Rais Dkt.Mwinyi:Hii ni heshima, hongera Dkt.Salim Ahmed Salim

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amempongeza Dkt. Salim Ahmed Salim kwa kutunukiwa tuzo ya heshima ya juu zaidi na Rais wa Jamhuri ya Cape Verde,Dkt.Jose Maria Neves.
"Nachukua fursa hii kumpongeza kwa dhati Dr.Salim Ahmed Salim kwa heshima kubwa aliyotunukiwa na Rais wa Cape Verde kwa mchango wake katika ukombozi wa Bara la Afrika.

"Tukio hili la kipekee ni heshima kubwa si tu kwake binafsi,bali pia kwa sisi Watanzania na Waafrika kwa ujumla;

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ametoa pongezi hizo leo Julai 7, 2023 ikiwa ni siku mbili zimepita tangu Dkt.Salim atunukiwe tuzo hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Julai 6, 2023 na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilieleza kuwa,Mheshimiwa Dkt.Jose Maria Neves, Rais wa Jamhuri ya Cape Verde amemtunuku Mhe.Dkt Salim Ahmed Salim, Waziri Mkuu wa Zamani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Katibu Mkuu wa Zamani wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Tuzo ya Juu ya Heshima ya Nchi: The 'Amilcar Cabral' (Order of Amilcar Cabral-First Class).

Ni kupitia sherehe iliyofanyika Julai 5, 2023 mjini Praia, Cape Verde wakati wa maadhimisho ya Miaka 48 ya Uhuru wa Kitaifa wa Jamhuri ya Cape Verde.

Tuzo hiyo ya juu zaidi nchini humo ilitunukiwa Mhe.Dkt.Salim Ahmed Salim kwa kutambua jukumu lake la kujitolea kuelekea mapambano ya utu na kujitawala kwa Cape Verde.

Aidha, tuzo hiyo ilipokelewa kwa niaba yake na mtoto wake, Bw. Ahmed Salim. Kupitia tamko la Rais wa Cape Verde ambalo lilienda sambamba na tuzo hiyo lilifafanua kuwa;

“Dkt.Salim katika nafasi yake kama mtetezi wa Cape Verde na mfuasi mwenye shauku na mipango ya kisiasa na kidiplomasia ya Amilcar Cabral na taasisi za Umoja wa Mataifa pia inapaswa kuangaziwa, ikiwa ni pamoja na pendekezo la kutuma, mwezi Aprili 1972, ujumbe wa uchunguzi kwa mikoa iliyokombolewa ya Guinea-Bissau.

"Hatimaye, ili kuhitimisha dhamira yake isiyoshindwa ya ukombozi wa nchi yetu, alikwenda moja kwa moja, hadi jiji la Praia kushuhudia kuanzishwa kwa Jamhuri ya Cape Verde mnamo Julai 5, 1975.”

Wakati huo huo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imetoa pongezi zake za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Salim Ahmed Salim kwa kupambwa na tuzo hiyo adhimu.

"Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, inapenda kutoa shukurani zake kwa Mheshimiwa Dkt.Jose Maria Neves, Rais wa Jamhuri ya Cape Verde kwa kumuenzi miongoni mwa watoto wakubwa wa Afrika na mwanadiplomasia mashuhuri, Mheshimiwa Dkt.Salim
Ahmed Salim,"iliongeza sehemu ya taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news