Rasilimali watu ni nyenzo muhimu-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika umetoa fursa ya kujadiliana na kubadilishana uzoefu wa njia na mbinu mbalimbali za kuharakisha kufikiwa kwa ufumbuzi wa kukabiliana na changamoto za rasilimali watu barani Afrika.

Ameyasema hayo Julai 26,2023 alipofunga Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali Watu (Africa Head of State Human Capital Summit) uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Rais Dkt.Mwinyi amefafanua masuala mawili ambayo yamejitokeza wakati wa mijadala na michango katika mkutano huo ikiwemo dhana ya kutumia rasilimali watu kama nyenzo ya kuongeza kasi ya maendeleo ya jamii kupitia uwekezaji kwa vijana.

Suala la pili amesema, utayari wa Afrika kuwekeza katika sekta ya elimu na mafunzo ya stadi za kazi kwa kuwawezesha vijana kuwa na ujuzi ili kufanikiwa.

Mkutano huo umehudhuriwa na Wakuu wa Nchi za Afrika akiwemo Rais wa Kenya, Mhe.William Ruto, Rais wa Msumbiji, Mhe.Filipe Nyusi, Rais wa Malawi, Mhe.Dkt. Lazaraus Chakwera.

Wengine ni Rais wa Sierra Leone, Mhe.Julius Maada Bio, Rais wa Madagascar, Mhe.Andry Rajoelina, Rais wa Sao Tome na Principe, Mhe. Carlos Manuel Vila Nova pamoja na wawakilishi kutoka nchi mbalimbali Afrika.

Awali akizungumza kwenye mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt.Stergomena Tax amesema, mkutano huo umehudhuriwa moja kwa moja na watu zaidi ya 1,000 wakiwakilisha Serikali na taasisi za kimataifa 44.

Amesema, watu wengine 1,300 wanashiriki mkutano huo kwa njia ya mtandao kupitia majukwaa tofauti na kufanya mkutano huo kushirikisha watu 2,300. Amewashukuru kwa kuupa umuhimu mkutano huo.

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inathamini ushiriki wenu viongozi wetu na inawashukuru Benki ya Dunia kwa kushirikiana nasi katika kuandaa mkutano huu. Ushirikiano huu ni ushahidi wa umuhimu wa maendeleo ya rasilimali watu na mchango wake katika kukuza uchumi na jamii katika bara letu,” amesema.

Amesema, mkutano huo umekuja wakati mwafaka ambapo Umoja wa Afrika (AU) unatekeleza Agenda2063, mpango unaolenga kuibadilisha Afrika kuwa kitovu cha nishati duniani. Kufikia lengo hili, uendelezaji wa rasilimali watu ni muhimu na hili linahitaji jitihada za pamoja.

Dkt.Tax amesema, mkutano huo unatoa fursa ya kubadilishana mawazo, uzoefu na mikakati ya ubunifu na kufungua njia kwa rasilimali watu yenye uwezo wa kuchangia maendeleo ya bara la Afrika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news