ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali imejiandaa kuhakikisha Zanzibar inakuwa mstari wa mbele kuyapokea mabadiliko ya teknolojia ambayo ni msingi muhimu kwa kukuza na kuendeleza uchumi wa kisasa pamoja na kurahisisha maisha ya wananchi wa hali zote.

Ameyasema hayo leo Julai 29,2023 katika hafla ya uzinduzi wa Mkakati wa Kidijitali wa Serikali na Mfumo wa Bajeti na Matumizi Serikalini (BAMAS) uliyofanyika Hoteli ya Golden Tulip Airport, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Rais Dkt.Mwinyi amesema, matumizi ya mifumo ya TEHAMA yataleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii katika utendaji kazi wa Serikali kwa ulazima wa kutumia mifumo hiyo kwa kuwa matumizi ya TEHAMA.
Pia, yataimarisha ukusanyaji wa mapato, kurahishisha utoaji wa huduma sekta ya Afya, Elimu, kudhibiti matumizi ya fedha za umma, kukomesha vitendo vya wizi, kuzuia rushwa na ubadhirifu pamoja na kuimairisha usalama wa nchi.
Aidha, Mheshimiwa Rais amesema, mfumo wa BAMAS unaleta uwazi kwenye matumizi serikalini, utaimarisha uwajibikaji kwa watendaji wa Serikali, kuwezesha mifumo yote ya malipo na matumizi ya fedha za Serikali kusomana kwa haraka na kwa ufanisi na kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuwaletea wananchi maendeleo.