga kuelekea katika kituo chake cha uwakilishi baada ya uteuzi wake hivi karibuni.

Katika mazungumzo na Balozi Bakari, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amegusia mambo mbalimbali katika kufungua fursa za uwekezaji na biashara kati ya Tanzania,Zanzibar na Uturuki ikiwemo kupata wawekezaji katika viwanda kwa maendeleo waliyopiga kupitia sekta hiyo kuja kuwekeza nchini.

Eneo lingine, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amemtaka kuzitangaza fursa zilizopo katika sekta ya utalii wa fukwe za bahari na urithi pia kupitia kuwepo kwa usafiri wa ndege ya Shirika Ndege la Uturuki linalofanya safari zake za moja kwa moja hapa nchini ili kutangaza vivutio vinavyopatikana nchini.

Sambamba na kujifunza na kutafuta fursa za uwekezaji zitokanazo na sekta ya miundombinu ikiwemo bandari, barabara, na viwanja vya ndege.

"Kama tunavyofahamu nchi ya Uturuki ni moja katika nchi ambazo ziko mstari wa mbele sana katika viwanda, ukiacha China nadhani Uturuki ipo pale juu kwa watu ambao wanazalisha vitu vingi sana.

'Kwa hivyo,ushauri wangu utakavyokuwa pale, basi ufanye mawasiliano na wafanyabiashara wa pale,ili tuweze kupata wawekezaji, wawekezaji katika eneo la viwanda, uwekezaji katika maeneo ambayo wenzetu wameshapiga hatua ili waje kuwekeza huku.

"Badala ya sisi kwenda kununua tu kutoka kwao, nadhani ni vizuri tukawashawishi kuja kuzalisha hapa nchini, na uchumi wa nchi yoyote ile unategemea miundombinu ya nchi hiyo, kwa hiyo, nikutakie majukumu mema ukiwa kule, lakini ukae ukijua kabisa kwamba iko fursa kubwa kule.

"Hivyo yafaa kushirikiana nao katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi, kwa sababu sasa hivi kazi kubwa mliokuwa nayo ninyi wawakilishi wetu katika nchi hizo, ni diplomasia ya uchumi kwa hiyo basi tujikite katika masuala ya uchumi, na haya niliyoyasema mimi ni machache tu, ninajua kuna fursa nyingi kule kwa hiyo uzitazame kwa ujumla.

"Na zote utakazoona zina manufaa kwa Zanzibar na kwa Tanzania kwa ujumla, basi utusaidie tuweze kuzipata fursa hizo kuja hapa nchini,"amefafanua kwa kina Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi na kumshauri Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uturuki.

Kwa upande wake Balozi Idd Seif Bakari amesema, Uturuki ina shirika la ndege ambalo linafanya safari zake za moja kwa moja kutoka huko kuja hapa nchini, hivyo atashirikiana nao kuhakiksha fursa za utalii zinapatikana kwa wingi.

Balozi Idd Seif Bakari aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uturuki Aprili 5, mwaka huu, kabla ya uteuzi huo alikuwa Konseli Mkuu, Dubai.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news