Rais Dkt.Samia atoa maagizo kwa taasisi zote za haki jinai

DAR ES SALAAM-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan amezitaka taasisi za haki jinai kufanya marekebisho ambayo hayana gharama za kifedha katika mifumo yao ya kiutendaji ili kuleta haki kwa wananchi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan akipokea Taarifa ya Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuimarisha Taasisi za Haki Jinai hapa Tanzania kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Julai 15, 2023. (Picha na Ikulu).

Rais Dkt.Samia ameyasema hayo leo Julai 15,2023 wakati akipokea taarifa rasmi ya Tume ya Kuangalia jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai hapa nchini katika hafla iliyofanyika Ikulu.

Aidha, Rais Dkt.Samia amesema, ni vyema marekebisho hayo yafanyike kabla ya mabadiliko ya kiutawala na kiufundi yanayoigharimu serikali fedha nyingi.

Rais Dkt.Samia pia ameelekeza kufanyiwe kazi masuala ya kuheshimu watuhumiwa kwenye ukamataji, upelelezi pamoja na uendeshaji wa mashtaka mbalimbali ili haki iweze kutendeka.

Vile vile, Rais Dkt.Samia amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama visitoe kipaumbele katika kukamata na kuhukumu na badala yake vijikite kuzuia kutenda makosa.

Kwa upande mwingine, Rais Dkt.Samia amevitaka vyombo vya jinai kuwa na mfumo unaosomana katika uendeshaji ili kurahisisha ufuatiliaji pamoja na kuzuia mfumo wa upelelezi kutoa mwanya wa rushwa.

Tume ya Haki Jinai iliyoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohamed Chande Othman ilikusanya maoni kutoka taasisi 12 kwa lengo la kupata ushauri na mapendekezo ya namna bora ya kuimarisha mfumo na utendaji kazi wa taasisi zinazohusika na haki jinai

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news